Bondia aliyetoroka Iran kutafuta uhuru wa kupigana

Sadaf Khadem anafanya mazoezi katika klabu yake ya ndondi huko Royan pwani ya kusini-magharibi ya Ufaransa mara tatu kwa wiki. Bondia huyo mzaliwa wa Iran anatarajia siku moja kuwa mtaalamu.
Mabango kadhaa ya kijana huyo mwenye umri wa miaka 28 katika vazi lake la ndondi yamebandikwa kwenye kuta za klabu.
Lakini Sadaf amelilipia gharama kubwa ya kibinafsi ili kufikia ndoto yake - kuishi uhamishoni hapa Ufaransa kwa miaka mitatu iliyopita.
Alianza mchezo huo kisiri mjini Tehran, kwenye viwanja vya bustani kwani wanawake nchini Iran hawaruhusiwi kushiriki mchezo wa ndondi .
Kwa kuhofia huenda akakosa nafasi ya kujindeleza katika mchezo hua aliamua kuwasiliana na raia wa Iran wanaoishi Ufaransa, ambapo pambano lilianzishwa katika mji wa pwani wa Royan mnamo 2019.
Rais wa klabu ya ndondi ya eneo hilo Franck Weus, bondia wa zamani na kiongozi wa jamii, alichukua changamoto hiyo. Takriban asilimia 40 ya mabondia katika klabu yake ni wanawake na hata alichangisha pesa za kumsafirisha Sadaf kwa ajili ya pambano hilo lililovutia watazamaji 1,500.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
“Nilikubali kazi hiyo mara moja kwa sababu kuna ngumi na mchezo bila shaka, lakini pia mambo ya kibinadamu ya kuzingatia,” alimwambia mwandishi wa BBC. "Mwanamke wa Kiiran ambaye anataka kupiga ndondi lakini haruhusiwi nyumbani. Tunajua kuhusu vikwazo vyote wanavyokumbana navyo na hasa wakati huu ambapo mamia wamefariki kwa sababu tu wanataka kuvua hijab zao."
Anaashiria maandamano makubwa yaliyozuka nchini Iran tangu kifo cha mwanamke mwenye umri wa miaka 22, Mahsa Amini, Septemba iliyopita. Alifariki akiwa kizuizini baada ya kukamatwa na polisi wa maadili kwa madai ya kutovalia hijab yake ipasavyo.
Kifo chake kimesababisha maandamano kote nchini, ambayo yamesababisha mamia ya waandamanaji vijana na makumi ya wanachama wa huduma za usalama kuuawa, kulingana na mashirika ya kutetea haki za binadamu.
Maelfu ya waandamanaji wamekamatwa ingawa kiongozi mkuu wa Iran amedokeza kuwa wengi wanaweza kusamehewa. Wanaume wanne wanaoshutumiwa na mamlaka ya Iran kwa kushiriki katika uasi wa ghasia wamenyongwa.
Sadaf Khadem alishinda pambano lake na aliporejea uwanja wa ndege kurudi nyumbani alipata habari kwamba anaweza kukamatwa kwa kosa la kucheza ndondi na kufanya mazoezi ya michezo bila kuvaa hijab. Kwa hivyo hakuwa na budi kughairi safari yake - na amesalia Ufaransa tangu wakati huo.
"Najua hali ya Iran na kwa bahati mbaya siko pamoja na watu wa Iran, lakini maisha yangu na makazi yangu sasa ni Ufaransa," anasema.

Masaibu ya Sadaf yamezua gumzo katika kusini-magharibi mwa Ufaransa. Alialikwa kwenye tafrija na mbunge wa eneo lake, Christophe Plassard, ambaye anajaribu kumsaidia kupata pasipoti ya Ufaransa.
"Angependa kuwa na uraia wa Ufaransa lakini hajatimiza vigezo vyote yanavyohitajika kwa sababu hajakaa hapa kwa miaka mitano," alimwambia mwandishi wa BBC, na kuongeza: "Lakini ninajaribu kwa sababu amepata fursa ya kuja huku kupitia mchezo wa ndondi na pambano lake ni la kushangaza."
Katika mapokezi, Sadaf alivaa mavazi ambayo yangeweza kumweka katika matatizo huko Tehran. Kitu ambacho mara nyingi huangazia katika picha anazochapisha kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii kwa wafuasi wake huko Iran.
"Kila siku kwenye Instagram au barua pepe yangu napokea jumbe nyingi sana: 'Kwa Sadaf, tunapoona maisha yako tunapata motisha ya kuendelea na maisha yetu.' Kwangu mimi ni furaha, heshima kwangu. Nafarijika sana kwamba nawapa motisha watu wengi pia kuendelea kupigania haki yao."
Wakati hayupo ulingani kupiga ndondi, Sadaf anapata anasomea diploma ya Mauzo na kupata uzoefu wa kazi.














