Miili iliyoachwa bila kutambuliwa na mafuriko ya Libya

Chanzo cha picha, Reuters
Onyo: Taarifa hii ina maelezo ambayo huenda ikiwaathiri baadhi ya wasomaji.
Daktari aliyevalia barakoa anainama chini kwenye mfuko mweusi wa plastiki, na kusogeza kwa upole miguu ya mtu aliye ndani. "Kwanza tunabaini umri, jinsia na urefu," anaelezea.
"Yuko katika hatua ya kuoza sasa, kwa sababu ya maji."
Katika maegesho ya hospitali katika mji wa Derna, mashariki mwa Libya, taarifa za mwisho za mmoja kati ya waathiriwa kadhaa zinaangaliwa kwa uangalifu na kurekodiwa.
Hii ni moja ya kazi muhimu zaidi hapa, na moja ya kazi ya kufadhaisha zaidi. Mtu huyo hatambuliki baada ya kuwa baharini kwa wiki moja. Mwili wake ulipatikana ufukweni asubuhi hiyo.
Mikono ya kitaalam inachunguza kwa upole, ikitafuta alama za kutambua na kuchukua sampuli ya DNA. Hiyo ni muhimu, ikiwa jamaa zake wameponea maafa wanaweza kumdai.

Ni rasmi zaidi ya watu 10,000 hawajulikani waliko, kulingana na takwimu za Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu.
Shirika la misaada la Red Crescent limekuwa likitoa takwimu zake.
Umoja wa Mataifa unasema idadi ya vifo ni 11,300 kufikia sasa na kwamba idadi kamili ya maafa haijulikani - ingawa jambo moja ambalo ni hakika ni ukubwa wa janga hili.
Mohammed Miftah anajua moyoni mwake familia yake ni miongoni mwa wahanga.
Alipoenda kuwatafuta dada yake na mumewe nyumbani kwao baada ya mafuriko, alikuta nyumba yao ilikuwa imesombwa na maji.
Hajapokea mawasiliano yoyote kutoka kwao tangu wakati huo. Ananionyesha video aliyoichukua wakati kijito kilipanda, maji ya rangi ya kahawia yakimiminika kupitia mlango wake wa mbele.
Huku misaada ya kimataifa ikianza kuwasili kwa kasi, Waziri wa Afya wa serikali ya mashariki ya Libya ametangaza kuwa waokoaji wanne wa Ugiriki wamefariki katika ajali iliyotokea kwenye barabara ya kuelekea Derna.
Wengine 15 walijeruhiwa. Walikuwa njiani kujiunga na timu ambazo tayari ziko uwanjani kutoka Ufaransa na Italia.
Kuwait na Saudi Arabia pia zimesafirisha tani za vifaa vya ziada.

Hatua inayofuata ni kuhakikisha kuwa zinatumika ipasavyo na kwa haki.
Abdullah Bathily, Mkuu wa Ujumbe wa Kimataifa wa Msaada wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, aliiambia BBC Arabic kuwa nchi hiyo sasa inahitaji kubuni utaratibu wa uwazi wa kusimamia michango yake yote ya kimataifa.
Ni wasiwasi unaotokana na changamoto zinazojulikana za uratibu kati ya serikali ya Tripoli ambayo inatambulika kimataifa, na serikali ya mashariki mwa Libya, ambayo inapigania nafasi yake.

Tukirejea Derna kuna maeneo ambayo yamezingirwa na matope na uchafu ambao umefunika jiji hili.
Kwenye kona moja ya barabara, mamia ya nguo za rangi tofauti zimetawanyika katika mirundo.
Kando ya barabara kuna foleni kubwa huku mafuta yakigawiwa kwa walionusurika.
Michango inapoendelea kuja, mwanamume mmoja anawasili na kuweka sanduku la mitandio moto miguuni mwa mwanamke mzee.
Anambusu kichwa chake kwa upole, huku akitabasamu na kuanza kuchagua moja.
Hawa ni Walibya wanaowasaidia Walibya katika moja ya wakati wao mbaya zaidi wa shida.













