Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini viongozi wa Ulaya wameshindwa kuzungumza kwa sauti moja kuhusu Iran?
Ulaya ilijua hali ya sasa ya vita huenda ikatokea. Kwa wiki kadhaa, viongozi na watunga sera walitazama jinsi jeshi la Marekani linavyoimarisha udhibiti wake Mashariki ya Kati. Walisikia vitisho vya utawala wa Trump kwa Tehran ya kutaka Tehran iachane na azmio lake la kuunda silaha za nyuklia.
Ila tangu mashambulizi ya Marekani na Israel yaanze dhidi ya Iran siku tatu zilizopita, bara Ulaya halijakuwa na sauti moja kuhusu msimamo wao.
Kila taifa la Ulaya linafikiria jinsi ya kuwalinda au kuwaondoa raia wake katika mataifa yanayoshuhudia vita.
Serikali za Ulaya pia zina wasiwasi kuhusu athari zinazoweza kutokea kutokana na vita hivyo na kuwaathiri moja kwa moja, haswa kupanda kwa bei ya chakula na nishati.
Tayari bei ya gesi barani Ulaya imepanda kwa kiwango kikubwa tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwaka wa 2022.
Kisiasa, Ulaya inajitahidi kuwa na sauti moja kuhusu yale yanayotokea mashariki ya kati.
Ufaransa, Ujerumani na Uingereza, zilifanikiwa kutoa tamko la pamoja mwishoni mwa juma lililopita, na kuionya Iran kuwa wako tayari kuchukua "hatua ya kujilinda" iwapo watashambuliwa.
Uingereza imekubali ombi la Marekani la kutaka kutumia vituo viwili vya kijeshi vya Uingereza kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Iran, ingawa Rais Trump amekuwa akilaumu Uingereza kwa kutowasaidia katika vita hivyo.
Ufaransa imeimarisha uwepo wake Mashariki ya Kati baada ya shambulio la Iran kugonga kambi ya kijeshi ya Ufaransa katika Falme za Kiarabu, huku Ujerumani ikisema wanajeshi wake wako tayari kuilinda taifa hilo iwapo watashambuliwa.
Nchi zote tatu ziliacha kuhoji uhalali wa hatua iliyochukulia na Marekani na Israel dhidi ya Iran chini ya sheria za kimataifa.
Viongozi hawa wote wa Ulaya hawataki kumtenga Donald Trump. Wanatumai matukio ya Mashariki ya Kati hayatakuwa kisingizio la kutoendelea kutafuta suluhu ya vita vinavyoendelea kati ya Ukraine na Urusi.
Lakini je,kunyamaza kwa mataifa ya Ulaya kuhusu uhalali wa hatua ambazo Marekani imechukua dhidi ya Iran na Venezuela kunaashiria nini? Na sheria ya kimataifa inasemaje?
Waziri mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez kupitia mtandao wa kijamii, alisema kuwa "mtu anaweza kuwa anapinga utawala wa chuki, kama ilivyo kwa utawala wa Iran na wakati huo huo pia anapinga uingiliaji wa kijeshi usio wa haki unaokiuka sheria za kimataifa."
Ndege kadhaa za Marekani ziliondoka Uhispania siku ya Jumatatu baada ya Madrid kusema kuwa kambi hizo haziwezi kutumika kwa mashambulizi dhidi ya Iran.
Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya umeonekana kutokuwa na umoja.
Kauli ya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama yanataka mabadiliko kufanyika katika serikali ya Iran. Hii ni baada ya rais wa tume ya Ulaya siku ya Jumapili kusema kuwa "mageuzi ya utawala nchini Iran yanahitajika haraka sana," Ursula von der Leyen rais wa EU alisema kupitia mtandao wa kijamii.
Mabadiliko ya nyuklia
Mwaka wa 2026 umegubikwa na vita;Venezuela, Greenland na Iran. Ulaya inakabiliwa na Urusi inayotaka kupanua mipaka yake, ukuaji wa nguvu ya kiuchumi ya China na Marekani ambaye ni mshirika wake wa karibu ambaye hatabiriki.
Siku ya Jumatatu, Rais Emmanuel Macron alitangaza kwamba Ufaransa itabadilisha sera yake ya nyuklia na kuongeza idadi ya silaha zake za nyuklia, kwa kusema kuwa, "washindani wetu wamejiboresha, pamoja na washirika wetu."
Urusi ina silaha nyingi zaidi za nyuklia duniani, China inaongeza kwa kasi uwezo wake wa kivita, huku Marekani ikiwa ya pili katika kumiliki silaha za nyuklia na kwa miongo kadhaa imekuwa ikihifadhi nyuklia ya Ulaya. Hatua ya hivi karibuni ya Marekani imewatia wasiwasi Ulaya.
Uswidi, Ujerumani na Poland wameiomba Ufaransa ulinzi zaidi kando na ule wanaoweza kuupata kutoka jumuiya ya kujihami ya Nato.
Rais Macron amejikuta katika nafasi ya "si ni niliwaambia" baada ya kuwataka Ulaya kwa miaka mingi kuwa na uhuru zaidi wa kimkakati katika masuala ya ulinzi.
Lakini suala la uratibu bado ni changamoto kubwa kwa Ulaya. Ununuzi wa silaha ni mfano dhahiri.
Wanachama wote wa NATO isipokuwa Uhispania walikubali shinikizo kutoka kwa Donald Trump mwaka jana wa kutenga fedha zaidi za ulinzi.
Vipaumbele vinavyotokana na historia
Kufuatia matukio yanayoendelea Mashariki ya Kati kila nchi bara Ulaya ina vipaumbele vyake, nguvu na udhaifu wake, vilivyotengenezwa na historia ya taifa hilo na raia wake.
Ujerumani ilifafanua wiki hii kwamba haipangi kuongeza uwepo wake wa kijeshi Mashariki ya Kati, wala kushiriki katika mashambulizi yoyote, na kutokana na historia yao, wajerumani hawapendi kujihusisha na vita.
Ujerumani imekuwa ikitegemea Marekani kwa usalama wake kwa miongo mingi.
Lakini baada ya utawala wa Trump kusisitiza kwamba Ulaya sasa ichukue jukumu kubwa zaidi la ulinzi wake, Ujerumani inapanga kutumia kiwango kikubwa cha bajeti yake kwa ulinzi ifikapo 2029, kuliko Ufaransa na Uingereza kwa pamoja, kwa mujibu wa NATO.
Waziri mkuu wa Italia, kwa upande wake, hajajihusisha na mashambulizi yanayoendelea Iran. Giorgia Meloni ni mmoja wa viongozi wachache barani Ulaya ambao wana uhusiano mzuri na Donald Trump.
Miungano ya muda mfupi
kufahamu zaidi kuhusu mizozo ya kimataifa na washirika wake, na ni nani anaweza kutegemewa wakati wa vita, ni kuangazia makubaliano ya ushirikiano kati ya mataifa haya.
Vikwazo vya kuchukua hatua "kwa umoja," kama tunavyoona tena sasa Mashariki ya Kati, vinaibua miungano midogo ya muda, zinazoundwa kwa ajili ya maslahi ya mataifa husika kuhusu masuala tofauti.
Miradi ya pamoja ya ununuzi wa silaha za ulinzi kama vile Mkataba wa Ulinzi wa Uingereza na Norway ya hivi karibuni kufuatilia uwepo wa manowari za Urusi katika maji ya bahari Kaskazini ya Atlantiki, au Muungano wa wanaoiunga Ukraine, unaoongozwa na Uingereza na Ufaransa.