IMF: Dunia itarajie muendelezo wa athari kubwa zaidi za kiuchumi

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika tathmini yake ya hivi punde ya uchumi wa dunia, IMF ilisema kuwa "kwa watu wengi, mwaka 2023 itaonekana kama mdororo wa uchumi."
Shirika linalofanya kazi ya kuleta utulivu wa uchumi wa dunia limezidisha utabiri wake kuhusu ukuaji wa uchumi kutokana na matokeo ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Ukuaji nchini Uingereza unatarajiwa kukaribia kudorora mwaka ujao kwa asilimia 0.3.
Hii inawakilisha kushuka kwa 0.2% kutoka kwa makadirio ya Julai wa IMF na kushuka kwa kasi kwa kiwango cha ukuaji wa uchumi wa Uingereza cha 3.6% kinachotarajiwa mwaka 2022.
'Kuwa thabiti'
Baada ya Kansela wa Uingereza wa Hazina Kwasi Kwarteng kufichua mipango ya kupunguza ushuru mkubwa, IMF ilikosoa mapendekezo ya serikali, na kuonya kuwa hatua hizo huenda zikaongeza mzozo wa gharama ya maisha.
Katika taarifa ya wazi, IMF ilisema pendekezo hilo huenda likaongeza ukosefu wa usawa na shinikizo ambazo zitaongeza bei.
IMF inafanya kazi ili kuleta utulivu wa uchumi wa dunia, na moja ya majukumu yake muhimu ni kutenda kama mfumo wa tahadhari ya mapema ya kiuchumi.
Mfuko huo ulisema unaelewa mpango wa kichocheo wa serikali, lakini ulibainisha kuwa kupunguzwa kwa ushuru kunaweza kuongeza kasi ya ukuaji wa bei, ambayo benki kuu ya Uingereza inajaribu kupunguza.
Katika ripoti yake ya hivi punde Jumanne, mshauri wa kiuchumi wa IMF Pierre-Olivier Gurincha alisema: "Wakati mawingu ya dhoruba yanapokusanyika, watunga sera lazima wawe na mkono thabiti."

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Alikiri kwamba kifurushi kikubwa zaidi cha kodi katika miaka 50, kilichopendekezwa na waziri, "kitakuza ukuaji katika muda mfupi", licha ya kupeleka mshtuko katika masoko ya fedha. Ripoti hiyo pia iliongeza kuwa hatua hizo zitafanya kuwa vigumu kupambana na mfumuko wa bei, ambao unaonyesha jinsi gharama ya maisha inavyobadilika kadri muda unavyokwenda.
IMF pia ilionya kuwa serikali zinapaswa kulinda watu wenye kipato kidogo kutokana na athari za kupanda kwa bei ya bidhaa.
Kaya maskini mara nyingi hutumia kiasi kikubwa zaidi kuliko nyingine kununua chakula na mafuta, ripoti inabainisha - ambazo zote zimeshuhudia kuongezeka kwa bei kutokana na vikwazo vya mauzo ya nje ya nishati na nafaka tangu kuanza kwa vita vya Urusi nchini Ukraine.
Nchi ambazo zilitegemea gesi ya Urusi huko Ulaya ziliathiriwa vibaya sana. Kwa mfano, uchumi wa Ujerumani unatarajiwa kushuka mwaka ujao.
Wakati huo huo, uchumi wa Urusi unatarajiwa kushuka kwa 2.3% mwaka ujao.
Akizungumza siku ya Jumatatu, mkuu wa IMF Kristalina Georgieva alibainisha kuwa ukuaji pia unapungua nchini China kutokana na vikwazo vinavyoendelea vya virusi vya corona, na katika Marekani ongezeko la kiwango cha riba "linaanza kuuma."
Katika mikutano ya kwanza ya ana kwa ana kati ya IMF na Benki ya Dunia tangu janga hilo, alisema nchi zinaweza "kupunguza maumivu ambayo yanatungojea mnamo 2023" ikiwa zitafanya kazi pamoja.
Aliongeza kuwa IMF itasisitiza kuwa mataifa makubwa ya kiuchumi yaendelee na juhudi zao za kupunguza gharama ya maisha, hata kama yataathiri ukuaji wa uchumi.
Wasipofanya vya kutosha, alisema, "tuko kwenye matatizo. Hatuwezi kuruhusu mfumuko wa bei. Pia alibainisha kuwa hatua lazima "ziwe za usahihi na si la kuchochea zaidi ongezeko la bei.














