Kwa nini Iran inashambulia majirani zake?

    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, Dar es Salaam
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Kuna waliotegemea vita kati ya Israel na Marekani kwa upande mmoja dhidi ya Iran, vingebaki katika mipaka ya Iran na Israel. Hali halisi ni kwamba mashambulizi yameenea katika mataifa mengine ya Mashariki ya Kati.

Mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran yameshuhudia mataifa kadhaa, ikiwa ni pamoja na Bahrain, Qatar, Falme za Kiarabu, Kuwait, Jordan, na Oman, yakipigwa na makombora na ndege zisizo na rubani kutoka Iran.

Idadi ya nchi zinazokumbwa na mashambulizi zinazidi kuongezeka, kuna ripoti pia za kutokea kwa mashambulizi nchini Jordan, Iraq, na Saudi Arabia.

Mashambulizi haya yamesababisha kufungwa kwa anga za anga ndani ya eneo hilo, huku mashirika ya ndege ya kimataifa yakifuta safari za ndege kuingia na kutoka Mashariki ya Kati na viwanja kadhaa vya ndege vimefungwa katika eneo hilo.

Kuna athari za kiuchumi kutokana na kukwama kwa safari za ndege, pia safari za baharini hasa katika mlango wa bahari wa Hormuz. Vilevile, kuna athari katika maisha ya watu, tayari kuna ripoti za majeruhi na vifo katika mataifa ya Kiarabu.

Nchi za Kiarabu zinajiona kuwa zinashambuliwa na Iran, ingawa Iran inajiona kuwa inashambulia kitu kingine tofauti. Ndipo lile la swali la kwa nini vita hivi vimevuka mipaka na kuingia katika mataifa mengine linaibuka.

Kwa nini Iran inashambulia majirani?

Jawabu ya swali hili ni rahisi: Ni kutokana na uwepo wa kambi za kijeshi za Marekani katika mataifa ya Mashariki ya Kati. Kwa ujumla, Marekani ina vituo vya kijeshi katika maeneo yasiyopungua kumi na tisa, nane kati yao yakizingatiwa kuwa kambi za kudumu.

Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amesema Tehran inaona kulipiza kisasi kwa mashambulizi ya Israeli na Marekani kama "haki na wajibu wake halali."

Lakini mashambulizi ya Iran hayajapiga kambi za jeshi la Marekani pekee, kuna ripoti kwamba hoteli na viwanja vya ndege vimeshambuliwa. UAE inasema mtu mmoja amefariki na wengine wakijeruhiwa baada ya shambulio kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zayed.

Iran inafanya hivi kutokana na ukweli kwamba haina uwezo wa kushambulia Marekani moja kwa moja. Kwa lugha nyingine ni kwamba, Iran haina makombora yenye uwezo wa kufika Texas na Florida.

Umbali wa kutoka mji mkuu wa Iran, Tehran hadi kufika New York, Marekani ni kilomita 9,881. Kombora lenye uwezo mkubwa la Iran lina uwezo wa kufika kilomita 3,000 tu.

Licha ya Iran kuwa na ndege nyingi zisizo na rubani na ndege za kivita, lakini haziwezi kufua dafu katika safari hii ndefu ambapo pia kuna mifumo imara ya ulinzi wa anga ya Marekani.

Fauka ya hayo, kwa Iran kuna jambo jingine la ziada inalitafuta katika mashambulizi dhidi ya nchi za Kiarabu. Mashambulizi hayafanyiki ili kulipiza kisasi tu, pia yanafanyika kama njia ya kuzishinikiza nchi hizi zimtulize rafiki yao Marekani.

Mahesabu ya Iran ni kwamba kadiri mashambulizi yao yanavyokuwa makali na mengi dhidi ya washirika wa Marekani katika eneo hilo, yanaweza kuzisukuma nchi hizi kutoa shinikizo kwa Marekani ili vita vifikie mwisho.

Igawa kuna hatari nyingine inaweza kutokea. Baadhi ya nchi za kiarabu zimeeleza kuwa zina haki ya kujibu mashambulizi ya Iran. Lakini hadi sasa hakuna nchi ambayo imeshambulia Iran. Kwa kuzingatia hayo yote, washirika wa Marekani katika eneo hilo wana jambo moja la kuchagua kati ya matatu. Tuendelee..

Nchi za Kiarabu zitafanya nini?

Moja: Kujibu mashambulizi ya Iran kwa kufanya mashambulizi dhidi ya Tehran na kuufanya mgogoro huu uzidi kutanuka na kuwa mbaya. Ikiwa watachukua hatua hii, itapendwa na Marekani na Israel lakini itazidi kuliingiza eneo hilo katika vita na machafuko mabaya.

Kuna hatari pia makundi mengine yanayoiunga mkono Iran katika nchi kama Yemen, Iraq na Lebanon nayo kuingia katika kuzishambulia nchi za Kiarabu.

Pili: Chaguo jingine la washirika wa Marekani ni kuendelea kuvumilia mashambulizi ya Iran hadi pale vita vitakapo malizika. Bahati mbaya, hatujui vita vitamalizaka lini.

Kwa mujibu wa kauli za Rais wa Marekani, Donald Trump na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, wamedhamiria vita viendelee kwa wiki kadhaa hadi watakapo fanikisha malengo yao.

Tatu: Jambo la tatu ambalo nchi za Kiarabu wanaweza kuchagua kufanya, ni kutoa shinikizo kwa Marekani na Israel kusitisha

mashambulizi yao dhidi ya Iran, ili Iran nayo iache kuzishambulia nchi hizi. Iran pia inatamani kuona jambo hili likitokea.

Bila shaka ni tabua kusema ikiwa nchi hizi kwa hakika zina ushawishi na nguvu ya kutoa shinikizo kwa Marekani kuacha vita, seuze kwa Israel ambaye uhusiano wao ni wa uadui na urafiki kwa wakati mmoja.

Wakati bei ya mafuta ikizidi kupanda, nchi za Kiarabu zikishindwa kuuza mafuta, utalii ukiporomoka, miji ikizidi kushambuliwa, majeruhi na vifo vikizidi kuongezeka; hawawezi kukaa kimya bila kufanya lolote, kuna chaguzi za kufanya, moja, mbili, tatu au zote kwa pamoja.