Je, G7 inaweza kuchukua hatua gani kuhusu Ukraine na Gaza?

Chanzo cha picha, Getty Images
Viongozi wa mataifa saba tajiri zaidi duniani wanakusanyika nchini Italia ili kuamua nini cha kufanya kuhusu vita vya Gaza na Ukraine.
Mkutano wa G7 pia utahusisha viongozi kutoka Afrika na eneo la Indo-Pacific, na utajadili ushirikiano wa kiuchumi na nchi zinazoendelea.
G7 ni nini ?
G7 (Kundi la nchi saba) ni shiŕika la mataifa saba makubwa zaidi duniani yanayoitwa yenye uchumi “wa hali ya juu,” ambayo yanatawala biashara ya kimataifa na mfumo wa fedha wa kimataifa. Nazo ni Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uingereza na Marekani.
Urusi ilijiunga mnamo 1998, na kuunda G8, lakini ilitengwa mnamo 2014 kwa sababu za kuichukua Crimea.
China haijawahi kuwa mwanachama, licha ya uchumi wake mkubwa na kuwa na idadi kubwa ya watu duniani.
Kiwango chake cha chini cha utajiri kwa kila mtu kinamaanisha kuwa hauonekani kama uchumi wa hali ya juu kama wanachama wa G7 walivyo.
Mataifa haya yote mawili yako katika kundi la G20 la mataifa yaliyoendelea na yanayoendelea.
EU sio mwanachama wa G7 lakini inahudhuria mkutano wa kilele wa kila mwaka.
Kwa mwaka mzima, mawaziri na maafisa wa G7 hufanya mikutano, kuunda makubaliano na kuchapisha taarifa za pamoja kuhusu matukio ya kimataifa.
Italia rais wa G7 mwaka 2024.

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, ni ajenda gani ya Italia inayotawala katika mkutano wa kilele wa 2024?
Mkutano wa kilele wa G7 wa 2024 utafanyika kutoka 13 - 15 Juni huko Apulia, nchini Italia.
Litakuwa kongamano la kwanza kuu la kimataifa ambalo waziri mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, amekuwa mwenyeji tangu aingie madarakani Oktoba 2022.
Serikali ya Italia inasema inataka mkutano huo uzingatie masuala kama vile vita vya Ukraine na Gaza, Afrika na uhamiaji, usalama wa kiuchumi, na ushirikiano wa kimataifa kuhusu Akili Mnemba (AI).
Je, viongozi wa G7 wanaweza kufanya nini kuhusu vita vya Ukraine na Gaza?
Kati yake, mataifa ya G7 tayari yameiwekea Urusi kifurushi kikubwa zaidi cha vikwazo kuwahi kuwekewa nchi yenye uchumi mkubwa.
Wamezuia nchi kufanya biashara ya kimataifa na mfumo wa kifedha wa kimataifa.
Pia wamezuia takribani $300bn mali za Urusi ambazo zilishikiliwa katika maeneo yao, kama vile akiba ya fedha za kigeni za benki kuu za Urusi.
Mataifa ya G7 sasa yanaripotiwa kufanya kazi katika mpango wa kupitisha riba iliyopatikana kutoka kwenye mali ya Urusi iliyohifadhiwa kuipeleka hadi Ukraine, kwa njia ya mkopo. Hii inaweza kufikia $50bn.
Mnamo tarehe 3 Juni, viongozi wa nchi za G7 waliunga mkono mpango uliowekwa na Rais wa Marekani Joe Biden wa kumaliza vita huko Gaza.
Amependekeza kusitishwa kwa mapigano mara moja na Israel na Hamas, kuachiliwa kwa mateka wote, ongezeko la misaada kwa Gaza na makubaliano ya amani ambayo yanahakikisha usalama wa Israel na usalama wa wakazi wa Gaza.
Je, G7 inawezaje kufanya kazi na mataifa yanayoendelea?
Serikali ya Italia inasema "mahusiano na mataifa yanayoendelea na mataifa yanayoinukia kiuchumi yatakuwa msingi" katika mkutano wa G7, na kwamba "itajitahidi kujenga mtindo wa ushirikiano unaozingatia ushirikiano wa kunufaishana".
Inawaalika viongozi kutoka nchi 12 zinazoendelea barani Afrika, Amerika Kusini na eneo la Indo-Pacific kuhudhuria mkutano huo.
Italia imeunda mpango unaoitwa, Mpango wa Mattei, ambapo itatoa euro 5.5bn ($5.9bn) ya misaada na mikopo kwa nchi kadhaa za Afrika, kuendeleza uchumi wao.
Mpango huo pia utaiweka Italia kuwa kitovu cha nishati, kujenga mabomba ya gesi na hidrojeni kati ya Afrika na Ulaya.
Hatahivyo, wachambuzi wengi wanashuku kuwa inaweza kuwa kinga kwa Italia kukabiliana na uhamiaji zaidi kutoka Afrika.
Italia imeyataka mataifa mengine kuchangia kifedha mpango huo.
Je, G7 inawezaje kukabiliana na usalama wa kiuchumi na hatari za akili mnemba (AI)?
Kama rais wa G7 mwaka 2023, Japan ililisukuma kundi hilo kuandaa mpango wa usalama wa kiuchumi wa kimataifa.
Kundi la G7 lilipitisha mkataba wa kusitisha nchi kama vile China na Urusi kutumia nguvu zao za kiuchumi kulazimisha matakwa yao kwa wengine.

Mnamo Desemba 2023, Italia ilijiondoa kwenye Mpango wa Ukanda na Barabara wa China, mpango wa kupanua bandari na njia za usafirishaji ulimwenguni kote ili kukuza biashara yake.
Bi Meloni alisema kuwa kujiunga kumekuwa "kosa kubwa". Marekani imeuita mpango huo "diplomasia ya mtego wa madeni" kwa upande wa China.
Inadhaniwa kuwa Marekani ina nia ya viongozi wa G7 kuchukua hatua zaidi kuhusu usalama wa kiuchumi katika mkutano wa kilele nchini Italia.
Usalama wa AI ulianza kuibuliwa katika mkutano wa kilele wa 2023 huko Japan na kusababisha Mchakato wa AI wa Hiroshima, uliokusudiwa kukuza "Akili mnemba salama, na ya kuaminika ulimwenguni kote".
Hata hivyo, huu ulikuwa tu mkusanyiko wa hatua za hiari. Mkutano wa kilele wa G7 unaweza kutayarisha kanuni zaidi za kimataifa za usalama wa akili mnemba, kwa kuzingatia Sheria yake iliyopitishwa na EU na agizo kuu la rais wa Marekani kuhusu akili mnemba.
Je, G7 ina nguvu?
G7 haiwezi kupitisha sheria. Hatahivyo, baadhi ya maamuzi yake ya zamani yamekuwa na athari kwa ulimwengu.
Kwa mfano, G7 ilichukua jukumu muhimu katika kuanzisha mfuko wa kimataifa wa kupambana na malaria na Ukimwi mwaka 2002.
Kabla ya mkutano wa kilele wa G7 wa 2021 nchini Uingereza, mawaziri wa fedha wa G7 walikubali kuyafanya makampuni ya kimataifa kulipa kodi zaidi.
Pia imetoa msaada wa kifedha kwa nchi zinazoendelea, na kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga












