Kwanini kuna upinzani dhidi ya ufugaji ndevu na kufunika uso Asia ya Kati?

    • Author, Kubat Chekirov
    • Nafasi, BBC

Nchini Kyrgyzstan, muswada wa sheria ya kupiga marufuku uvaaji wa nguo za kufunika uso na ufugaji ndevu refu umepelekwa kwa umma ili kujadiliwa. Mijadala mikali sana imefanyika. Wapo watetezi na wapinzani.

Rasimu hiyo inalenga kutoza faini ya pesa au saa 30-40 za utumishi wa umma kwa wale wanaofunika nyuso zao na kufuga ndevu refu.

Muswada huo umeletwa ili kuzuia mavazi hayo sehemu za umma na kuhakikisha usalama wa umma - kwani aina hiyo ya mavazi huzuia utambulisho wa mtu.

"Rasimu inalenga kuweka uwiano kati ya kuheshimu imani za kidini na hitaji la usalama wa umma. Inalenga kuwafanya watu wa jamii zote kuishi pamoja kwa kuzingatia kanuni za msingi za uhuru wa raia na sheria za usalama katika maeneo ya umma," unaeleza muswada huo.

Wanaounga mkono Muswada

Katika mila ya Wakyrgyz, wasichana na wanawake hawavai mitandio ya kufunika nyuso na vijana wa kiume hawafugi ndevu. Lakini wanawake wanaofunika nyuso zao na wanaume wanao fuga ndevu katika miaka ya hivi karibuni wanabadilisha mila hiyo.

Muswada uliowasilishwa na Mbunge Sharapatkan Majitova unatokana na wasiwasi wa umma kuhusu jambo hilo.

“Idadi ya watu wanaovaa hijabu inaongezeka, sisemi wasivae, waache wavae, lakini kujifunika uso ni hatari na kunaathiri usalama. Nimeshawaambia viongozi wa dini. Serikali haiwezi kukaa bila kutoa amri na kuchukua hatua," anasema Majitova.

Katika hotuba ya hivi karibuni, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Chama cha Kikomunisti cha Kyrgyzstan, Kamchybek Tashiev, alitoa wito wa kuimarishwa kwa mapambano dhidi ya ushabiki wa kidini - ambao unajaribu kugeuza mila na tamaduni za muda mrefu.

"Siyo siri sasa kuna watu wengi ambao wanatofautiana na desturi ya Uislamu wa mababu zetu, wanaweka sheria na matakwa yaliyopotoka ya dini yetu, kuvaa nguo tofauti na za jamii yetu, na kufanya vitendo vya ushabiki wa kidini usioendana na uislamu wa jadi.''

''Watoto wetu wa miaka 20 na 25 hawakufuga ndevu hadi kwenye vitovu. Hakuna anayekwambia usifuge ndevu, zikuze kwa utaratibu. Vaa kitambaa, ishi vizuri, lakini usituletee mila za mataifa mengine na madhehebu mengine ya kidini," anasema Tashiev.

Wanaopinga Muswada

Viongozi wa dini ya Kiislamu wa Kyrgyzstan, wameonyesha upinzani kwa mswada huu. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, wanawake wanaruhusiwa kufunika mikono, miguu na uso, huku sehemu nyingine ya mwili ni lazima kufunikwa.

"Baadhi ya wanawake hufunika nyuso zao kwa nikabu, huu ni uamuzi wao. Hata hivyo niqab si wajibu, ni hiyari," Mufti alieleza. Ama kuhusu ndevu, Mufti anasema ni Sunnah, na ndevu ziwe safi na maridadi.

Licha ya muswada huo dhidi ya kufunika uso na ndevu, wapo pia wanaoamini hakuna haja ya kuzipiga marufuku na kutoza watu faini, katika karne ya 21 kila mtu avae apendavyo.

Wale waliopendekeza muswada huu wanasema kupitishwa kwa sheria hiyo hakutasababisha madhara ya kijamii, kiuchumi, kisheria, jinsia, mazingira au rushwa, na umependekezwa kwa kuzingatia kanuni za kikatiba, sheria na viwango vya kimataifa.

Sheria Zinasemaje?

Mtaalamu wa sheria, Tattybubu Ergeshbaeva, anaeleza maoni yake ya kisheria kuhusu muswada huu, ''sina cha kusema kuhusu ndevu, lakini haiwezekani kumtambua mtu bila kuonyesha uso wake.''

"Ndevu zozote kubwa hazizuii utambulisho wa uso. Kwa hivyo, ni kitu cha kawaida kwa wanaume. Ama nikabu ni nguo ambazo haziruhusu utambulisho wa uso.

Hijabu inaweza kuruhusiwa. Katika muktadha wa sheria - haijakataza kuvaa nguo zisizoruhusu utambulisho wa uso katika maeneo ya umma.''

Uzbekistan

Mbunge Sharapatkan Majitova anasema alipata wazo la kuandaa muswada dhidi ya ndevu refu na kufunika uso kutoka Uzbekistan.

Kwa mujibu wa sheria za Uzbekistan, ni marufuku kuvaa nguo za kidini katika maeneo ya umma, isipokuwa kwa wale wanaofanya kazi katika mashirika ya kidini. Pia, baadhi ya shule haziruhusu wanafunzi kuvaa hijabu.

Kuna ripoti kwamba wanaume kumi wenye ndevu walikamatwa na kufungwa kwa siku 15 huko Tashkent.

2019 Gavana wa mkoa wa Fergana alivitaka vyombo vya kusimamia sheria vikamate watu wenye ndevu na kunyoa ndevu zao.

Vizuizi vingi vilianzishwa wakati nchi ikitawaliwa na Islam Karimov. Baada ya shambulio la kigaidi Tashkent 1999 na maandamano huko Anjian 2005. Ilikuwa kawaida kuwakamata wanaume wenye ndevu mitaani na kuwaweka ndani.

Kwa sasa wenye ndevu wanatembea na hawaguswi, hata hivyo kuna matukio ya polisi kufanya msako na kuwakamata. Mfano mwaka jana, walifanya uvamizi katika jengo la Malika, wakakamata watu wenye ndevu na kuwachukua.

Mwaka huu walianzisha nyongeza ya sheria, mtu akifunika uso wake na hakuna njia ya kumtambua, hatua zitachukuliwa dhidi yake.

Tajikistan

Rais Emomali Sharipovich wa Tajikistan ndiye wa kwanza kuwapinga watu wenye ndevu. Vilevile kuvaa hijab ni marufuku katika taasisi za umma na maeneo ya umma.

Mamlaka zimekuwa zikipinga uvaaji wa mavazi ya Kiislamu, na mwaka 2017 wanawake walipigwa marufuku kuingia kwenye kumbi za harusi wakiwa wamevaa hijabu.

Wanaume wenye ndevu refu hawawezi kutembea kwa uhuru mitaani. Rais Emomali Rahmon anasema sio dalili ya Uislamu, na ametaka watu kumwabudu Mungu kutoka moyoni na sio kwa sifa za nje.

Mwaka 2015, iliripotiwa kuwa wanaume 13,000 walinyolewa kwa nguvu wakiwa wameshikilia ndevu zao katika mkoa wa Khatlon.

Afrika na Ulaya

Katika baadhi ya nchi, niqabu inachukuliwa kuwa tishio la usalama. Vazi hilo limepigwa marufuku katika nchi za Afrika kama Chad, Gabon, Congo-Brazzaville na Cameroon.

Nchini Chad, mwaka 2015, mshambuliaji aliyejifunika uso alijitoa mhanga katika mji mkuu, N'Djamen, na kuua watu 33.

2010, Ufaransa ikawa nchi ya kwanza barani Ulaya kupiga marufuku kufunika uso kwa wanaume na wanawake katika maeneo ya umma.

Takriban Waislamu milioni tano wanaishi Ufaransa, nchi ambayo ina Waislamu wengi zaidi katika nchi za Ulaya Magharibi. Karibu elfu mbili kati yao huvaa mavazi ya kiislamu.

Ubelgiji ilifuata nyayo za Ufaransa 2012 - ilipiga marufuku uvaaji wa mavazi ambayo yanazuia watu kutambuliwa hadharani.

Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi