Wanaakiolojia waugundua mskiti wa miaka 1,200 chini ya ardhi jangwani Israel

Mojawapo ya misikiti ya kwanza iliyotambulika duniani, uliojengwa takriban miaka 1,200 iliyopita, umegunduliwa na wanaakiolojia katika jangwa la Negev nchini Israel.

Masalio hayo, ya kutoka karne ya 7 au ya 8 yaligunduliwa katika mji wa Bedouin - Rahat.

Mamlaka inayosimamia vitu vya kale Israel (IAA) inasema msikiti huo uligunduliwa chini ya ardhi wakati wa ujenzi katika enoe hilo.

Ni mskiti wa kwanza unaotambulika katika eneo hilo kutoka wakati huo, ukishindana kwa umri na yale yaliogunduliwa Makka na Jerusalem, IAA limesema.

Watafiti Jon Seligman na Shahar Zur wanasema mskiti, wa kutoka karne ya 7 au 8 ni jambo adimu kuligundua kokote.

Watafiti wanaamini huenda wakulima wa eneo hilo ndio waliokuwa waumini waliosali katika msikiti huo.

Jengo hilo lilikuwa la wazi, lenye umbo la mstatili na lilikuwa na "Mihrab" - au upembe anaosimama muongoza sala linaloelekea mji mtukufu wa Makka au Qibla.

"Huu ni ushahidi wa lengo la jengo hili na lilivyotumika miaka mia kadhaa iliyopita," amesema Seligman.

Ni mojawapo ya misikiti ya kwanza baada yakuwasili kwa Uislamu katika inayojulikana hii leo kama Israel wakati waraabu walipolitawala jimbo la Byzantine mnamo mwaka 636, kwa mujibu wa Gideon Avni, mtaalamu wa historia ya kale ya uislamu.

"Ugunduzi wa kijiji na msikiti katika eneo hilo ni mchango muhimu katika uchunguzi wa historia ya nchi hiyo wakati wa kipindi hicho kigumu," amesema.

Getty na Mamlaka ya vitu vya kale Israeli, zinamiliki haki zote miliki za picha hizi.