Yanayotokea ndani ya jela ya siri Libya: 'Kuwa hai ni muujiza'

Walid Al-Hudayri
Maelezo ya picha, Mfanyakazi wa zamani wa serikali ya Libya Walid Al-Hudayri

Mnamo Oktoba 1, 1990, Walid Al-Hudayri aliitwa kufanya tafsiri katika mkutano na mabalozi kadhaa katika mji mkuu, Tripoli.

Baada ya mkutano kumalizika, Al-Hudayri anakumbuka akitembea na balozi wa Congo na kumpeleka kwenye gari lake akimpa kwaheri, kisha akarudi kwenye chumba cha mkutano kukusanya vitu vyake. "Wakati huo, nilikuta na watu wananisubiri.

Walinipiga na kunipiga makofi, na kunishikia bunduki tumboni. Baada ya hapo, wakanifinika uso na kuniteka nyara. Sikujua tena nilipokuwa ", Walid Al-Hudayri anasema.

Wanaume hao wanne, wakiwa wamevalia mavazi ya kawaida, walikuwa wametumwa na idara za ujasusi na, Al-Hudayri anasema, alipelekwa katika moja ya magereza ya siri ya Tripoli, ambayo wakati mwingine yanasimamiwa na vikundi vya wanamgambo wanaodhibiti maeneo mengi ya mji mkuu.

Tukio la kutoweka kwa watu limeangaziwa sana na Umoja wa Mataifa baada ya mapinduzi ya 2011, ambayo yalisababisha kupinduliwa kwa kiongozi wa muda mrefu Muammar Gaddafi, na kuiingiza nchi katika machafuko. "Kwa muda wa siku 47, hakuna aliyejua nilikuwa wapi", Al-Hudayri anasema.

Siku na wiki baada ya kutekwa kwake zilikuwa kama kimbunga. Al-Hudayri alishutumiwa kwa kujaribu kutafuta siri za kijeshi, akawekwa mahali peke yake, kisha kuhamishiwa eneo jingine, kuteswa, na kunyimwa mambo yote ya maisha ya kawaida. Al-Hudayri anaendelea kusema, "Walininyima maji kwa siku tatu mfululizo, na walikuwa wakija kunipiga mgongoni mara tatu kwa siku. Hawakuniuliza kitu chochote.

Baada ya takribani wiki mbili, hatimaye kuhojiwa kwa Hudayri kulianza, na kupigwa kwake kulikomeshwa kwa kiasi kikubwa. Akapelekwa kwa mwendesha mashitaka, na mwezi mmoja baadaye, katikati ya Novemba mwaka wa 2020, yeye na mwenzake ambaye pia aliwekwa kizuizini walihamishiwa kwenye gereza la al-Rweimi katika kitongoji cha Ain Zara mjini Tripoli.

Muammar Gaddafi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kupinduliwa kwa Muammar Gaddafi mwaka 2011 kuliibua matumaini ya maisha bora nchini Libya.

Wakati alipowekwa kizuizini, Al-Hudayri alikuwa amefanya kazi katika idara ya tafsiri ya Wizara ya Mambo ya Nje kwa miezi michache tu.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Al-Hudayri alikuwa mwajiriwa mwenye malengo na aliyesomea teknolojia ya habari na haki za binadamu, na hivi karibuni alikuwa ameteuliwa kuwa mkuu wa idara ya mawasiliano na teknolojia ya habari, cheo ambacho kumbe kingemgharimu zaidi ya thamani ya nafasi hiyo.

Awali, Al-Hudayri alishutumiwa kwa "kukiuka mfumo wa habari za siri wa wizara hii".

Vyombo vya habari viliripoti kuwa aliwekwa kizuizini katikati ya Oktoba 2020, na kuchapisha taarifa iliyotegemea ile iliyotolewa na Ofisi ya mwendesha mashtaka wa serikali iliyoelezea kuwa amekamatwa na idara ya upelelezi.

Kisha yeye na mwenzake Sufyan Mrabet, mfanyakazi katika Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika wizara hiyo, baadaye walituhumiwa kwa "kutumia njia za mawasiliano kwa lengo la kupata siri za wizara ya ulinzi".

Al-Hudayri pia alishutumiwa kwa kuweka mifumo kwenye kompyuta (seva) ya wizara hiyo iliyounganishwa na seva nyingine ya nchini Ufaransa, ambapo baba yake anafanya kazi kama balozi.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa ilikanusha kutoa maoni kuhusu kesi hiyo. Mrabet aliwekwa gerezani wakati sawa na Al-Hudayri, na

wawili hao waliachiwa huru mwezi Januari mwaka huu, baada ya takribani miezi 15.

Al-Hudayri, anaelezea kilichotokea kama "njama", na anamtuhumu mkurugenzi wa zamani wa Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wakati huo - mtu anayemuelezea kama "mwenye ushawishi mkubwa mjini Tripoli" - kwa kuwa nyuma ya mashitaka ya "uongo" yaliyosawishwa dhidi yake, katika jaribio, alisema, la kumzuia kuwa mkuu wa idara ya ICT, cheo ambacho huwa na mazuri mengi.

Baada ya miezi kadhaa ya kampeni ya familia yake, wanasheria wake, na Kamati ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu nchini Libya, ambayo yeye alikuwa akishiriki, mahakama iliamua kwamba tuhuma hizo "hazina msingi wowote au kisheria, lakini zilikuwa (matokeo ya) ugomvi kati yake na wenzake kazini".

Pia katika kutupiliwa mbali kwa kesi hiyo, ilisemekama kuwa Al-Hudayri na Mrabet walilazimishwa kukiri chini ya ulinzi mkali, walikabiliwa na ukandamizaji wa kimwili na kisaikolojia, na "walitekwa nyara na kupelekwa mahali ambapo hakuna aliyejua walipokuwa, jambo ambalo lilisababisha familia zao kuwasiliana na Ofisi ya mwendesha Mashitaka ya Umma na kuwasilisha ripoti za wao kutojulikana walipo".

Hukumu hiyo pia ilisema kuwa daktari aliyefanya uchunguzi wa Al-Hudayri aligundua "majeraha mengi, hasa michubuko ambayo aliyahimili katika kipindi hicho hicho kutokana na kifaa kilichotobolewa (butu) au fimbo ya chuma".

Wizara ya Mambo ya Nje ya Libya, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, au mkurugenzi wa zamani wa Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano hakujibu maombi yetu ya mara kwa mara ya kutoa maoni yao.

Walid Elhouderi (kulia) anaonekana akiwa na kaka yake na binamu zake kufuatia kuachiliwa kwake

Chanzo cha picha, Walid Elhouderi

Maelezo ya picha, Walid Elhouderi (kulia) anaonekana akiwa na kaka yake na binamu zake kufuatia kuachiliwa kwake

Kilichotokea kwa wote Al-Hudayri na Mrabet ni zaidi ya simulizi ya ushindani kati ya wafanyikazi wa serikali.

Kwa maoni ya waangalizi, ni mfano wa utamaduni wa rushwa na kukosekana kwa umoja katika nchi ambapo dhuluma dhidi ya maslahi binafsi na ushawishi wa wanamgambo vimetawaliwa na nguvu.

Mwezi Agosti mwaka huu, Idara ya Ukaguzi ya Libya ilisema kuwa ilifuatilia "ukiukwaji" kuhusu uteuzi wa kidiplomasia ndani ya wizara hiyo, na kuonyesha uteuzi wa watu "nje ya sekta ya mambo ya nje".

Ofisi hiyo ilitoa mapendekezo kwamba ni pamoja na "kusitisha ongezeko la idadi ya wanachama wa misafara ya kidiplomasia" nje ya nchi.

Al-Hudayri alipohojiwa kwa mara ya kwanza yapata majuma mawili baada ya mkasa huo, mtu aliyekuwa akimhoji aliendelea kumwambia kuwa ana bahati.

Akaniambia: '’Unajua una bahati sana. Sufyan amekufa, tulimuua... Lakini wewe, una bahati. Kwanza, tulikusudia kukupeleka kwenye kikosi cha kuuwa watu."

"Ilikuwa wiki mbili baada ya kuteswa, wakati nilipokuwa nimefumbwa macho muda wote. Na hivyo ndivyo mahojiano yalianza. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa mtu kuzungumza nami katika kipindi cha wiki mbili ".

Mapema mwaka wa 2020, mwaka ambao aliwekwa kizuizini, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL) ulisema kwamba umepokea ‘’taarifa kadhaa za upotevu wa nguvu na mateso ya raia, ikiwa ni pamoja na, lakini sio tu, wanaharakati wa mashirika ya kiraia, waandishi wa habari, wahamiaji, na maafisa wa serikali’’ na wanamgambo katika mwaka uliopita.

UNSMIL, ambayo Bw Al-Hudayri alisema alifahamishwa kuhusu kesi yake, alikataa kutoa maoni yake, na kusema alitaka ‘’kuondoa madhara yoyote’’ kwa wafanyikazi wake na familia.

‘’Kilichonipata ni kisa cha kila raia wa Libya. Watu wengi hawasemi, Bw Al-Hudayri anasema.

Anasimulia kisa cha mtu aliyekutana naye kizuizini ambaye alikuwa akiendesha mkahawa huko Qasr bin Ghashir, yapata kilomita 20 kusini mwa Tripoli ya kati, ambaye inadaiwa alikamatwa na dinari iliyotolewa na benki kuu ya mashariki - ambapo utawala hasimu una makao yake.

‘’Alipofunga duka siku hiyo, alikuwa na takriban dinari 100 au 200 kutoka mashariki, kati ya dinari zipatazo 2,000. Ndiyo maana alishtakiwa.

Lakini hakuwahi kufikishwa mbele ya mwendesha mashtaka, na familia yake haikujua alikokuwa.’’

‘’Baadhi ya watu walifia huko... Wengine walikuwa huko kwa miezi mitano au sita. Hawakuwahi wamefikishwa mahakamani. Hakuna aliyejua waliko,’’ Bw Al-Hudayri anasema.

Na bado, hata kwa yote hayo, bado ilichukua zaidi ya mwaka mmoja kwake kuachiliwa.

Miezi kadhaa baada ya kuachiliwa kwao, si Bw Al-Hudayri wala Bw Mrabet waliorejeshwa katika wizara hiyo, wala hawajapokea aina yoyote ya fidia.