Wimbi la vifo vya wapinzani linavyoongezeka duniani

S

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Mfano wa hivi karibuni ni Anicet Ekane, kiongozi wa upinzani nchini Cameroon, aliyefariki akiwa kizuizini.
Muda wa kusoma: Dakika 4

Katika enzi ambapo demokrasia mara nyingi hutajwa kama kielelezo cha uhuru wa maoni na upinzani wa kawaida wa siasa, inaibuka wimbi la hofu. Wimbi hili ni vifo visivyotarajiwa vya wapinzani wakiwa magerezani wakiwemo walioshtakiwa kwa mashtaka ya kisiasa.

Kwa miaka ya karibuni, kumekuwapo ongezeko la ripoti za wakosoaji wa serikali, wanaharakati, na viongozi wa upinzani kukamatwa kwa tuhuma mbalimbali zingine za kisiasa na kusekwa ndani, kisha kutoweka au kufariki katika mazingira yenye utata wakiwa wanashikiliwa jela.

Zaidi ya hayo, mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu yamekuwa yakitoa tahadhari juu ya kile wanachoeleza kama kuongezeka kwa "udhalilishaji wa kimfumo dhidi ya upinzani," ambapo serikali hutumia vyombo vya dola kama mahakama, polisi, na idara za ujasusi kudhibiti au kunyamazisha sauti mbadala.

Ripoti hizo zinaonyesha kuwa katika baadhi ya nchi, kifo cha mpinzani kikiwa gerezani hakionekani kama tukio la bahati mbaya bali dalili ya muundo mpya wa kukabiliana na wapinzani muundo unaozua hofu kuhusu hali ya demokrasia katika karne ya 21.

Kutoka Afrika mpaka Asia, ni vifo tu

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Alexei Navalny, alikuwa mkosoaji mkubwa wa Rais wa Urusi Vladmir Putin na serikali yake

Katika siku za hivi karibuni, visa vya vifo vya viongozi na wapinzani wakiwa gerezani vinazidi kuchukua sura ya janga la kimataifa. Upinzi wa kisiasa na hata wakosoaji wasio wanasiasa wakiwemo wanaharakati wamekuwa wakikutwa na dhahama ya kufa gerezani. Hakuna ushahidi wa kuthibitisha vyanzo vyake lakini kufa kwao kunatia wasiwasi.

Mfano wa hivi karibuni ni Anicet Ekane, kiongozi wa upinzani nchini Cameroon, aliyefariki akiwa kizuizini. Familia na wanasheria wake wanasema alikumbwa na matatizo ya kupumua na hakupata matibabu stahiki licha ya ombi la mara kwa mara la kuomba ahamishiwe hospitali ya kiraia.

Pia ni tukio la Alexei Navalny, mpinzani mkubwa wa serikali ya Urusi, aliyefariki akiwa katika gereza lenye ulinzi mkali, Urusi. Serikali ilisema alikumbwa na mgogoro wa kiafya ghafla, lakini viongozi wa magereza walikataa kuweka wazi sababu za kifo, jambo lililizusha maswali makubwa ya kimataifa.

Zaidi ya hayo huko Amerika ya Kusini katika nchi ya Venezuela ni mfano mwingine: Alfredo Díaz, gavana wa zamani na mwanasiasa wa upinzani, alifariki Disemba 2025 akiwa gerezani katika jengo la ujasusi la serikali, El Helicoide, Caracas, ambapo familia yake na chama chake wanasema hakupata huduma ya matibabu inayotakiwa na kwamba kifo chake kinapaswa kuchunguzwa kwa uangalifu.

Hii ni baadhi tu ya mfano ya karibuni kuhusu wapinzani kufikia magerezani katika mazingira ya utata na kuashiria muendelezo wa hatari ambapo upinzani wa kisiasa unapoishia nyuma ya kuta za gereza.

Demokrasia katika mtihani?

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Alfredo Díaz, gavana wa zamani na mwanasiasa wa upinzani, alifariki Disemba 2025 akiwa gerezani katika jengo la ujasusi la serikali, El Helicoide, Caracas.

Vifo hivi na visa vingine vya mateso au kuachwa bila matibabu vinaibua swali moja gumu. Kama demokrasia inatetea uhuru wa maoni na haki ya upinzani, mbona wapinzani wanaishia gerezani, wanauawa au kupitia mateso?

Katika visa kama Ekane au Díaz, vyombo vya dola vinatumia masharti ya kisheria, ili kuwafungulia mashtaka wapinzani na mara nyingi kuyachukua kama silaha ya kisiasa dhidi ya wapinzani.

Hali ya utekelezaji wa sheria mara nyingi ni ya maamuzi, na vyombo vya utekelezaji huonekana kukosa uwazi. Hii inaashiria kwamba demokrasia inapotumiwa kama fasihi ya uwajibikaji na haki, inaweza kubadilishwa kuwa zana ya kuondoa upinzani na kuifanya sheria na vyombo vya dola kuwa kinara wa utulivu wa kisiasa, sio uhuru wa maoni.

Kwa mantiki hiyo, vifo gerezani vinaweza kuwa sehemu ya mchakato mkubwa wa "kupunguza upinzani" na kuwatisha viongozi wa upinzani.

Nini hatma ya upinzani?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa hali kama hii, hatima ya upinzani inaonekana kuwa tete hasa pale vyombo vya dola vinaposhikana na vyombo vya siasa na misingi ya demokrasia. Wapinzani wanaweza kukumbwa na kashfa, kukamatwa, kutupwa mbaroni, kufungwa vifungo virefu au kuwekwa ndani muda mrefu, na hata kufa hata kama hawajafanya uhalifu wowote.

Ili upinzani wa kweli uweze kuishi, ni lazima kuwe na uwazi katika vyombo vya dola, uhuru kamili wa vyombo vya sheria na mahakama, haki za mawasiliano na habari, na ulinzi wa haki ya kisiasa bila hofu. Bila hayo, maoni mbadala kwa serikali, hata yenye nia njema, ina hatari ya kuzimwa na demokrasia itabakia jina tu.

Kwa upande mwingine, jamii yenye upinzani imara ndiyo msingi wa maendeleo endelevu, kwa kuwa sauti mbadala huchochea uwajibikaji, ubunifu wa sera, na uwiano wa nguvu kati ya watawala na wananchi. Kadiri nafasi hizi zinavyofifia, ndivyo hofu ya wananchi huongezeka na kuathiri uwezo wao wa kushiriki katika masuala ya nchi yao.

Mwisho wa yote, mustakabali wa upinzani utategemea kiwango ambacho serikali ziko tayari kujenga mazingira ya ushindani wa kisiasa usio na visasi. Bila kuimarishwa kwa taasisi huru, kulindwa kwa haki za binadamu, na kupunguzwa kwa matumizi ya nguvu dhidi ya wakosoaji, hatima ya upinzani itaendelea kuwa simulizi ya kuhuzunisha, vifo vyao magerezaji vitazidi kushika kasi na mustakabali wa demokrasia utazidi kutetereka.