Jinsi Trump anavyotaka Marekani kunufaika kutokana na mkataba wa amani wa Congo

    • Author, Farouk Chothia
    • Nafasi, BBC News
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Utawala wa Trump unaongoza mpango kabambe, lakini wenye utata, wa amani unaolenga kumaliza mzozo wa muda mrefu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ambao pia unajumuisha nchi jirani ya Rwanda.

Juhudi zake za upatanishi hazishangazi, kwani DR Congo - taifa lililo katikati mwa Afrika - limejaliwa kuwa na utajiri wa madini ambao Marekani inahitaji kuendesha Teknlojia ya mawasilaino (IT), na sasa Akili Mnemba (AI),ambayo kwa kiwango kikubwa kwa sasa yanakwenda China.

Rais wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kuwa mwenyeji wa viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda - Félix Tshisekedi na Paul Kagame - katika wiki zijazo ili kutia saini makubaliano ya amani ambayo ameyataja kama "ushindi mtukufu", akitumai kuunga mkono na mikataba ambayo itaongeza uwekezaji wa Marekani katika eneo hilo.

Mkurugenzi mtendaji wa wakfu wa World Peace yenye makao yake nchini Marekani Prof Alex de Waal aliiambia BBC kwamba utawala wa Trump unakuza "mtindo mpya wa kuleta amani, unachanganya utendaji na makubaliano ya kibiashara".

"Trump amefanya hivyo nchini Ukraine pia. Anataka kutumia mpango huo kukuza hadhi yake ya kisiasa, na kupata madini kwa maslahi ya Marekani," Prof De Waal alisema.

Hata hivyo, alibainisha kuwa "China tayari imeshanyakua madini mengi nchini DR Congo, hivyo Marekani iki mbioni kuwafikia".

Alisema kuwa makampuni ya Marekani mpkaka sasa yamekuwa makini kuhusu kuwekezaji katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa kuhofia usalama na "hatari ya kimaadili" ya kushughulika na kile kinachoitwa "madini ya damu" - madini yanayofadhili uasi - lakini hii inaweza kubadilika wakati utawala wa Trump unatekeleza mpango wake wa amani.

Prof De Waal alisema hilo linaweza pia kutokea katika mataifa mengine yenye migogoro kama vile Sudan, ambako utawala wa Trump - pamoja na mataifa ya Kiarabu kama vile Saudi Arabia, Falme za Kiarabu na Misri - yalitarajiwa kushiriki katika juhudi za upatanishi baada ya mipango ya awali kushindwa.

Ameongeza kuwa mtindo wa amani wa utawala wa Trump hauwezi kupuuzwa, haswa ikiwa utasimamisha mapigano ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na mamilioni ya wengine kuyahama makazi yao katika migogoro ambayo imedumu kwa zaidi ya miaka 30 mashariki mwa Kongo DR.

"Trump anaweza kuwa upande tofauti katika kuzungumza, na kutikisa mambo," Prof De Waal alisema.

Lakini Prof Hanri Mostert, msomi wa sheria ya madini katika Chuo Kikuu cha Cape Town, Afrika Kusini, aliiambia BBC kwamba DR Congo "inakabiliwa na hatari itakalemaza mamlaka yake juu ya madini yake".

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo inaweza kujikuta ikiwa imefungwa katika mikataba kwa miaka mingi, badala ya kupata dhamana zisizo wazi za usalama, alisema.

Hii ilikuwa ukumbusho wa mikataba ya "ubadilishanaji wa rasilimali" iliyofuatiliwa na China na Urusi katika mataifa mengi ya Afrika, Prof Mostert aliongeza.

Alitolea mfano Angola, ambapo China ilijenga miundombinu mbadala ya mafuta.

"Hata wakati bei ya mafuta ilipopanda, Angola haikuweza kupata thamani yake zaidi," Prof Mostert alisema.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema mwaka 2023 kwamba DR Congo ilikadiriwa kuwa na hifadhi ya madini inayo thamani yake ni takriban dola trilioni 25 ($25trn).

Hii ilijumuisha madini ya kobalti, shaba, lithiamu, manganese na tantalum - zinazohitajika kutengeneza vifaa vya kielektroniki vinavyotumika katika kompyuta, magari ya umeme, simu za rununu, mitambo ya nishati ya upepo na vifaa vya kijeshi.

"Je, Congo italazimika kutoa cobalt yake kwa wawekezaji wa Marekani kwa muda gani? Je, itakuwa miaka 20 au miaka 50? Kweli hii ndio thamani ya amani?" Prof Mostert aliuliza.

Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Patrick Muyaya alithibitisha kwenye kipindi cha Newsday cha BBC mwezi Machi kwamba nchi yake ilitaka kuipatia Marekani "madini muhimu" kwa makubaliano ya usalama.

Kundi la waasi la M23 lilianzisha mashambulizi makubwa mapema mwaka huu, na kuteka maeneo makubwa ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na kusafirisha madini kuvuka mpaka hadi Rwanda, walisema wataalam wa Umoja wa Mataifa katika ripoti mapema mwezi huu.

Madini hayo yalichanganywa na uzalishaji wa Rwanda, na "usafirishaji wao uliofuata kwa watendaji wa chini ulifikia viwango ambavyo havijawahi kushuhudiwa", wataalam wa Umoja wa Mataifa waliongeza.

Rwanda inakanusha shutuma kwamba inaunga mkono M23, ingawa UN imetoa ushahidi kuwa ina maelfu ya wanajeshi nchini DR Congo.

Katika kile kinachoonekana kuwa ni jaribio la kushughulikia suala la usafirishaji haramu wa madini, mkataba wa amani uliosimamiwa na Marekani kati ya DR Congo na Rwanda unatoa "mfumo wa ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda" ambao bado unajadiliwa kati ya mataifa hayo mawili hasimu.

Hii "itahakikisha njia haramu za kujinufaisha kiuchumi zimedhibitiwa" na "ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote mbili na fursa za uwekezaji" zinazoundwa kwa ajili ya "ufanisi mkubwa - hasa kwa wakazi wa eneo hilo".

''Marekani itanufaika kutokana na haki nyingi za madini kutoka Congo kama sehemu ya makubaliano," Trump alisema, kabla ya mkataba wa amani uliotiwa saini na wawakilishi wa serikali hizo mbili tarehe 27 Juni huko Washington.

Mtafiti wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika Taasisi ya Utafiti wa Usalama yenye makao yake makuu nchini Afrika Kusini, Bram Verelst, aliiambia BBC kwamba mpango huo wa Marekani unakwenda sambamba na mwingine ukiongozwa na Qatar, mshirika wa karibu wa Marekani.

Bw Verelst alisema lengo la Marekani lilikuwa hasa katika mwelekeo wa kanda, wakati Qatar ilikuwa katika masuala ya ndani kati ya serikali ya DR Congo na kundi la waasi la M23 ambalo limeanzisha utawala wake mashariki baada ya kuuteka mji mkuu wa eneo hilo, Goma.

Prof Jason Stearns, mwanasayansi wa masuala ya kisiasa kutoka Canada ambaye ni mtaalamu katika eneo hilo, aliambia BBC kwamba Qatar, kama mataifa mengine ya Ghuba yenye utajiri wa mafuta, inatanua wigo wake barani Afrika "kiumarisha uwezo, ushawishi wake lakini pia kutafuta fursa za kiuchumi".

Aliongeza kuwa taifa hilo lilijihusisha na juhudi za upatanishi katika eneo la maziwa makuu kwa ombi la Rwanda, ambayo inahisi kuwa Marekani inapendelea DR Congo, jambo ambalo Washington inakanusha.

Prof Stearns anasema Qatar ina masilahi "makubwa" ya kiuchumi nchini Rwanda, akiashiria kuwa nchi hiyo ya Ghuba inajenga uwanja mpya wa ndege wa mabilioni ya dola mjini Kigali na iko mbini kununua asilimia 49 ya hisa katika shirika la ndege la taifa hilo.

Alieleza kuwa Marekani na Qatar zinashirikiana kwa karibu, kuidhibiti Rwanda kupitia michakato miwili kwa sababu "haitaki kuishia katika hali ambapo kuna makubaliano ya amani kati ya DR Congo na Rwanda, lakini Rwanda inasema: 'Hatuwadhibiti M23', na M23 inaendelea na mapigano [mzozo] mashariki mwa DR Congo".

"Kwa hivyo ni muhimu sana kwamba michakato hiyo miwili kufikia malengo kwa sababu wapatanishi wana uhusiano wa karibu," Prof Stearns aliongeza.

Chini ya mkataba huo wa amani, DR Congo na Rwanda zilikubali kuzindua "utaratibu wa uratibu wa usalama" ndani ya siku 30 za makubaliano ya 27 Juni.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi