Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Bowen: Siku ya nne ya mashambulizi, haijabainika vita vinaelekea wapi
- Author, Jeremy Bowen
- Nafasi, International Editor
- Muda wa kusoma: Dakika 8
Leo ni siku ya nne tangu vita kuzika upya kati ya Marekani, Israel na Iran.
Tayari vimegeuka vita vya kikanda, baada ya Iran kuamua kushambulia nchi za kiarabu ambazo ni mshirika wa Marekani na majirani katika eneo la Ghuba.Uingereza imekubaliombi la Marekani kutumia vituo vyake vya kijeshi kuishambulia Iran licha ya kukataa hapo awali.
Vita vinaendelea kuongezeka, na taarifa zimiminika kwenye simu yangu. Nimesoma hivi punde taarifa kwa vyombo vya habari kutoka kwa Kamandi Kuu ya Marekani ikisema kwamba ndege tatu za kivita za Marekani aina ya F-15E Strike Eagles zimedunguliwa na walinzi wa anga wa Kuwait katika "tukio ambalo halikukusudiwa". Nikimaliza kuandika kipande hiki makombora zaidi yatakuwa yamerushwa na kuna uwezekano watu ambao wako hai sasa watakuwa wameuawa.
Ni mapema sana kuwa na wazo lolote la lini au jinsi vita vitaisha. Mara tu vita vinapoanza, ni vigumu kudhibiti. Lakini hizi ni baadhi ya njia ambazo wapiganaji wangelipenda iishe.
Tafsiri ya Trump ya ushindi
Rais Trump, kama ilivyo ada yake, amedhihirisha imani yake kwa mamlaka ya Marekani tangu alipotangaza vita vimeanza katika ujumbe wa video uliorekodiwa katika makazi yake ya Mar-a-Lago jijini Florida. Marais wengine wangechagua kutoa tangazo hilo katika Ikulu ya White House hususan Ofisi ya Oval.
Trump alivalia shati bila tai na kofia nyeupe iliyovutwa chini hadi juu ya macho yake. Alisoma taarifa ndefu, kuelezea jinsi Iran imekuwa tishio kwa Marekani tangu Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979.
Trump anajulikana kwa hulka yake ya kubadili msimamo hapa kwa hapa, lakini katika hotuba hiyo, anatoa ufafanuzi wa tathmini yake ya ushindi. Ni sawa na orodha ya ukaguzi:
"Tutaharibu makombora yao na kuteketeza viwanda vyao vya makombora na kuvitokomeza. Itafutiliwa mbali kabisa. Tutaangamiza jeshi lao la wanamaji. Tutahakikisha kwamba washirika wa kigaidi wa eneo hilo hawawezi tena kuyumbisha eneo au ulimwengu, na kushambulia vikosi vyetu, na kutotumia tena vilipuzi vyao au mabomu ya kutegwa kando ya barabara, ambayo wakati mwingine huwajeruhi maelfu ya watu. wakiwemo Wamarekani."
Trump alidai kuwa Iran inatengeneza makombora yakifyatuliwa yanaweza kufika Marekani, kauli ambayo haijthibitishwa na mamlaka za kijasusi za Marekani. Pia alidai kuwa ilikuwa karibu kutengeneza silaha ya nyuklia, kinyume na kauli yake mwenyewe msimu wa joto uliopita kwamba Marekani "imeharibu kabisa" maeneo ya nyuklia ya Iran.
Trump anaamini kuwa Marekani na Israel zinaweza kuangusha utawala wa Tehran. Wasipofanikiwa kufikia lengo hilo, anahisi utakuwa umelemazwa kiasi cha kuwawezesha watu wa Iran kuandamana hadi washinikize mabadiliko serikalini:
"Tutakapomaliza, chukueni serikali yenu. Hii bila shaka Itakuwa fursa yenu ya kuamua mustakabali wa taifa kwa vizazi vijavyo. Kwa miaka mingi mumumba msaada wa Marekani, lakini hamukuwahi kupata. Hakuna rais yuko tayari kufanya kile ninachofanya usiku huu. Sasa mna rais ambaye anawapatia kile mnachotaka. Sasa wacha tuone mtakavyojibu."
Kukabidhi jukumu la mabadiliko ya utawala kwa watu wa Iran, huku akiwahimiza moja kwa moja kuchukua hatua, kunampa uwezo wa baadaye kujiondoa ikiwa serikali itasalia. Lakini pia inaweza kutazamwa kama jukumu la kimaadili kwa Marekani kuliona hilo, ingawa ni swali la wazi ni kwa kiasi gani hilo linaweza kumshawishi rais ambaye anaamini kuwa kuna mpango wa kufanywa kila wakati.
Hakuna mfano wa kubadilisha utawala au kushinda vita dhidi ya adui mwenye silaha kwa kutumia nguvu ya anga. Mwaka 2003 Marekani na washirika wake ikiwemo Uingereza walituma vikosi vikubwa vya ardhini nchini Iraq kumuondoa Saddam Hussein. Mnamo 2011, Kanali Muammar Gaddafi wa Libya aliondolewa na vikosi vya waasi waliokuwa na silaha na Nato na nchi za Ghuba na kulindwa na vikosi vyao vya anga. Trump anatumai kuwa Wairan wanaweza kufanya kufanikisha hilo wenyewe.
Mpango wa Trump ni karata kubwa. Kadi mbaya zimepangwa dhidi ya ulipuaji wa mabomu pekee na kusababisha mabadiliko ya serikali.
Je, kuna uwezekano wa kufanyika kwa mapinduzi ya ndani yanayoungwa mkono na mataifa ya magharibi? Sio kwamba haiwezekani, lakini ni vigumu kubashiri hilo siku ya tatu ya vita.
Kuna uwezekano mkubwa kwamba viongozi wanaoendesha utawala huo watanyenyekea, watafyatua makombora zaidi, yanayochochewa na itikadi na imani kwamba wanaweza kupata maumivu zaidi kuliko Marekani, Israel au mataifa ya Ghuba ya Kiarabu. Maumivu mengi yatahisiwa na watu wa Iran wenye subira. Lakini hawana usemi katika jambo hilo.
Mahesabu ya Netanyahu
Saw ana Donald Trump, Benjamin Netanyahu pia ametoa wito wa kuwaasa Wairan kuchukua hatima yao mikononi mwao. Lakini wadhibitiwa na vikosi vya usalama vya utawala wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu, kipaumbele cha Netanyahu ni kuvunja uwezo wa kijeshi wa Iran na uwezo wake wa kuimarisha upya nguvu ya wanamgambo kuzunguka eneo ambalo linaweza kutishia Israel.
Kwa miongo kadhaa, Benjamin Netanyahu amechukulia Iran kama adui hatari zaidi wa Israeli. Anaamini kuwa watawala wa Jamhuri ya Kiislamu wanataka kuunda silaha ya nyuklia ili kuliangamiza taifa hilo la Kiyahudi.
Jumapili, sikuku ya pili ya vita, alisimama juu ya paa huko Tel Aviv, pengine jengo la wizara ya ulinzi katikati mwa jiji, na kusema jinsi alivyoona vita hivyo vikiisha.
Alisema kuwa Israel na Marekani kwa pamoja zitaweza "kufanya kile nilichotarajia kufikia kwa miaka 40 - kuuangamiza kabisa utawala wa kigaidi".
Alisema ni ahadi ambayo atahakikisha inatimia.
Vita daima vina mwelekeo wa kisiasa wa ndani. Kama Trump, Netanyahu anakabiliwa na uchaguzi baadaye mwaka huu. Tofauti na Trump, kazi yake mwenyewe iko kwenye mizani. Waisraeli wengi wanamlaumu Netanyahu kwa dosari za kiusalama zilizoipatia Hamas fursa ya kushambulia tarehe 7 Oktoba 2023. Atachukua hatua kubwa kuelekea msamaha wa uchaguzi ikiwa anaweza kusema ameiongoza Israel kupata ushindi mnono dhidi ya Iran. Anaweza hata kuwa asiyeweza kushindwa.
Ushindi kupitia ustahamilivu
Mauaji ya Kiongozi Mkuu na washauri wake wakuu wa kijeshi yalikuwa pigo kubwa kwa serikali. Lakini haimaanishi kwamba itaanguka.
Ayatollah Ruhollah Khomeini na waanzilishi wake wengine karibu miaka 50 iliyopita walibuni taasisi zake kunusurika vita na mauaji. Sio onyesho la mtu mmoja. Mataifa ya Syria na Libya chini ya Assad na Gaddafi yalijengwa karibu na familia zinazotawala. Wakati familia ziliondolewa - Gaddafi aliuawa na Bashar al-Assad alikimbia - tawala zilianguka.
Utawala wa Iran ni mfumo wa dola, unaoegemea kwenye mtandao tata na mnene wa taasisi za kisiasa na kidini zenye majukumu yanayoingiliana. Imeundwa kkustahamili vita na mauaji.
Hiyo haina maana haitatetereka. Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unakabiliwa na mtihani wake mkali zaidi. Lakini utawala umejipanga kwa wakati huu.
Tathmini ya ushindi kwa utawala wa Iran sio ustahalivu pekee bali pia ni kuishi. Ili kufikia hilo inajizingira na kiwango cha kutisha cha ulinzi.
Ina vifaa vya nguvu na vyombo vya kikatili vya usalama vinavyoendeleza ukandamizaji. Mnamo Januari watu walijitokeza barabarani, kupinga amri iliyotolewa ya kuwaua maelfu ya waandamanaji. Kufikia sasa - na kama nilivyosema mara kwa mara, ni siku ya nne ya vita ninapoandika haya - hakuna dalili kwamba vikosi vya jeshi vya serikali vinasalimu, kama alivyofanya Assad baada ya kukimbilia Moscow mnamo Desemba 2024.
Pamoja na vikosi vya kawaida vya jeshi na polisi walio na silaha za kutosha, kuna Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na mamlaka ya wazi ya kulinda utawala ndani na nje ya nchi. Ipo kama msingi uliyojengwa nyuma ya velayat-e faqihi, ulezi wa mwanasheria. Hayo ndiyo mafundisho muhimu ya mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, ambayo yanahalalisha utawala wa viongozi wa kidini wa Shia.
IRGC inaaminika kuwa na wanajeshi 190,000 na askari wa akiba 600,000. Mafundisho ya kidini, pia yanaendesha sehemu kubwa ya uchumi. Viongozi wake wana sababu za kifedha na kiitikadi za kuendelea kuwa waaminifu.
IRGC inaungwa mkono na Basij, kikosi cha wanamgambo wa kujitolea. Inakadiriwa kuwa wanachama wake 450,000 wana sifa ya uaminifu kwa serikali.
Niliwaona wakihudumu huko Tehran kama safu ya kwanza ya ulinzi wa serikali wakati wa maandamano yaliyofuatia uchaguzi wa 2009 uliokumbwa na utata, wakiwatishia na kuwapiga waandamanaji mitaani kwa marungu. Nyuma yao kulikuwa na polisi wenye silaha nzito na wanajeshi wa IRGC. Basij pia walikuwa na vikosi vya kuruka vya pikipiki ambavyo vilikimbia kuzunguka jiji vikikabiliana na milipuko maandamano ya upinzani.
Donald Trump ameitishia IRGC na Basij kwa kifo - alisema "haitakuwa kifo kizuri" - mpaka waweke silaha zao chini. Vitisho vyake huenda vikabadili mawazo mengi miongoni mwa watu wenye silaha wa utawala huo.
Iran ni nchi kubwa, karibu mara tatu ya ukubwa wa Iraq na idadi kubwa ya watu kutoka jamii mbalimbali zaidi ya milioni 90. Iwapo utawala wa Iran utaanguka, machafuko yanaweza kuzuka na kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe kama vile vilivyosababisha vifo vya maelfu ya watu nchini Syria na Iraq.
Hatua za kijeshi za Marekani na Israel zinaharibu uwezo wa kijeshi wa Iran. Hatua hiyo inabadilisha hali ya kiusalama Mashariki ya Kati, hata kama utawala utaendelea kuwepo.
Huenda baadhi ya Wairan, wangefurahia kuangushwa kwa utawala. Lakini itakuwa changamoto kubwa kuchukua nafasi ya utawala ulioondolewa kwa nguvu na kwa maslahi ya amani na uthabiti.
Trump anaamini itawezekana, vita hivi vitaifanya Mashariki ya Kati kuwa sehemu bora na salama.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi