Vita vya Tigray: Mapigano mapya yasambaratisha makubaliano ya kibinadamu

Mapigano makali yamezuka kaskazini mwa Ethiopia kati ya vikosi vya serikali na eneo la Tigrayan, na kuvunja makubaliano ya miezi mitano ya kibinadamu.

Usuluhishi huo ulikubaliwa kuruhusu msaada kuingia katika eneo la Tigray - ambapo maelfu wamekufa katika vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe na mamilioni wanahitaji vifaa vya kimsingi.

Watu katika mji wa karibu waliiambia BBC kuwa wamesikia silaha nzito na kuona vitengo vya jeshi la serikali vikiwasili. Pande zote mbili zimelaumiana kwa kuzuka upya kwa mapigano.

Siku ya Jumatano asubuhi, Getachew Reda, mshauri wa kiongozi wa Tigrayan, alisema vikosi vya Ethiopia vilihusika na kuanzisha mashambulizi dhidi ya Tigray baada ya "chokozi ya wiki nzima" katika eneo jirani la Amhara.

Serikali baadaye ilishutumu vikosi vya Tigrayan kwa kuvunja makubaliano - na kusema jeshi la shirikisho na vikosi vya usalama vilikuwa vikijibu mashambulizi yao "kwa mafanikio".

Maafisa wa Ethiopia pia walisema kuwa vikosi vyao viliidungua ndege iliyokuwa imebeba silaha za wanajeshi wa Tigray, jambo ambalo Bw Getachew alikanusha.

Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema ameshangazwa sana na mapigano hayo na kutoa wito wa "kukomeshwa mara moja kwa uhasama".

Mwanaume mmoja huko Kobo, takriban kilomita 25 kutoka maeneo ambayo mapigano yameripotiwa, aliiambia BBC kwamba alisikia milio ya risasi kwa mara ya kwanza Jumanne usiku.

"Mnamo saa tano asubuhi, milio ya risasi iliongezeka kutoka pande zote mbili na tulikuwa tunasikia silaha nzito zikifyatuliwa," alisema.

Vita vya Tigray vilizuka katika eneo la kaskazini mwa Ethiopia mnamo Novemba 2020 - baadaye kuenea kusini hadi mikoa ya Amhara na Afar.

Maelfu waliuawa, zaidi ya watu milioni mbili walikimbia makazi yao na takribani watu 700,000 waliachwa wakiishi katika "mazingira ya njaa", maafisa wa Marekani walisema.

Mkoa huo umekatiwa huduma ya mtandao na simu tangu mzozo huo uanze na hivyo kusababisha ugumu wa kujua nini hasa kinaendelea, na kuwawia vigumu watu kuendelea na shughuli zao za kimsingi zikiwemo za benki.

Serikali ya Ethiopia ililaumiwa kwa kuweka kizuizi katika eneo hilo ambalo lilizuia utoaji wa misaada muhimu.

Usitishaji mapigano wa kibinadamu uliofikiwa Machi 2022 ulienda kwa njia fulani katika kuongeza kiwango cha misaada kufikia kanda - lakini haikutosha.

Wiki iliyopita, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani lilisema kuwa karibu nusu ya wakazi wa Tigray 5.5m walikuwa na uhitaji "mkubwa" wa chakula.

"Njaa imeongezeka, viwango vya utapiamlo vimeongezeka, na hali inakaribia kuwa mbaya zaidi wakati watu wanaingia msimu wa njaa hadi mavuno ya mwaka huu mnamo Oktoba," ripoti hiyo ilisema.

Makubaliano hayo yaliibua matumaini ya mazungumzo ya amani kati ya pande hizo mbili.

Kwa kuwa sasa mapigano yameanza tena, mashirika ya kutoa misaada yanaweza kupata ugumu tena kuwafikia mamilioni ya watu wanaohitaji, na mazungumzo yoyote ya kisiasa yatacheleweshwa zaidi.