Viongozi 6 maarufu duniani waliowahi kuwekewa sumu

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Alexander Litvinenko
Muda wa kusoma: Dakika 6

Madai ya hivi karibuni nchini Tanzania kuhusu jaribio la kumuwekea sumu kiongozi wa upinzani Tundu Lissu, yamezua mijadala mikali na kuibua maswali kuhusu hatima ya viongozi wa upinzani duniani na hata wengine wa kisiasa.

Chama kikuu cha upinzani Tanzania, Chadema, mnamo Julai 03, 2025, kilidai kupokea taarifa zinazodai kuwa Mwenyekiti wake taifa, Tundu Lissu, ana mpango wa kuwekewa sumu akiwa kizuizini.

Taarifa hiyo ilimnukuu David McAllister, kiongozi mwandamizi wa Bunge la Ulaya, aliyedai kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter) kwamba: "Nina wasiwasi mkubwa kuhusu ripoti za kutisha za jaribio la kumtilia sumu kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu akiwa kizuizini."

Serikali ya Tanzania, kupitia kwa msemaji wake, Gerson Msigwa, ilikanusha taarifa hizo vikali, ikisema "haijawahi kuwa na mpango wa kumwekea sumu mtu yeyote aliyepo gerezani wala haina mpango wa kufanya hivyo kwa mtu yeyote."

Matukio ya watu maarufu ama wapinzani wanaopingana vikali na serikali kudaiwa kupewa sumu huvuta hisia za wengi. Hawa hapa ni watu sita mashuhuri ambao wanadaiwa kupewa sumu kutokana na misimamo yao.

Baadhi ya visa hivi, uchunguzi bado unaendelea au hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai ya sumu.

1. Yasser Arafat - Palestina

Yasser Arafat

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Yasser Arafat

Yasser Arafat, kiongozi wa kihistoria wa Palestina na Mwenyekiti wa Shirika la Ukombozi wa Palestina (PLO), alifariki dunia nchini Ufaransa mnamo Novemba 11, 2004, akiwa na umri wa miaka 75. Kifo chake kilitokea baada ya kuugua ghafla kwa wiki kadhaa na kulazwa katika hospitali ya kijeshi ya Percy huko Paris. Ingawa rekodi rasmi za matibabu zilionyesha alifariki kutokana na kiharusi kilichotokana na shida ya damu, uvumi ulienea haraka kuwa alikuwa amepewa sumu.

Baada ya kifo chake, familia yake na wengine walishinikiza uchunguzi zaidi. Mnamo 2012, sampuli kutoka kwenye mwili wake zilichukuliwa na kuchunguzwa na wataalamu kutoka Uswisi, Ufaransa, na Urusi. Ripoti ya Uswisi, iliyopatikana na Al-Jazeera, ilionyesha viwango vya juu vya Polonium-210, dutu ya mionzi, katika sampuli hizo, ikipendekeza uwezekano wa sumu.

Hata hivyo, matokeo hayakuwa ya uhakika na yalipingwa na ripoti nyingine za kisayansi. Hakuna ushahidi thabiti uliowahi kupatikana kuthibitisha kuwa aliuawa kwa sumu, na Israeli imekanusha vikali kuhusika kwake. Kifo chake kinaendelea kuwa mada ya mjadala mkali na nadharia mbalimbali, na hadi leo, ukweli kamili wa kifo chake umejaa utata.

2. Alexei Navalny - Urusi

Alexei Navalny

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Alexei Navalny
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Alexei Navalny, mwanasiasa mashuhuri wa upinzani nchini Urusi na mkosoaji mkubwa wa utawala wa Rais Vladimir Putin, alidaiwa kupewa sumu ya Novichok mnamo Agosti 20, 2020, ambayo ni hatari kwa mifumo ya fahamu, iliyotengenezwa enzi za zama za Sovieti.

Alipoteza fahamu akiwa kwenye ndege kuelekea Moscow kutoka Tomsk, Urusi, na ndege hiyo ilifanya kutua kwa dharura huko Omsk ambapo alilazwa hospitalini akiwa katika hali mbaya. Baadaye, alihamishwa kwa matibabu nchini Ujerumani, ambapo alikuwa hajitambua, ili kusaidia kumuokoa. Ilithibitishwa na maabara tano zilizoidhinishwa na Shirika la kuzuia silaha za kemikali (OPCW), kuwa alikuwa na sumu ya Novichok mwilini.

Tukio hili lilisababisha mshtuko mkubwa duniani na kulaaniwa vikali na mataifa ya Magharibi, ambayo yaliishutumu serikali ya Urusi kwa kuhusika moja kwa moja. Kremlin imekanusha vikali madai hayo, ikiyaita ya kisiasa.

Navalny alipata nafuu kiasi Septemba 7, 2020, na aliruhusiwa kutoka hospitalini Septemba 22, 2020. Licha ya hatari iliyokuwepo, Navalny alirejea Urusi mnamo Januari 2021, ambapo alikamatwa mara moja na kufungwa jela kwa mashtaka ya ubadhirifu na kudharau Mahakama, mashtaka ambayo yeye na wafuasi wake waliyaita ya kisiasa.

Alifariki dunia mnamo Februari 16, 2024, akiwa gerezani, chini ya mazingira yanayoendelea kuibua maswali na shutuma za kimataifa.

3. Viktor Yushchenko - Ukraine

Viktor Yushchenko

Chanzo cha picha, ABC

Maelezo ya picha, Viktor Yushchenko

Viktor Yushchenko, kiongozi wa upinzani na mgombea urais wa Ukraine, alipatiwa matibabu baada ya kubainika kuwa Dioxin, kemikali yenye sumu kali mwilini, wakati wa kampeni za uchaguzi mnamo Septemba 2004. Sumu hiyo ilisababisha mabadiliko makubwa na ya kutisha usoni mwake, akipata makovu na uvimbe, pamoja na matatizo makubwa ya kiafya yanayoendelea. Yushchenko alikuwa mpinzani mkuu wa Viktor Yanukovych, mgombea aliyekuwa anaungwa mkono na Urusi, katika uchaguzi uliokuwa na mvutano mkubwa.

Madai ya sumu yaliibua kashfa kubwa na kuongeza mvutano wa kisiasa nchini Ukraine, huku baadhi ya madaktari wa Austria waliodaiwa kulazimishwa kuacha kazi zao baada ya kutilia shaka madai ya hospitali yao kuhusu sumu hiyo, jambo lililoleta utata zaidi.

Licha ya uchunguzi kufanyika, suala hili halijatatuliwa kikamilifu na hakuna mtu aliyewahi kufunguliwa mashtaka kwa jaribio hilo la mauaji. Hata hivyo, Yushchenko alinusurika na hatimaye alishinda uchaguzi wa urais, na alihudumu kama Rais wa Ukraine kuanzia 2005 hadi 2010, huku kovu za sumu zikiendelea kuwa ukumbusho wa shambulio hilo.

4. Alexander Litvinenko - Urusi

Alexander Litvinenko

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Alexander Litvinenko

Alexander Litvinenko, aliyekuwa afisa wa Shirika la kijasusi la Urusi (FSB) na baadaye akawa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Urusi, alifariki dunia nchini Uingereza mnamo Novemba 23, 2006. Kifo chake kilitokana na sumu kali ya Polonium-210, na kumfanya kuwa mtu wa kwanza kuthibitishwa kufa kutokana na sumu hiyo.

Litvinenko alikuwa amekimbilia Uingereza kutafuta hifadhi ya kisiasa mnamo 2001, na alikuwa akijihusisha na kuandika vitabu akifichua madai ya ufisadi na uhalifu ndani ya FSB, ikiwemo kudai kuwa FSB ilihusika katika milipuko ya majengo ya Moscow mnamo 1999.

Kabla ya kifo chake, Litvinenko alitoa madai ya wazi akiwa hospitalini kwamba Rais Vladimir Putin alikuwa nyuma ya yeye kupewa sumu, Uingereza pia ilihusisha hilo, madai ambayo Urusi imeyakanusha vikali.

Kifo chake kiliibua mvutano mkubwa wa kidiplomasia kati ya Uingereza na Urusi, na kusababisha kufukuzwa kwa wanadiplomasia kutoka nchi zote mbili. Simulizi yake imekuwa mada ya filamu na vitabu vingi, ikisisitiza mazingira hatarishi wanayokabiliana nayo wakosoaji wa serikali nchini Urusi.

5. Khaled Mashal - Hamas

Khaled Mashal - Hamas

Chanzo cha picha, Khaled Mashal

Maelezo ya picha, Khaled Mashal

Khaled Mashal, kiongozi mkuu wa kisiasa wa kundi la wanamgambo wa Palestina la Hamas, alinusurika jaribio la kuuawa kwa sumu mnamo Septemba 25, 1997, huko Amman, Jordan. Jaribio hilo lilifanywa na mawakala wawili wa Mossad, shirika la ujasusi la Israeli, ambao walimwagia sumu inayodhaniwa kuwa ni Levofentanyl kwenye sikio lake. Lengo lilikuwa kumuua Mashal, ambaye alikuwa akiongoza operesheni za Hamas kutoka nje ya maeneo ya Palestina.

Operesheni hiyo ya siri ilishindwa baada ya mawakala hao wa Israeli kukamatwa na polisi wa Jordan. Kukamatwa kwao kulisababisha mgogoro mkubwa wa kidiplomasia, na Mfalme Hussein wa Jordan alishinikiza Israeli kutoa dawa ya kuzuia sumu hiyo ili kuokoa maisha ya Mashal, akitishia kuvuruga uhusiano wa amani kati ya nchi hizo mbili.

Hatimaye, Israeli ililazimika kutoa dawa hiyo na kuwaachilia wafungwa kadhaa wa Kipalestina, ikiwemo mwanzilishi wa Hamas, Sheikh Ahmed Yassin, kama sehemu ya makubaliano ya kuwaachia majajusi wake. Tukio hili lilionyesha mbinu za hatari za ujasusi na lilisababisha kumdhoofisha Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu wakati huo.

6. Kim Jong-nam - Korea Kaskazini

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Kim Jong-nam, kaka wa kambo wa kiongozi wa sasa wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un, aliuawa kikatili kwa sumu ya VX, kemikali ya mishipa ya fahamu iliyoainishwa kama silaha ya kemikali, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kuala Lumpur, Malaysia, mnamo Februari 13, 2017. Alishambuliwa na wanawake wawili ambao walimwagia kemikali hiyo usoni mwake wakati akisubiri ndege. Kifo chake kilitokea haraka kutokana na ukali wa sumu hiyo ya VX.

Uchunguzi uliofanywa na mamlaka ya Malaysia ulihitimisha kuwa shambulio hilo lilipangwa na serikali ya Korea Kaskazini, ingawa Pyongyang ilikanusha vikali kuhusika. Wanawake hao waliodaiwa kuwa walidanganywa kufanya hivyo wakiamini walikuwa wakishiriki katika onyesho la vichekesho, walikamatwa na kufunguliwa mashtaka, ingawa baadaye mmoja wao aliachiliwa na mwingine alipewa kifungo kifupi.

Kifo cha Kim Jong-nam, ambaye alikuwa amejikita katika maisha ya uhamishoni na kuikosoa familia yake ya kitawala, kiliibua mshtuko wa kimataifa na kuangazia ukatili na mbinu za siri zinazotumiwa na serikali ya Korea Kaskazini dhidi ya wale wanaowaona kama tishio.