Clemence Mtenga:Familia ya Mtanzania aliyefariki Gaza yazungumza

TH

Chanzo cha picha, MASHAV ISRAEL

Na Alfred Lasteck

BBC Dar es Salaam

Familia ya Marehemu Clemence Mtenga inasubiri Serikali ifanye taratibu za usafirishaji wa mwili wa marehemu kutoka nchini Israel ili waweze kufanya maziko.

Clemence alikuwa miongoni mwa wanafunzi wawili kutoka Tanzania ambao Serikali ya Israeli hapo awali ilithibitisha kuwa walitekwa na kundi la Hamas baada ya shambulio la Oktoba 7.

Akizungumza na BBC, Msemaji wa familia ya marehemu, Boniface Mtenga alisema kuwa kwa sasa hakuna wanachoweza kukifanya mpaka pale serikali itakapowaambia lini mwili utakapofika nchini kwa ajili ya maziko.

Mtenga alisema, “Tulipata taarifa ya kifo cha kijana wetu siku ya Ijumaa, ambapo Mkuu wa Wilaya ya Rombo alifika nyumbani akiwa na ujumbe huo kutoka kwa serikali…

“…Tulipokea taarifa hiyo kwa majonzi kwasababu tumeondokewa na kijana wetu ambaye ndio kwanza alianza kupambania ndoto zake za maisha. Kwa sasa hatuna cha kufanya mpaka pale serikali itakapotuletea mwili kwa ajili ya maziko,” alisema Mtenga na kuongeza kuwa wanatarajia kuwa leo watapata taarifa rasmi ya lini mwili utakapowasili.

Serikali kuthibitisha kifo chake

TH

Chanzo cha picha, COURTESY

Ijumaa iliyopita, Serikali ya Tanzania ilitangaza kuwa Clemence, mwanafunzi mwenye miaka 22, ndiye aliyefariki.

Kwenye taarifa yake, serikali ilieleza kuwa inaendelea kuwasiliana na Israel juu ya taarifa za Mtanzania mwingine, Joshua Mollel ambaye bado anashikiliwa mateka.

Kwa mujibu wa Israel, jumla ya watu 230 walichukuliwa mateka baada ya shambulio la Oktoba 07. Mateka hao, ambao walipelekwa katika ukanda wa Gaza na wanatoka katika mataifa 25 tofauti, ikiwemo raia mmoja wa Afrika Kusini ambaye hadi sasa hajatambulika.

Safari ya kwenda Israel

Kwa mujibu wa familia, Clemence aliondoka nchini Tanzania Septemba mwaka huu ambapo alienda nchini Israel kushiriki mafunzo ya kilimo biashara kwa utaratibu ulio chini ya mpango wa ushirikiano kati ya serikali za Tanzania na Israel.

Kijana huyo ni miongoni mwa wanafunzi wa kitanzania 260 waliokuwa nchini humo kwaajili ya masomo ya vitendo katika eneo la kilimo.

Imehaririwa na Yusuf Jumah