Idadi ya watu wa India kuzidi China ifikapo katikati ya 2023 - UN

Watu

Chanzo cha picha, Getty Images

India iko tayari kuipiku China na kuwa nchi yenye watu wengi zaidi duniani, data iliyotolewa na Umoja wa Mataifa inaonesha.

Idadi ya watu nchini India inakadiriwa kufikia milioni 1,428.6 dhidi ya milioni 1,425.7 ya China ifikapo katikati ya mwaka.

Hii inaonesha India itakuwa na watu milioni 2.9 zaidi ya jirani yake wa Asia.

China ina zaidi ya watu bilioni 1.4 kila moja, na wamechukua zaidi ya theluthi moja ya idadi ya watu ulimwenguni kwa zaidi ya miaka 70.

Idadi ya watu nchini India, hata hivyo, ni makadirio kwani hakujakuwa na Sensa nchini baada ya mwaka 2011.

Pia, Umoja wa Mataifa unasema makadirio yao hayajumuishi idadi ya wakazi wa Mikoa miwili ya Utawala Maalum ya China - Hong Kong na Macau - na kisiwa cha Taiwan, ambacho Beijing inakiona kama jimbo lililojitenga kuunganishwa na bara siku moja. Lakini Taiwan inajiona kuwa tofauti na China, ikiwa na katiba yake na viongozi waliochaguliwa kidemokrasia.

Mnamo Novemba, idadi ya watu ulimwenguni ilivuka bilioni 8. Lakini wataalamu wanasema ukuaji si wa haraka kama ilivyokuwa zamani na sasa uko katika kiwango cha polepole zaidi tangu 1950.

India na China zimeshuhudia kupungua kwa viwango vyao vya uzazi. Nchini China, idadi ya watu ilianza kupungua mwaka jana, licha ya nchi hiyo kutelekeza sera yake ya mtoto mmoja mwaka 2016 na kuanzisha motisha kwa wanandoa kupata watoto wawili au zaidi.

Nchini India pia, viwango vya uzazi vimepungua kwa kiasi kikubwa katika miongo ya hivi karibuni kutoka kwa uzazi 5.7 kwa kila mwanamke mwaka wa 1950 hadi uzazi 2.2 kwa kila mwanamke leo.

Utafiti ulioidhinishwa na UNFPA ulikuwa na Wahindi wengi wakisema kuwa idadi ya watu katika nchi yao ilikuwa kubwa mno na viwango vya uzazi vikubwa mno.

Takribani watu wawili kati ya watatu waliohojiwa walibainisha masuala ya kiuchumi kama mambo yanayowasumbua sana wanapofikiria kuhusu ongezeko la watu.

Wanademografia, hata hivyo, wanasema idadi ya watu wa India wanaoipita China haipaswi kuonekana kama suala la wasiwasi na tahadhari dhidi ya kutoa wasiwasi juu ya idadi inayoongezeka.

"Badala yake, zinapaswa kuonekana kama ishara ya maendeleo, na matarajio ikiwa haki za mtu binafsi na chaguzi zinazingatiwa," ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema.