Tequila fish: Kisa cha samaki 'ambaye amekataa kutokomea'

Chanzo cha picha, Chester Zoo
"Ni samaki wadogo tu, hawana rangi nyingi - hakuna shauku kubwa katika suala la uhifadhi wa kimataifa," anaelezea Gerardo Garcia.
Spishi ambayo mhifadhi wa Chester Zoo anazungumza juu yake - samaki wa Tequila - sasa wamerudishwa porini baada ya kutangazwa kutoweka.
"Hawajaonekana" tangu 2003, wamerudi kwenye mito ya kusini-magharibi mwa Mexico.
Urejeshaji unafanywa kama mfano wa jinsi mifumo ya ikolojia ya maji baridi na spishi zinaweza kuokolewa.

Chanzo cha picha, Chester Zoo
Makao ya makazi ya maji safi ni baadhi ya yaliyo hatarini zaidi duniani, kulingana na Muungano wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN), huku viumbe vinavyotegemea maji baridi "vinatoweka kwa kasi zaidi kuliko wanyamapori wa nchi kavu au baharini".
Vitisho vikiwemo uchafuzi wa mazingira vinaendelea kuweka shinikizo, sio tu kwa wanyamapori, lakini kwa maji safi na usambazaji wa chakula ambao unategemea mito na maziwa.
Muhimu zaidi, jamii ya wenyeji - watu wanaoishi karibu na eneo la kutolewa samaki wa Tequila huko Jalisco, Mexico - wanachukua jukumu muhimu, kufuatilia ubora wa maji ya mito na maziwa.
Profesa Omar Dominguez, kutoka Chuo Kikuu cha Michoacana cha Mexico, ambaye timu yake ilichukua nafasi kubwa katika uanzishwaji upya alisema: "Hatungeweza kufanya hivi bila watu wa ndani - ndio wanaofanya uhifadhi wa muda mrefu.
"Na hii ni mara ya kwanza kwa aina ya samaki waliotoweka kuwahi kuletwa tena kwa ufanisi nchini Mexico, kwa hivyo ni hatua kuu ya uhifadhi.

Chanzo cha picha, Chester Zoo
"Ni mradi ambao sasa umeweka historia muhimu kwa siku zijazo za uhifadhi wa aina nyingi za samaki nchini ambao wanatishiwa au hata kutoweka porini, lakini ambao mara chache huzingatiwa."
Wakati wahifadhi awali waliachilia samaki 1,500, wanasema idadi ya samaki hao sasa inaongezeka katika mfumo wa mito.

Chanzo cha picha, Chester Zoo
Ni mradi - na ushirikiano - kati ya wahifadhi wa mazingira nchini Mexico na Uingereza ambao ulianza miongo kadhaa iliyopita.
Mnamo 1998, mwanzoni mwa mradi huo, wanasayansi katika Kitengo cha Biolojia ya Majini cha Chuo Kikuu cha Michoacana cha Mexico walipokea jozi tano za samaki kutoka kwa hifadhi ya wanyama ya Chester Zoo , iliyotolewa na mhifadhi wa viumbe wa majini wa Uingereza Ivan Dibble. Samaki hawa 10 walianzisha koloni mpya katika maabara ya vyuo vikuu, ambayo wataalam huko waliitunza na kuipanua kwa miaka 15 iliyofuata.
Katika matayarisho ya kurejeshwa, wanaume 40 na wanawake 40 kutoka koloni walitolewa katika madimbwi makubwa, kimsingi wakiwafunza samaki waliofugwa kwa mazingira ya porini na rasilimali za chakula zinazobadilika-badilika, washindani wanaowezekana, vimelea, na wanyama wanaowinda wanyama wengine. Baada ya miaka minne, idadi hii ilikadiriwa kuongezeka hadi samaki 10,000 na kuwa chanzo cha kurejeshwa porini.
Inatarajiwa kuwa inaweza kuwa kielelezo kwa spishi zingine za maji baridi, pamoja na spishi ya achoque - jamaa wa karibu wa axolotl anayeishi katika ziwa moja tu kaskazini mwa Mexico, na ambayo inakabiliwa na vitisho kama hivyo vya kuangamia .
Amfibia huyu wa kipekee - ambaye anaaminika katika utamaduni wa wenyeji kuwa na sifa za uponyaji - ameokolewa kutokana na kutoweka, kwa sehemu, na kikundi hapa cha watawa, ambao wanaendesha kituo cha kuzalishwa kwa wanyama.

Chanzo cha picha, Andre Gunther
"Hii inaonyesha tu," anasema Gerardo Garcia, "kwamba wanyama wanaweza kuzoea tena pori wanaporejeshwa kwa wakati unaofaa na katika mazingira yanayofaa".














