Jinsi Liverpool ilivyochanganya mbinu za Klopp na Slot ili kuishinda Man City

Mkufunzi wa Liverpool Arne Slot ni shujaa wa Anfield baada ya kuanza vizuri alipomrithi Jurgen Klopp

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Phil Mc Nulty
    • Nafasi, Mwandishi mkuu wa soka Anfield
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Liverpool walileta mashambulizi kisha wakadhibiti mchezo. Mchanganyiko bora wa Kocha wa zamani Jurgen Klopp ambao ni Mchezo wa mashambulizi ya haraka kisha utulivu wa Kocha aliyechukua pahali pake Arne Slot.

Ilikuwa ni Manchester City, timu bora Uingereza wakati huu, ambayo ilijipata katika mtego huu wa kimbunga, kwa kweli wakitoswa nje ya kinyang’anyiro cha kuwania kushinda kombe la EPL kwa mara ya tano mfululizo.

Mfumo wa Kocha wa Liverpool Arne Slot umekuwa wa kupimwa, mbinu iliyo na utulivu ukilinganishwa na ule wa Klop uliokuwa na hamasa na jazba. Huu ulikuwa mchanganyiko wa mifumo yote miwili ambayo Manchester City ya Pep Guardiola ilishindwa kudhibiti.

Ushindi wa mabao mawili pekee ukionekana kama umewafanyia hisani City, matokeo ambayo yamewaacha wakiwa alama 11 nyuma ya Liverpool ambao pia wameweka pengo la alama tisa kati yao na Arsenal walio kwenye nafasi ya pili.

Huenda Mwezi wa Disemba ukawa ndio umeingia tu, msimu wa Ligi kuu ya kandanda England umeingia raundi 13 pekee, lakini tayari inaonekana kama itakuwa vigumu kwa timu yoyote kuishinda Liverpool ikiwa katika hali hii.

Guardiola na City wamecheza mechi saba mfululizo bila kuandikisha ushindi na kupoteza mechi nne za ligi mfululizo, lakini hawajawahi shuhudia wimbi la mashambulizi kutoka kwa timu pinzani kama walivyoshuhudia katika dakika za kwanza za mechi hiyo huku Liverpool wakicheza mchezo wa kupendeza.

Liverpool waliirarua City, wakinusa harufu ya damu kutoka kwa mpinzani wao aliyejeruhiwa.

Mlinda lango Stefan Ortega ambaye aliingia badala ya Kipa wa Brazil Ederson aliyetemwa nje, akiwa tarayi amejaribiwa mara kadhaa na Virgil van Dijk akipiga mlingoti kwa mpira wa kichwa kabla ya Cody Gakpo kuunganisha pasi safi kutoka kwa Mohamed Salah na kufunga bao la kwanza.

Hii ilikuwa baada ya dakika 12 pekee.

Si jambo dogo kwa Slot kurejesha kumbukumbu za Klopp katika ubora wake katika dakika 25 za kwanza – kwa kweli ni sifa kwake – kisha dakika 65 zilizosalia kocha huyo ambaye ni raia wa Uholanzi akaleta udhibiti wa kiufundi kwenye kikosi kilichojaa talanta ambacho alirithi kutoka kwa mtangulizi wake.

Mashambulizi ya kwanza ya Liverpool yaliiwacha City ikiwa imeduwaa.

Mashambulizi ya mapema ya Liverpool yalididimisha Man city

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Akizungumza baadaye, hata Slot alikiri kwamba timu yake ilikuwa na ubora wa hali ya juu.

“Mwisho wa siku matokeo ndio muhimu, lakini tulicheza mchezo mzuri sana,” alieleza BBC Match of the Day. "Ukitaka kushinda dhidi ya timu kama City unafaa kuwa mzuri katika kila sehemu ya mchezo.

Ulinzi wa juu, ulinzi wa chini, muundo, juu, chini, kila kitu. Wanakuletea changamoto nyingi

" Katika mechi yoyote unataka kuanza vizuri sana, lakini tulianza jinsi tulivyotaka. Jambo hilo husaidia sana maana ukianza vibaya basi mashabiki hawatakuwa na wewe.

" Ukianza namna hii, inawapa nguvu wachezaji. Na pia mashabiki watakupa motisha na hilo litakupa nguvu zaidi.”

Hakukuwa na shaka yoyote kuhusu msisimko ulioshuhudiwa uwanjani Anfield, ambao ulileta mhemko kufuatia mashambulizi ya mapema kutoka kwa Liverpool yaliowaacha City wakionekana kuwa na mshangao kwa kilichowapata.

Katika Robo hiyo ya kwanza, Liverpool walifurahia asilimia 61 ya umilisi wa mpira na walikuwa na mikwaju saba, huku City wakikosa hata mkwaju mmoja.

Ukweli ni kwamba, iliwachukua City hadi dakika ya 39 kuandikisha mkwaju wa aina yoyote ile – muda mrefu zaidi katika historia ya ligi kuu ya soka England tangu mwaka 2010.

Hadi wakati huo, ilikuwa mechi ya upande mmoja, shambulizi baada ya shambulizi.

Huo ndio ulikuwa ukubwa wa Liverpool katika umuliki wa mechi hiyo kiasi cha kuwa mfungaji wa bao la kwanza Gakpo alikuwa amegusa mpira katika kisanduku cha timu pinzani mara nane, zaidi kuliko mchanganyiko wa wachezaji wote wa Manchester city katika kipindi cha kwanza.

katika mechi yote, Liverpool waliilazimisha City kukimbia sana, kikosi cha Guardiola kikifikisha masafa ya kilomita 11.1 ikilinganishwa na wenyeji ambao walifikisha masafa aya kilomita 107.2.

Na ilionekana kama zilikuwa mbio za sakafuni maana katika mechi yote walidhalilishwa.

Jinsi Van Dijk alivyoonyesha umahiri na kumtuliza Haaland

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Jinsi Van Dijk alivyoonyesha umahiri na kumtuliza Haaland

Mchanganyiko wa mfumo wa zamani wa Klopp na mfumo mpya wa Slot

Wakati Liverpool walipoponyoka na taji lao pekee la EPL msimu wa 2019-20, walikuwa na alama 37 kutokana na kushinda mechi 12 na sare moja baada ya mechi 13 sawia na sasa, wakiongoza Leicester City kwa alama nane na Manchester City kwa alama tisa.

Msimu huo ulichukua mkondo huo huo, ukiisha bila mashabiki uwanjani, na hivi sasa inaonekana italazimu timu zinazoifukuza Liverpool kujitahidi sana ili kubadilisha mambo.

Uongozi wa Liverpool wa alama tisa ndio mkubwa zaidi kwao tangu siku ya mwisho ya msimu huo ambapo walishinda ligi wakiwa wameweka pengo la alama 18 kileleni.

Mchezo huu wa Liverpool ulikuwa na upepo wa kutishia wapinzani, mazowea ya kuingia polepole katika mechi kisha baadaye waanzishe mashambulizi ambayo yaliwaacha City wakiwa wameyumba, Ulinzi wa Kyle Walker na Ruben Dias ukionekana kujadiliana mapema kuhusu jinsi ya kukabiliana na mashambulizi hayo.

Hawakupata jawabu lolote, Dias akipokonywa mpira na Darwnin Nunez ambaye alikuwa ameingia katika kipindi cha pili, na kumuacha Luis Diaz pekee kabla ya kuangushwa na Ortega.

Salah alikamilisha mchezo kwa kufunga bao la pili kupitia mkwaju wa penalti kukiwa kumesalia dakika 12 pekee.

Takwimu zinaonyesha kuwa Liverpool walitumia mbinu ya moja kwa moja, huku asilimia 14.8 ya pasi zao zikiwa ndefu, ikilinganishwa na asilimia 9.1 kabla ya mechi hii.

Huu ulikuwa mfumo tofauti, mchanganyiko wa mfumo wa zamani wa Klopp na wa hivi sasa wa Slot.

Mpito wa kufana kutoka kwa Klop hadi Slot ulipitia mchujo mapema sana. Ya kwamba kila kitu kilikuwa shwari, lakini swali likawa je, ni nani wa maana sana ambaye wamecheza naye?

Jawabu limewasilishwa tena kwa kishindo uwanjani Anfield ndani ya siku tano, kwanza washikilizi wa ligi ya mabingwa barani ulaya Real madrid, kisha mabingwa watetezi wa EPL Manchester City wakazidiwa nguvu, ushindi sawia wa 2-0 ishara tosha ya ubabe wa Liverpool.

Maandishi ya Slot katika kikosi alichoachiwa na Klopp

Arne Slot anasema Liverpool ilikuwa imejipanga vyema kuishinda City

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Arne Slot anasema Liverpool ilikuwa imejipanga vyema kuishinda City

Dakika za mwisho, Guardiola akiwajibu mashabiki wa Liverpool waliokuwa wakimkejeli kwamba ataachishwa kazi asubuhi kwa kuwaonyesha vidole sita kuashiria mara sita alizonyakua kombe la EPL tangu ujio wake.

Vilevile huenda ikawa anaashiria kichapo alichopokea Anfield kama mkufunzi wa Manchester city katika ziara yake mara 10, akiwa amepata sare tatu na ushindi mmoja pekee, wa 4-1 wakati ambapo hakukuwa na mashabiki mnamo februari mwaka 2021.

Anfield pamekuwa pahala pagumu sana kwa Guardiola, na imedhihirika wazi mara kadhaa, hivi sasa cha kushangaza ni kuwa City haikuwa hata ndani ya timu nne bora EPL.

Upande mwengine, Maisha hayangekuwa bora zadi kwa Slot, ambaye ameweka rekodi ya kushinda mechi 18 kati ya 20 za kwanza.

Mlinzi joe Gomez ambaye aliingia kuchukua pahala pa Ibrahima Konate aliyejeruhiwa, alimsifu sana Slo – na pia Klopp – akieleza kikosi cha BBC’s Match of the Day: “ Nadhani jambo kubwa ni kuwa hajajaribu kuvaa viatu vya Klopp ama kuwa kama klopp.

"Historia iliyowekwa na Jurgen imepigwa muhuri katika historia ya klabu hii na haiwezi badilishwa.

Slot amekuwa yeye binafsi. Limekuwa jambo jipya na wafanyikazi wote wamekuwa na mtazamo chanya.

"Kazi bado haijafanyika. Hatujashinda chochote. Ni mwanzo mzuri sana na kila wakati yeye hutukumbusha kuwa tuendelee tena. Anajua tuna wachezaji walio na uzoefu mubwa katika kikosi chetu na yeye hutusukuma kila wakati.”

Maandishi ya Slot hivi sasa yako kwenye kikosi alichoachiwa na Klopp – na katika siku hii kubwa ya ushindi, Liverpool na Mshabiki wake wamefurahia ubora wa pande zote mbili.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Seif Abdalla