Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Mistari yote mekundu imevukwa': Mataifa ya Kiarabu yatajibu mashambulizi ya Iran?
Mataifa ya Kiarabu ya Ghuba yamejikuta katika mstari wa mbele wa vita vipya vya Mashariki ya Kati, na yamekasirika.
Iran imejibu mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel kwa kurusha mamia ya makombora na ndege zisizo na rubani kwa majirani zake wa Kiarabu - ikilenga kambi za kijeshi za Marekani katika ardhi yao, lakini pia miundombinu ya kiraia na nishati.
Kwa kufanya hivyo inaharibu taswira ya Ghuba kama eneo salama na ustawi katika usafiri, utalii na fedha, na kuvuruga sekta ya mafuta na gesi katika nchi hizo.
Hivi ni vita ambavyo serikali za Kiarabu hazikutaka vitokee na zilijaribu kuvizuia. Swali ni ikiwa nao wataingia katika vita baada ya mashambulizi waliyoyaitaya ya "usaliti" ya Iran.
"Mistari yote mekundu tayari imevukwa," amesema msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Qatar, Majed al Ansari, katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumanne.
"Mashambulizi dhidi ya ardhi yetu ni ya mara kwa mara," aliwaambia waandishi wa habari.
"Kuna mashambulizi dhidi ya miundombinu. Kuna mashambulizi katika maeneo yetu ya makazi. Na athari za mashambulizi haya ziko wazi. Linapokuja suala la kulipiza kisasi, chaguzi zote ziko mikononi mwa uongozi wetu. Lakini tunapaswa kuweka wazi kwamba mashambulizi kama haya hayatakosa majibu na hayawezi kukosa majibu."
Iran na Mataifa ya Ghuba
Makombora mengi ya Iran yanazuiliwa katika eneo hilo, lakini mabaki yanapoanguka huwasha moto na kuua watu. Ndege zisizo na rubani ambazo zinaweza kupita kwa urahisi kwenye ulinzi wa anga mara nyingi husababisha uharibifu mdogo lakini bado husababisha taharuki ambayo huvuruga biashara na usafiri.
Huo ndio mkakati wa Iran - kuongeza hatari kwa majirani zake wa Kiarabu kwa matumaini kwamba wataongeza shinikizo kwa Marekani ili kukomesha vita.
Inaaminika Iran ilirusha karibu ndege zisizo na rubani na makombora kwa United Arab Emirates sawa na idadi iliyorusha kwenda Israel, UAE ni kitovu kikuu cha biashara na utalii katika ghuba hiyo.
Iran inaweza kuleta vurugu katika sekta muhimu ya mafuta na gesi katika eneo hilo - jambo ambalo linaweza kusababisha misukosuko katika uchumi wa dunia.
Hilo pia lina maana kwamba mkakati wa Tehran unaweza kuwageukia. Kwani kuna hatari ya kuyasukuma mataifa ya Ghuba kuwa karibu zaidi na Washington, hata kuyafanya yajiunge na vita hivyo kwa namna fulani.
Hadi sasa, wamekataa kuruhusu Marekani kutumia anga na eneo lao kuanzisha mashambulizi dhidi ya Iran. Hilo linaweza kubadilika. Wanaweza kuamua kushiriki katika shughuli za kijeshi.
Hawajaamua hilo bado - kwa sasa Waarabu wamejikita katika ulinzi. Lakini maamuzi mengi yatategemea muda ambao vita vitaendelea.
Baadhi wanasita kuonekana kuwa wanaunga mkono upande wa Israel katika mzozo huo.
Mashambulizi mabaya na ya uharibifu ya Israel huko Gaza kujibu mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 2023, pamoja na uingiliaji wake wa kijeshi katika nchi kama vile Lebanon na Syria, yamezidi kuathiri uhusiano wa Israel na Waarabu.
Walikasirika sana Israel ilipoishambulia Qatar mwaka jana katika jaribio la kuua viongozi wa Hamas.
Kilicho wazi ni kwamba mashambulizi ya Iran yameimarisha umoja miongoni mwa mataifa ya Ghuba
Wajumbe sita wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba - Saudi Arabia, Kuwait, Qatar, Bahrain, Falme za Kiarabu na Oman - walikutana katika kikao cha dharura siku ya Jumapili kuelezea mshikamano.
Pia wameahidi "kuchukua hatua zote muhimu kulinda usalama na utulivu na kulinda maeneo yao, raia, na wakazi wao, ikiwa ni pamoja na chaguo la kujibu mashambulizi."
Mshauri mkuu wa kidiplomasia wa rais wa Imarati, Anwar Gargash, ameitaka Iran ifanye maamuzi sahihi.
"Vita vyako si dhidi ya majirani zako," aliandika katika chapisho X. "Fanya maamuzi sahihi, na ushughulike na majirani zako kwa busara, kabla ya kutengwa na hali kuzidi kuchafuka."