Odinga asema maandamano yataendelea huku mabalozi wakitaka utulivu Kenya

th

Chanzo cha picha, AFP

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amesema ataendelea kuongoza maandamano dhidi ya serikali kutaka gharama ya maisha kupunguzwa na kufunguliwa kwa seva za Tume ya Uchaguzi.

Muungano wa Azimio la Umoja ulitangaza kufanya maandamano ya kila wiki ,siku za Jumatatu na Alhamisi.

Msimamo wake huo unajiri huku balozi nane za kigeni nchini Kenya zikiwemo za Marekani na Uingereza kuelezea wasi wasi kuhusu ghasia zinazoanza kushuhudiwa nchini kutokana na maandamano hayo ya upinzani .

Takriban watu 3 wameuawa tangu Jumatatu iliyopita wakati upinzani ulipoitisha maandamano dhidi ya gharama ya maisha na serikali. Raia pia wameibiwa, magari kupigwa mawe na biashara kuporwa.

Wakati wa maandamano ya Jumatatu, takriban watu 2000 walivamia shamba la familia ya rais wa zamani Uhuru Kenyatta. Waliiba mamia ya mifugo, wakachoma sehemu za shamba na hata kujaribu kutwaa ardhi hiyo. Baadaye kampuni ya mitungi ya gesi inayomilikiwa na familia ya Raila Odinga pia ilishambuliwa.

Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki sasa amesema ghasia hizo sasa zinatishia uthabiti wa nchi na ametoa wito wa kukomeshwa kwa matukio hayo aliyoyataja kama ‘ya kichaa’

Maelezo ya video, Maandamano ya Azimio:Odinga alaani uvamizi wa shamba la rais mstaafu Uhuru Kenyatta

Odinga, ambaye alishindwa katika uchaguzi wa urais mwaka jana na William Ruto, amekataa kukubali matokeo na uamuzi wa mahakama ya juu ambao uliidhinisha ushindi wa Rais Ruto. Anataka serikali kufungua seva za uchaguzi wa urais ili kuthibitisha ni nani alishinda kama mojawapo ya masharti ya kumaliza maandamano ya kila wiki. Bw Odinga pia anasema anataka serikali kushughulikia gharama ya juu ya maisha na kukomesha mchakato wa kuteua tume mpya ya uchaguzi.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lakini katika taarifa ya pamoja, wajumbe hao wa kidiplomasia walikariri imani yao katika uchaguzi wa mwaka jana ambao waliutaja kama uliofanikiwa. Balozi hizo zilisema zinatambua haki ya maandamano ya amani lakini zikawakumbusha wahusika wote ‘wajibu wao kwa kanuni za demokrasia’. Siku ya Jumanne, mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahammat pia alitoa wito wa utulivu na mazungumzo huku akisisitiza kwamba uchaguzi wa Kenya ulikuwa wa mafanikio na matokeo yalithibitishwa katika Mahakama ya Juu.

Naibu Rais Rigathi Gachagua sasa anamshutumu kinara wa upinzani Raila Odinga kwa madai ya uzushi kuhusu maandamano ambayo yanapangwa kufanyika kila Jumatatu na Alhamisi. Bw Gachagua alisisitiza kuwa serikali haitashinikizwa katika mazungumzo na upinzani. Rais William Ruto, ambaye yuko Ujerumani, aliambia DW TV kwamba upinzani ulikuwa unatumia ‘suala la hisia’ la gharama ya maisha kufanya ghasia kuhusu uchaguzi ambao ulikuwa ‘suala lililosuluhishwa’.

Ujumbe wa Marekani ukiongozwa na Seneta Chris Coons umekutana na Naibu wa rais Gachagua na Raila Odinga jijini Nairobi kujadili hali ilivyo nchini Kenya