Ni mpango gani ulikuwa nyuma ya mkakati wa kuondoa uongozi wa Iran?

    • Author, Gordon Corera
    • Nafasi, Mchambuzi wa masuala ya usalama BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Marekani na Israel waesema wana uwezo mkubwa wa zana za kivita za angani ambao unawawezesha kushambulia shabaha zao ndani Iran wapendavyo.

Pia wameonyesha uweledi wao wa kijasusi, ambao umewawezesha kuwaangamiza viongozi kwakuu wengi wa Iran.

Lakini kuna mkakati gani nyuma ya hili? Jibu moja ni kusababisha mkanganyiko.

Hatua ya kwanza katika kampeni hiyo haikuwa shambulio dhidi ya makaazi ya kiongozi mkuu, bali wadukuzi wa Kamandi ya anga ya juu ya Marekani na wenzao wa Israel.

Walivuruga uwezo wa Iran kubaini kilichokuwa kinafanyika, kudhidbiti mawasiliano na kujibu mashambulizi, kulingana na maafisa wa jeshi la Marekani.

Kwa kutumia mbinu hiyo viongozi wa gazi ya juu walishumbuliwa katika maeneo tofauti. Viongozi hao walikuwa wamefuatiliwa kwa miezi kadhaa na majasusi wa the CIA na Mossad, miongoni mwa wengine.

Hilo liliwezekana zaidi kupitia upenyaji wa kiufundi wa muda mrefu wa mifumo ya mawasiliano ya Iran na vile vile majasusi walioko ardhini, ambao mara nyingi huendeshwa na Mossad.

Israel inaaminika kuongoza mashambulizi hayo.

Marekani kwa upande wake inasema iliendelea kushambulia kamandi na udhibiti wa mawasiliano ya Iran, maeneo ya makombora ya balestiki na miundombinu ya kijasusi katika mshambulizi ya awali.

Lengo kuu lilikuwa "kuwashangaza na kuwachanganya" Wairan, alisema Dan Caine, mwenyekiti wa Wakuu wa Pamoja wa kijeshi katika mkutano wa Jumatatu.

Matarajio ya Marekani na Israel yalikuwa kulemaza Iran.

Hata hivyo,Tehran ilikuwa imejitayarisha katika suala lauongozi wake, na maafisa waliambiwa wawateue warithi wao endapo watakufa (na kuweka utambulisho wao kuwa siri).

Kwa kuzingatia hatari inayoambatana na hatua ni jambo la kustaajabisha kwamba baadhi ya viongo wa ngazi ya juu katika utawala wa Iran walikuwa wakikutana Jumamosi asubuhi - hali ambayo ilisababisha wengi wa kuuawa.

Je, mauaji hayo yanamaanisha kipindi hiki cha vita?

Kwa sasa huwenda ikawa vigumu kwa Iran kupata jibu. Mkanganyiko unaosababishwa na ulengaji una faida za kijeshi lakini pia unaweza kuwa na hatari.

Haijabainika iwapo misururu ya makombora na ndege zisizo na rubani zinazotumwa katika Mashariki ya Kati ni matokeo ya sera iliyotanguliwa ambayo sasa ni ya majaribio, ikiwa makamanda wa ndani wanafanya kwa hiari yao wenyewe, au kuna mtu wa serikali kuu anayetoa maagizo kupitia safu ya utendaji kazi.

Swali linalofuata ni ikiwa kuuawa kwa idadi kubwa ya viongozi kimsingi kutabadilisha mkakati wa Iran wa kuendelea kupigana au kutafuta njia kujiondoa.

Tathmini ya kijasusi ya CIA iliyokamilika kabla ya vita kuanza ilitabiri kuwa kuondolewa kwa kiongozi mkuu kunaweza kusababisha watu wenye msimamo mkali katika kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi kuchukua udhibiti zaidi.

Kiongozi yeyote mpya atalazimika kukokotoa kama uhai wa utawala utahakikishwa kwa kuendelea kupigana - au, kwa njia nyingine, kuzungumza na kukubali matakwa ya Marekani.

Lakini wakiendelea kuuawa, huenda ikawa vigumu kufikia uamuzi au mazungumzo yoyote.

Marekani huenda inatarajia mtu kama Delcy Rodríguez - ambaye alichukua nafasi ya Nicolas Maduro nchini Venezuela, inayesadikiwa kushirikiana na Marekani - lakini haijabainika kama mtu kama huyo yupo au anaweza kuongoza nchi hiyo.

Swali la mwisho - ambalo ni muhimu zaidi - ni ikiwa mauaji ya viongozi hao yatachangia mabadiliko ya serikali?

Historia inaonyesha kwamba mashambulizi ya anga pekee haitoshi, na Marekani haijaonyesha nia ya kujiingiza kwenye mapigano ya ardhini

Huenda kuna matumaini kuwa kuondoa vikosi vya usalama na kijasusi huenda kukasaidia uasi wa wananchi kufanikiwa wakati huu, baada ya waandamanaji kukandamizwa mwezi Januari.

Rais Trump alitoa wito kwa Wairani kuendelea kuandamana na hata kuahidi kinga kwa maafisa wa vikosi vya usalama ambao wataweka silaha zao chini. Lakini utawala huo umejikita sana na utafanya lolote liwezekanalo kusalia madaraka.

Ingawa mustakabali wa uongozi wa siku zijazo unayumba, kipaumbele cha Israel na Marekani inaonekana kusambaratisha utawala huo.

Ikiwa hiyo itasababisha mabadiliko, inaweza kukaribishwa na watu wa Iran - lakini hatari itawaangukia.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi