Marekani dhidi ya Iran: Viongozi wa dunia wachukua misimamo tofauti

Muda wa kusoma: Dakika 4

Dunia inaonekana kugawanyika mara mbili, baada ya mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Ingawa mataifa mengi yameiunga mkono Israel na Marekani, kuna yale ambayo yanaiunga mkono Iran.

Aidha kuna mataifa mengi ambayo hayajaegemea upande wowote, na wametoa taarifa zao kuhusu vita hivyo kwa umakini sana. Wanazungumzia amani ila hawataji kuunga mkono upande wowote.

Viongozi wengi wa Iran wameuawa ikiwemo Ayatollah Ali Khamenei. Kulipiza kisasi, Iran ililenga kambi za kijeshi za Marekani zilizoko katika mataifa ya Ghuba.

Mataifa mengi duniani yametoa hisia zao

India inasema nini?

Waziri mkuu wa India, Naredra Modi, alizungumza na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kwa njia ya simu siku ya jumapili kuhusu hali ya sasa.

Modi aliandika kwenye mtandao wa X kuwa ' India ina wasiwasi kuhusu matukio ya hivi karibuni, na usalama wa raia wake unafaa kupewa kipaumbele."

Waziri huyo mkuu aidha alitoa wito wa vita hivyo kusitishwa.

Mapema siku hiyo, Modi alizungumza na rai swa falme za kiarabu Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan.

Modi alishtumu shambulio dhidi ya falme za kiarabu, na kumshukuru Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan kwa kuwalinda rai awa India wanaoishi nchini humo,

Wizara ya Mambo ya Nje ya India ilitoa taarifa Jumamosi ikieleza wasiwasi juu ya hali katika eneo la Ghuba.

"India ina wasiwasi mkubwa kuhusu matukio ya hivi karibuni nchini Iran na eneo la Ghuba. Tunaomba pande zote zichukue tahadhari na kuweka usalama wa raia wao mbele, na kuepuka kutanua vita," ilisema Wizara ya Mambo ya Nje.

Uingereza imesema haitashiriki katika kuishambulia Iran

Uingereza ilikubali ombi la Marekani la kutaka kutumia kambi ya kijeshi ya Uingereza kujilinda dhidi ya mashambulizi ya makombora ya Iran.

Waziri mkuu wa Uingereza, Keir Starmer alitoa taarifa hiyo na kusema ni kutokana na mafunzo waliyoyapata baada ya vita vya Iraq.

Waziri huyo alisema taifa lake halitahusika kuishambulia Iran.

Starmer alisema alikubali ombi la Marekani kutokana na ushirikiano wa kijeshi walionao.

Aidha, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, walitoa taarifa ya pamoja kushtumu hatua ya Iran kutekeleza mashambulizi magharibi mwa bara Asia.

Mataifa ya Ulaya yanaunga nani mkono?

Rais wa Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, alisema Umoja wa Ulaya tayari ilikuwa imeiwekea vikwazo utawala wa Iran.

"Pande zote zinapaswa kuwa na subira ili kulinda maisha ya watu. Sheria za kimataifa zinapaswa kuheshimiwa," alihoji.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, ilisema inawaunga mkono raia wa Iran.

"Tunasimama pamoja na raia wa Iran, wanaopigana dhidi ya ukandamizaji," alisema Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese. Aliongeza kwamba anaunga mkono juhudi za Marekani za kuzuia Iran kupata silaha za nyuklia.

Mataifa ya Ghuba yatoa onyo kwa Iran

Nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba (GCC) walikutana Jumapili kujadili uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya Iran. Baraza hilo lilisema kwamba Iran ililenga maeneo ya makazi na miundombinu ya kiraia.

Mataifa hayo yalisema Iran inakiuka sheria za kimataifa.

GCC inajumuisha Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain, Saudi Arabia, Oman, Qatar, na Kuwait

Katika taarifa kwa vyombo vya habari GCC, imeitaka Iran kusitisha mashambulizi yake, nakuonya kuwa watatumia nguvu zote walizonazo kulinda usalama wao.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi, amepinga shtuma kuwa wanawalenga mataifa jirani.

"Sisi hatuwashambulii majirani zetu eneo la Ghuba. Tunalenga vituo vya Marekani katika nchi hizi. Majirani wanapaswa kupeleka malalamiko yao kwa wale waliyoanzisha vita hivi," aliambia shirika la habari la Al Jazeera.

Pakistan yamuomboleza Khamenei

Waziri mkuu wa Pakistan Shahbaz Sharif, ameelezea kusikitisjwa na kifo cha kiongozi mkuu wa kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei.

"Serikali ya Pakistan inasimama pamoja na raia wa Iran katika wakati huu wa huzuni. Ninatoa rambirambi zangu kwa mfia dini Ayatollah Sayyed Ali Khamenei," Waziri Mkuu Shahbaz Sharif aliandika kwenye mtandao wa X.

China inaiunga mkono Iran

China imetoa taarifa ikikashifu mashambulio ya Israel na Marekani dhidi ya Iran na kwa mauaji ya Ayatollah Khamenei.

China ilisema mashambulio ni "kinyume na madhumuni na sheria ya mkataba wa Umoja wa Mataifa."

"Shambulio dhidi ya Iran, na kumuua Kiongozi Mkuu ni ukiukaji mkubwa wa utawala uhuru wa Iran, uhuru na usalama wake. China inaishtumu vikali mashambulizi hayo" Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo ilisema

China pia ilitoa wito wa amani kudumishwa.

Urusi yakosoa mashambulizi ya Marekani

Rais wa Urusi Vladimir Putin, alituma rambirambi zake baada ya kifo cha kiongozi wa kidini wa Iran Ali Khamenei kutangazwa.

"Kifo cha Ali Khamenei na familia yake ni mauaji ambayo yanakiuka maadili ya binadamu na sheria za kimataifa," BBC Persian iliripoti .