Jack Teixeira: Tunachojua kuhusu anayetuhumiwa kuvujisha nyaraka za Pentagon

Lilikuwa ni kundi la binafsi la mtandaoni lililokuwa na machapisho kuhusu michezo ya video, bunduki, memes - na faili za siri za Marekani.

Mshukiwa wa uvujaji huo ambao umeaibisha Marekani na washirika wake ametajwa kama Mlinzi wa Kitaifa wa Ndege Jack Douglas Teixeira, 21.

Miongoni mwa vijana katika chumba cha mazungumzo kiitwacho Thug Shaker Central kwenye mtandao wa kijamii maarufu kwa wachezaji, aliripotiwa kujulikana kama "OG".

Sasa anakabiliwa na mashtaka chini ya Sheria ya Ujasusi.

Alijiunga na kikosi hicho mwaka wa 2019 na aliandikishwa katika Kamandi ya 102 ya Ujasusi wa Walinzi wa Kitaifa wa Wanaanga wa Massachusetts - ambao ni akiba ya Jeshi la Wanaanga la Marekani.

Bw Teixeira alipandishwa cheo Julai mwaka jana hadi Airman 1st Class - nafasi ya chini kiasi - na alikuwa na makao yake katika kambi ya Otis Air National Guard huko magharibi mwa Cape Cod.

Kulingana na rekodi yake ya utumishi, nafasi yake rasmi ni mtaalamu wa mifumo ya Mtandao.

Tovuti rasmi ya Jeshi la Anga inabainisha kuwa wafanyakazi waliopewa kazi za Mifumo ya Usafiri wa Mtandaoni wanawajibika kuendesha mtandao mkubwa wa mawasiliano wa kimataifa wa Jeshi la Anga, unaounganisha vitengo vinavyofanya kazi Marekani na ng'ambo.

Maafisa wa ulinzi wamesema kuwa kazi kama hizo zinaweza kujumuisha ukarabati wa vitovu vya mtandao nchini Marekani au mifumo ya mawasiliano ya fibre-optic katika vituo vya nje ya nchi, kwa mfano. Rekodi ya Bw Teixeira haipendekezi kupelekwa ng'ambo.

Familia ya Bw Teixeira inaripotiwa kuwa na historia ndefu ya utumishi wa kijeshi. Baba yake wa kambo, Thomas Dufault, alistaafu baada ya miaka 34 ya huduma, kulingana na Washington Post. Chapisho lake la mwisho lilikuwa kama sajenti mkuu kutoka kitengo cha Bw Teixeira, Kamandi ya 102 ya Ujasusi.

Mama yake, Dawn Dufault, amewahi kufanya kazi katika mashirika yasiyo ya faida yaliyolenga maveterani, pamoja na Idara ya Huduma za Veterani ya Massachusetts, kulingana na LinkedIn na rekodi za umma zilizotajwa na vyombo vya habari vya Marekani.

Bw Teixeira aliripotiwa kujulikana kama kiongozi wa mazungumzo ya kundi lililoundwa mnamo 2020.

Thug Shaker Central ilijumuisha takribani wanachama 20 hadi 30 - wengi wao wakiwa vijana - kutoka nchi mbalimbali.

Gazeti la Washington Post liliripoti kwamba kikundi hicho kilikuwa kimebadilishana "meme, vicheshi vya kukera na chitchat", walitazama filamu pamoja.

Mwanachama wa chumba cha mazungumzo alisema Bw Teixeira alikuwa kijana, mpenda bunduki mwenye haiba.

Wanachama wengine waliliambia gazeti la New York Times kwamba Bw Teixeira alikuwa mkubwa kwa umri kuliko wengi katika kundi na alionekana kuwa na nia ya kuwavutia.

Gazeti la The Post liliripoti kuwa aliliambia kundi hilo kuwa alifanya kazi katika kituo ambacho simu zilipigwa marufuku.

Hapo awali aliandika matoleo ya habari nyeti na kuishiriki kwenye chumba cha mazungumzo.

Lakini alianza kushiriki picha za faili hizo baada ya kuripotiwa kuwa na "hasira" zaidi wakati wanachama wengine wa chumba cha mazungumzo hawakuzingatia.

Wakati fulani, gazeti la Post liliripoti, alituma ujumbe uliokasirishwa kwa kikundi ambapo alilalamika kwamba walivutiwa zaidi na video za YouTube kuliko machapisho yake kuhusu hati, ambayo mwanachama alielezea kuwa imejaa "ufafanuzi na maelezo ya mambo ambayo sisi wananchi wa kawaida tusingeelewa”.

"Alikasirika, na alisema mara kadhaa, ikiwa nyinyi hamtawasiliana nao, nitaacha kuwatuma," mwanakikundi huyo ambaye hakutambulika aliliambia gazeti hilo.

Wanachama wa kikundi cha mtandaoni wanaonekana kuwa na maoni yanayokinzana kwa nini Bw Teixeira alishiriki hati hizi.

"Kijana huyu alikuwa Mkristo, aliyepinga vita, alitaka tu kuwajulisha baadhi ya marafiki zake kuhusu kile kinachoendelea," kijana mmoja aliiambia The New York Times.

Mwanachama mwingine alisema Bw Teixeira alikuwa "mtu mwerevu".

"Alijua alichokuwa akifanya alipochapisha hati hizi, bila shaka," mwanachama huyo aliliambia Washington Post.

Nyumba ya familia ya Bw Teixeira iko maili 40 (64km) kusini mwa Boston huko North Dighton, Massachusetts.

Picha za angani zilionesha takribani maafisa dazeni wa FBI wakizunguka eneo lake la makazi na kumkamata Bw Teixeira siku ya Alhamisi.

Bw Teixeira alihitimu mwaka wa 2020 kutoka Shule ya sekondari ya Mkoa ya Dighton-Rehoboth, inaripoti CBS News, mshirika wa BBC wa Marekani.