Mauaji ya Ayatollah Khamenei: Jinsi Afrika inavyojibu kwa tahadhari, ukosoaji na huzuni

Muda wa kusoma: Dakika 5

Mauaji ya kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, katika shambulio la pamoja kati ya Marekani na Israel, yamesababisha athari kubwa katika sehemu nyingi za Afrika.

Serikali, vikundi vya kidini, na viongozi wa kijamii wamejibu kwa njia tofauti, wakionyesha uhusiano wa kidini na kisiasa wa muda mrefu kati ya Afrika na Iran.

Kwa miongo kadhaa, Iran imewekeza katika vituo vya kidini, ufadhili wa masomo, na taasisi za kitamaduni katika nchi kama vile Nigeria, Niger, Ghana, na Gambia.

Kwa hivyo, matukio yanayotokea Tehran mara nyingi huwa na athari mbali zaidi ya Mashariki ya Kati.

Maandamano Nigeria na Niger

Nigeria, ambayo ina idadi kubwa zaidi ya Waislamu wa Kishia barani Afrika, ilishuhudia maandamano katika takribani majimbo 12 ya kaskazini ya kuomboleza kifo cha Khamenei.

Serikali imeongeza usalama, ikionya kwamba itachukua hatua dhidi ya yeyote anayejaribu kuchochea machafuko au mivutano ya kidini.

Ibrahim Musa, Shia mashuhuri na mhariri wa Almizan, gazeti la kidini la Nigeria, amesema waumini walimwona Khamenei kama chanzo cha "mwongozo wa kidini, kimaadili na kiroho," akiheshimiwa sana kwa taaluma wake.

Profesa Isah Mshelgaru, mwanaharakati wa Kishia wa Nigeria, amesema kifo chake "kinauma sana," akiongeza: "Atakumbukwa sana. Na kutokana na jinsi alivyofariki, tunajivunia sana. Ni heshima kubwa."

Ibrahim Zakzaky, aliyeanzisha Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) baada ya mapinduzi ya Iran ya 1979, ana uhusiano wa karibu na Iran na mchango mkubwa katika kuibuka kwa Uislamu wa Shia nchini Nigeria.

Harakati hiyo inakuza Uislamu wa Kishia na inadumisha uhusiano wa kidini na kiitikadi na Iran.

Omer Carmi, afisa wa zamani wa kijeshi katika Taasisi ya Washington na mwanafunzi wa udaktari katika Chuo Kikuu cha Tel Aviv, amesema katika makala kwamba kiongozi mkuu wa Iran alimtaja Zakzaky hadharani na IMN, akionyesha kwamba harakati hiyo ni sehemu ya mtandao mpana wa Iran na una jukumu muhimu Afrika Magharibi.

Katika nchi jirani ya Niger, maandamano ya usiku yalifanyika katika mji mkuu, Niamey. Waandamanaji walilaani mauaji ya Ayatollah Khamenei na wakaelezea mshikamano wao na Iran.

Nchini Gambia, ambako Uislamu wa Kishia pia unazidi kuimarika, profesa wa Kisufi Atif Amin Al Hussaini alimtaja Khamenei kama "kiongozi halali" wa jumuiya ya Kiislamu.

Aliita shambulio hilo "kushindwa kimaadili na kisheria" na amesema Marekani na Israel "zimepoteza vita vya kidiplomasia na kimaadili."

Kufungwa kwa ubalozi wa Marekani

Burkina Faso imepitisha moja ya uamuzi mkali zaidi katika eneo hilo. Serikali hiyo imelaani shambulio hilo na kutangaza kufungwa kwa ubalozi wa Marekani huko Ouagadougou. Pia imemrudisha balozi wake kutoka Washington.

Uamuzi huu unaonyesha mabadiliko makubwa katika sera ya kigeni ya nchi hiyo. Burkina Faso, kama Mali na Niger, imepunguza uhusiano wake na nchi za Magharibi katika miaka ya hivi karibuni huku ikitafuta washirika wengine.

Mauaji ya Khamenei yamezidisha matamshi makali kuhusu uhuru na upinzani dhidi ya uingiliaji kati wa kigeni.

Senegal yasikitika

Senegal ni moja ya nchi za kwanza za Kiafrika kutoa maoni hadharani. Waziri Mkuu Ousmane Sonko ameelezea mauaji hayo kama "makubwa sana" na "ya kusikitisha."

"Kwa siku mbili, vita vimezuka Mashariki ya Kati, vilivyochochewa na Marekani na mshirika wake Israel, ambao wamechagua kuishambulia Iran... Ni jambo la kusikitisha... kushambulia nchi zingine, kuzikandamiza nchi ili baadaye kuzimiliki; nchi isiyofuata azimio au agizo kutoka Umoja wa Mataifa inaweza kuamua kuishambulia nchi zingine..kuua, ni jambo zito sana."

Senegal kwa kawaida ina uhusiano wa karibu na nchi za Magharibi na ulimwengu wa Kiislamu.

Kauli hii inaonyesha msimamo mkali zaidi katika muktadha wa kuongezeka kwa mvutano wa kimataifa.

Afrika Kusini na Kenya

Mbali na Sahel, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amelaani mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, akisisitiza kwamba hayaendani na sheria za kimataifa.

"Kufanya shambulizi kwanza kwa kisingizio cha kujilinda hakuruhusiwi chini ya sheria ya kimataifa na kujilinda hakuwezi kutegemea mawazo au matarajio," amesema, akitaka "mashambulizi yasite."

Afrika Kusini ni mwanachama wa kundi la BRICS, ambalo linajumuisha Iran.

Kama Ramaphosa, William Ruto wa Kenya pia ameelezea msimamo wake kuhusu mashambulizi haya, akisema "Kenya inalaani vikali mashambulizi dhidi ya Falme za Kiarabu, Qatar, Saudi Arabia, Iraq, Oman, Kuwait, Jordan na Bahrain katika muktadha wa mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati."

Ameonya ikiwa mzozo huo utaenea hadi nchi zingine katika eneo hilo, unaweza kutishia amani na utulivu wa dunia.

Kote barani Afrika, kumezuka kauli za kulaani na wito wa kusitisha mapigano hadi maandamano ya mitaani.

Huku Iran ikifanya mashambulizi ya kulipiza kisasi na mataifa makubwa duniani yakionya kuhusu kuongezeka kwa mapigano, serikali za Afrika zinafuatilia kwa karibu hali hiyo.

Kwa wengi katika Sahel, mgogoro wa sasa si tu mgogoro wa mbali, bali unagusa upinzani na utambulisho wa kidini, maadili na maisha ya Ayatollah Ali Khamenei.