Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Ukraine: Uvujaji unaonyesha vikosi maalum vya Magharibi vipo Ukraine
Uingereza ni miongoni mwa nchi kadhaa zilizo na vikosi maalum vya kijeshi vinavyohudumu ndani ya Ukraine, kulingana na moja ya nyaraka nyingi zilizovuja mtandaoni.
Inathibitisha kile ambacho kimekuwa mada ya uvumi wa kimya kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Faili zilizovuja, baadhi zikiwa na alama ya "siri kuu", zinatoa picha ya kina ya vita vya Ukraine, ikiwa ni pamoja na maelezo nyeti ya maandalizi ya Ukraine ya kufanya mashambulio ya majira ya kuchipua.
Serikali ya Marekani inasema inachunguza chanzo cha uvujaji huo.
Kwa mujibu wa waraka huo, wa tarehe 23 Machi, Uingereza ina kikosi kikubwa zaidi cha vikosi maalum nchini Ukraine (50), ikifuatiwa na mataifa mengine ya Nato Latvia (17), Ufaransa (15), Marekani (14) na Uholanzi (1). .
Hati hiyo haisemi vikosi hivyo viko wapi au vinafanya nini.
Idadi ya wanajeshi hao maalum inaweza kuwa ndogo, na bila shaka itabadilika. Lakini vikosi maalum kwa asili yao ni bora sana. Uwepo wao nchini Ukraine huenda ukatumiwa na Moscow, kwa malengo yake ya kuendeleza Propaganda kwani katika miezi ya hivi karibuni imesema kuwa haikabiliani tu na Ukraine, bali Nato pia.
Kwa mujibu wa sera yake ya kawaida juu ya masuala kama hayo, Wizara ya Ulinzi ya Uingereza haijatoa maoni yoyote, lakini katika ujumbe wa Twitter siku ya Jumanne ilisema uvujaji wa habari za siri umeonyesha kile ilichokiita "kiwango kikubwa cha kutokuwa sahihi".
"Wasomaji wanapaswa kuwa waangalifu kuhusu kuamini madai ambayo yana uwezo wa kueneza habari potofu," ilisema.
Haikufafanua au kupendekeza ni hati gani mahususi ilikuwa inarejelea. Hata hivyo, maafisa wa Pentagon wamenukuliwa wakisema nyaraka hizo ni za kweli.
Hati moja, ambayo ilieleza kwa kina idadi ya waliopoteza maisha nchini Ukraine kwa pande zote mbili, ilionekana kuwa imefanyiwa ukarabati.
Vikosi maalum vya Uingereza vinaundwa na vitengo kadhaa vya kijeshi vya wasomi vilivyo na maeneo tofauti ya utaalam, na vinachukuliwa kuwa kati ya vikosi vyenye uwezo zaidi ulimwenguni.
Serikali ya Uingereza ina sera ya kutotoa maoni yoyote kuhusu vikosi vyake maalum, tofauti na nchi nyingine ikiwa ni pamoja na Marekani.
Uingereza imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono Ukraine, na ni mfadhili wa pili kwa ukubwa baada ya Marekani wa msaada wa kijeshi kwa Kyiv.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin alisema Idara ya Sheria imefungua uchunguzi wa jinai na amedhamiria kutafuta chanzo cha uvujaji huo.
“Tutaendelea kuchunguza na kugeuza kila mwamba hadi tupate chanzo cha jambo hili na ukubwa wake,” alisema.