Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jack Teixeira: Mhudumu wa ndege Marekani ashtakiwa kwa kuvujisha nyaraka za Pentagon
Mhudumu wa ndege wa Marekani anayeshutumiwa kwa kuvujisha nyaraka za siri za kijasusi na ulinzi amefunguliwa mashtaka rasmi katika mahakama ya Boston.
Jack Teixeira, 21, alikuwa na pingu na sare ya gereza alipokuwa akisimama mbele ya hakimu wa serikali siku ya Ijumaa.
Baada ya sauti iliyosikika ikisema "nakupenda, Jack" kutoka kwa mtu mmoja katika chumba cha mahakama, mshtakiwa alijibu "mimi pia, baba".
Bw Teixeira anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 15 jela kwa tuhuma za kusambaza taarifa kuhusu ulinzi wa nchi bila kibali.
Pia anashtakiwa kwa kuondoa na kuhifadhi hati zilizoainishwa bila kibali.
Mhudumu huyo wa ndege anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 10 jela kwa shtaka la kwanza, na jela hadi miaka mitano kwa kosa la pili.
Nyaraka nyingi zilizovuja zilikuwa zimefichua tathmini za Marekani kuhusu vita vya Ukraine pamoja na siri nyeti kuhusu washirika wa Marekani.
Uvujaji huo uliaibisha Marekani na kuibua maswali mapya kuhusu usalama wa habari zilizoainishwa.
Kibali cha Usalama cha "Siri Kuu"
Nyenzo za kijasusi zilizovuja zilionekana kwa mara ya kwanza kwenye chumba cha mazungumzo ambacho Bw Teixeira anasemekana kuwa msimamizi.
Wanachama wake mara nyingi walijadili mambo ya kijiografia na vita.
Hati ya kiapo iliyotolewa na Ajenti Maalum wa Shirika la Ujasusi Marekani - FBI Patrick Lueckenhoff kwa mahakama -ilisema kuwa mshukiwa alianza kuchapisha stakabadhi hizo zilizovuja muda fulani mwezi wa Disemba.
Uvujaji wa awali ulikuwa katika mfumo wa aya za maandishi, kulingana na hati ya kiapo, lakini Bw Teixeira kisha akaendelea na kuchapisha picha za hati mnamo Januari.
Hadi nyenzo za kijasusi zilipochapishwa nje ya kundi la chumba cha mazungumzo ndipo maafisa wa Pentagon walipofahamu juu ya uvujaji huo, na kusababisha kutafutwa kwa mhalifu.
Bw Teixeira alifanya kazi kama mtaalamu wa IT katika kitengo cha ujasusi wa Walinzi wa Kitaifa wa Massachusetts, wenye makao yake katika Kituo cha Walinzi wa Kitaifa cha Otis Air huko magharibi mwa Cape Cod.
Walinzi wa Kitaifa ni wanajeshi wa akiba wa Jeshi la Wanahewa la Marekani. Hawajaajiriwa muda wote katika jeshi, lakini wanaweza kutumwa inapobidi.
Jina rasmi la nafasi kazini ya Bw Teixeira lilikuwa mlinzi wa masuala ya mtandao, kulingana na malalamiko ya jinai yaliyowasilishwa katika mahakama ya Boston.
Alishikilia cheo cha Airman 1st Class - nafasi ya chini kiasi.
Hati hiyo ya kiapo ilisema kuwa Bw Teixeira alikuwa na kibali cha usalama cha "siri kuu" tangu 2021, na kwamba angekuwa "ametia saini makubaliano ya maisha ya kutofichua siri" kuchukua jukumu lake.
Bw Luekenoff aliongeza mshukiwa "angelazimika kukiri kwamba ufichuzi usioidhinishwa wa habari zinazolindwa unaweza kusababisha mashtaka ya uhalifu".
Hati hiyo ya kiapo pia ilidai kuwa Bw Teixeira alitumia kompyuta yake ya serikali kutafuta taarifa za kijasusi za siri kwa kutumia neno "kuvuja" tarehe 6 Aprili - siku ambayo taarifa hizo za siri zilivuja kwa umma kwa mara ya kwanza.
Waendesha mashtaka walidai kuwa Bw Teixeira alitafuta neno hilo ili kujua ikiwa ujasusi wa Marekani ulikuwa na habari juu ya utambulisho wa mtu aliyehusika na uvujaji huo.
Nini kinaweza kutokea ikiwa atapatikana na hatia?
Sheria ya Ujasusi ilipopitishwa awali, ilitaja vifungo vya miaka 20 au chini ya hapo na faini ya hadi $10,000 kwa kila kosa.
"Huyu ni mtu ambaye anakabiliwa na kuangaziwa kwa miaka gerezani ... kwa sababu uvujaji ulikuwa mbaya sana," Brandon Van Grack, mwendesha mashitaka wa usalama wa kitaifa wa Idara ya Sheria sasa na kampuni ya mawakili ya Morrison Foerster, aliambia Reuters.
"Kwa hakika kuna mashtaka ya jinai ambayo yanaweza kushikamana nayo [Sheria ya Ujasusi] na kuna adhabu za kifedha pia," Bw Stransky alisema.
"Ikiwa idara ya haki inafuatilia ukiukaji wa jinai kwa Sheria ya Ujasusi, mara nyingi wanatafuta hukumu ya jela kama njia ya kuzuia aina hizi za vitendo vya siku zijazo."
Katibu wa waandishi wa habari wa Pentagon alionyesha kwamba ingeshughulikia uvujaji huo kwa umakini mkubwa, akisema ni "kitendo cha uhalifu cha makusudi".
Msemaji wa Pentagon alisema kuwa miongozo "mikali" iliwekwa kwa wafanyikazi na kwamba "mtu yeyote anayekiuka sheria hizo anafanya hivyo kwa makusudi".
Bw Teixeira alikamatwa na maafisa wa FBI waliokuwa na silaha nyumbani kwake Massachusetts siku ya Alhamisi.
Jaji aliamua kuwa mshukiwa anahitimu kuwa mtetezi wa umma - wakili aliyeajiriwa kwa gharama ya umma katika kesi ya jinai kwa watu ambao hawawezi kumudu ada za kisheria.
Bw Teixeira bado yuko kizuizini.
Rais wa Marekani Joe Biden alishukuru utekelezaji wa sheria katika taarifa kwa "hatua yao ya haraka" ya kuchunguza chanzo cha uvujaji huo.
Alisema ameelekeza jeshi la Marekani na kijasusi kulinda na kupunguza usambazaji wa taarifa zozote nyeti zaidi.