Mwili wangu tu ndio uko hai - Walibya bado wanaomboleza mwaka mmoja baada ya mafuriko

Chanzo cha picha, Abdul Aziz Aldali
- Author, Marco Oriento
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Taswira ya mafuriko makubwa yaliyokumba mji wa pwani wa Libya wa Derna, na kuua maelfu ya watu, iko katika kumbukumbu za wale walionusurika mwaka mmoja baadaye.
“Maisha yalisimama. Ni mwili tu ambao bado uko hai. Mimi si mtu yule wa kitambo,” anasema Abdul Aziz Aldali, mkazi mdogo.
Alimpoteza mama yake, baba na wapwa wake, ambao walikuwa wamekuja kwa ajili ya kulala nyumbani kwao, wakati kimbunga Daniel kilipotua jijini humo usiku wa 10 Septemba.
"Ninawachukulia kuwa wafia imani. Majirani zangu, familia ya Nasser, walipoteza wafia dini 24. Maji yaliwafikia kwanza," Bw Aldali asema.
Derna imejengwa kwenye kingo za mto Wadi Derna. Mto huo unapitia kwenye mabwawa mawili kabla ya kuvuka jiji na kumwaga maji yake baharini.
Mvua kubwa zisizokuwa na msimu - ziliharibu miundomsingi iliyozeeka - mabwawa, yalijaa maji na hatimaye kupasuka mwendo wa saa 02:00 kwa saa za ndani tarehe 11 Septemba.
Maji yalijaa sakafuni kwa chini ya sekunde moja. Maji yalikuwa yanaingia nyumbani kwenye giza,” Bw Aldali anakumbuka.
“Maji yalikuwa yakinipeleka juu na chini. Ninaogelea vizuri sana, lakini ni vigumu kudhibiti maji yanapoendelea kuwa mengi.”
Hatimaye, mawimbi yalinitoa nje.
"Niliona mnara wa mtandao. Wimbi lilikuja na kunisukuma kuelekea huko, kwa hivyo nilishikilia na kujaribu kujiokoa kadri nilivyoweza.
Mafuriko yalipiga jiji kwa nguvu inayokadiriwa ya tani milioni 24, bila kumwacha mtu yeyote.
"Nilishuhudia watu - watoto wadogo ambao hawakuweza kujiokoa wakisombwa na maji. Wale waliobahatika kuishi walijiokoa,” Bw Aldali anakumbuka.

Chanzo cha picha, Abdul Aziz Aldali
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kama wakazi wengine wengi, Bw Aldali ameondoka jijini. Sasa amehamia Umm al-Rizam, kijiji cha kailicho umbali wa dakika 40 kuelekea kusini mwa Derna.
Zaidi ya watu 5,900 walifariki, kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (Ocha), na wengine 2,380 wanaripotiwa kutoweka katika jiji hilo lenye wakazi 90,000.
Wenyeji wanaamini kuwa idadi ya watu waliofariki katika mafuriko hayo ni kubwa zaidi.
“Karibu marafiki zangu wote walipoteza mtu wa familia. Watu wa Derna wanaamini zaidi ya 10,000 walikufa katika mafuriko,” anasema mwandishi wa habari wa Dernawi Johr Ali, ambaye sasa anaishi katika mji mkuu wa Uturuki, Istanbul, na amekuwa akifuatilia matukio katika mji wake wa asili.
Kulingana na baadhi ya watu wa Derna, kiwewe cha mkasa huo kinachangiwa na kutokuwa na uhakika wa kutojua hatima ya jamaa zao waliopotea.
"Nilipata tu [miili] ya wapwa wangu," anasema Bw Aldali. "Dunia hii haina thamani bila wazazi wangu. Namuomba Mwenyezi Mungu tu aniunganishe nao mbinguni”.
Mamlaka ya pamoja ya Kuwatafuta na Kuwatambua Watu Waliopotea (Gasimp) imetumia muda wa miezi 12 iliyopita kukusanya sampuli za DNA kutoka kwa mabaki ya binadamu kwa matumaini ya kupata mlinganisho na wanafamilia walionusurika.
"Tuliikusanya miili hiyo, tukachukua sampuli za meno na mifupa mingine, tukatoa ripoti kuhusu chanzo cha kifo, na kuzika miili," mkurugenzi wa Gasimp Dk Kamal Sewi anasema.
Lakini kupata mabaki ya waathiriwa imekuwa ngumu, na baadhi ya viungo vya mwili vilipatikana ubali wa hadi kilomita 60 kutoka baharini au chini ya majengo yaliyoporomoka.
Makaburi maalum yamejengwa kwa ajili ya wahanga nje kidogo ya jiji la Derna, lakini makaburi hayo bado hayana jina kwa sababu miili mingi haijatambuliwa rasmi, na hivyo kuacha maelfu ya familia na huzuni ya kutowaaga wapendwa wao.
Nambari za mawasiliano huwekwa ndani na nje ya kila eneo la kuzikia. Hawa hatimaye watapewa jina ikiwa DNA ya marehemu italingana na ya jamaa aliye hai.
Hata hivyo, ukubwa wa uhamishaji uliosababishwa na mafuriko umefanya hatua hii ya utambuzi kuwa ngumu.
"Ni rahisi kulinganisha sampuli za DNA kutoka kwa jamaa moja kwa moja kama wazazi au ndugu," Dk Sewi anasema, lakini kupata wanafamilia hao wa karibu imekuwa changamoto.
"Watu walihama kutoka jijini kwa sababu hawana nyumba tena, lakini hawakuja kuripoti kupotea kwa jamaa zao," Dk Sewi anasema.
Hii imechelewesha zaidi mchakato wa utambuzi kwa sababu timu zinapaswa kutafuta jamaa wa kizazi cha pili au cha tatu, ambayo inafanya ulinganishaji wa DNA kuwa mgumu zaidi.
"[Utambulisho] sio mchakato ambao utachukua mwezi mmoja au miwili kukamilika," Dk Sewi anasema.
Lakini wakati maisha ya watu wengi wa Derna yanabakia katika hali duni wanaposubiri habari za wapendwa wao, ujenzi wa jiji hilo unaendelea.

Chanzo cha picha, Moataz Fadil
Barabara zimesafishwa, shule na misikiti inakarabatiwa, na nyumba mpya zimeanza kujengwa.
Majengo yanayoitwa ya Korean Building yanaonekana.
Kazi ujenzi imekamilika zaidi ya muongo mmoja baada ya serikali ya mtawala wa wakati huo Muammar Gaddafi kuagiza kampuni ya Korea Kusini kujenga jengo hilo.
Kazi ya ujenzi ilisitishwa baada ya kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo 2011, lakini ilianza tena baada ya mafuriko.
Baadhi ya familia zilizokimbia makazi pia zimerejea Derna, zimevutiwa na fursa ya kupokea fidia ya hadi dola 21,000 na kodi ya ruzuku.
Lakini msaada wa kifedha kwa baadhi ya familia - pamoja na juhudi za ujenzi - umecheleweshwa na vikwazo vya ukiritimba, na madai ya usimamizi mbaya wa kifedha.
Chanzo cha shirika la habari la uchunguzi la The Sentry kiliiambia BBC kwamba mchakato huo ulionekana "kutokuwa wazi", na hauna sheria wazi.
"Baadhi ya familia zilizofikiri kuwa zinastahiki bado zinasubiri kufidiwa," aliongeza.
Pia wasiwasi unaoongezeka kwamba wahanga wa mafuriko hayo wamekuwa vinara katika mzozo wa madaraka kati ya serikali pinzani za Libya - zenye makao yake makuu katika mji mkuu, Tripoli, na katika mji wa mashariki wa Bengazi.
Belqasem Haftar - mtoto wa shujaa wa kijeshi Jenerali Khalifa Haftar, ambaye anatawala sehemu ya mashariki ya Libya - anaongoza juhudi za uokoaji kupitia Mfuko wa Ujenzi wa Derna,

Chanzo cha picha, Getty Images
Zaidi ya dola bilioni mbili za kimarekani zilizotengewa mradi huo, inawapa ndugu wa Haftar ushawishi mkubwa kupanua wigo wao kwa nguvu.
"Ni hundi tupu isiyo na uangalizi wowote," mchambuzi wa Libya Anas El Gomati, ambaye anaongoza taasisi ya Sadeq Institute, aliliambia shirika la habari la AFP.
Msemaji wa Jeshi la Kitaifa la Jenerali Hatar hakujibu ombi la BBC la kutoa maoni yake.
Chanzo cha The Sentry, ambacho kilipendelea kutotajwa jina kwa sababu ya unyeti wa suala hilo, kilidokeza kwamba gavana wa benki kuu ya Libya aliikimbia nchi hiyo baada ya kutofautiana na serikali huko.
"Pesa zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Derna zilichangia kuifanya benki kuu ya Tripoli kuwa karibu na familia ya Haftar, lakini serikali ya Tripoli ilikuwa na uchungu dhidi ya hili," aliongeza.
Mapambano ya kuwania madaraka na machafuko yanapoendelea, wakazi wa Derna kama Bw Aldali wanajizatiti kujenga upya maisha yao.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












