Marwan Issa: Mfahamu Kamanda wa Hamas ambaye Israel inadai kumlenga katika handaki

hgb

Chanzo cha picha, WALA

Maelezo ya picha, Uso wake haukujulikana kabla ya picha hii.

Jeshi la Israel limetangaza lilimlenga kiongozi namba mbili wa kundi la kijeshi la Al-Qassam la Hamas, Marwan Issa, katika shambulio la anga karibu na kambi ya Nuseirat katikati mwa Ukanda wa Gaza.

Jeshi la Israel limesema bado linajaribu kuthibitisha ikiwa Issa aliuawa katika shambulio hilo, wakati Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Galant anaamini Marwan Issa alikuwa katika handaki wakati wa shambulio hilo.

JHN

Chanzo cha picha, Al-Aqsa TV

Maelezo ya picha, Kivuli cha Marwan Issa akihojiwa na Al-Aqsa TV.

Msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari alisema, "handaki lililolengwa lilitumiwa na viongozi wawili wakuu wa Hamas; Marwan Issa na Ghazi Abu Tamaa, ambaye kwa sasa anafanya kazi ya kusimamia mbinu za mapambano za Hamas.

Tovuti ya Israel 24 iliripoti Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alidokeza katika video juu ya shambulio dhidi ya Marwan Issa, aliposema:

"Tunaendelea na njia ya kukamilisha ushindi. Tayari tumemwondoa namba 4 wa Hamas (akimaanisha Saleh Al Arouri, afisa wa vuguvugu la Ukingo wa Magharibi) na namba 3, 2, na 1 wako njiani. Wote ni watu wa kufa, na tutawafikia mmoja baada ya mwingine.”

Netanyahu anaashiria mkuu wa vuguvugu la Ukanda wa Gaza, Yahya Sinwar, wa pili Muhammad al-Deif, kiongozi wa tawi la kijeshi la harakati hiyo na wa tatu anaashiria ni Marwan Issa.

Israel inasema Isaa alihusika katika kupanga, pamoja na kiongozi Muhammad al-Deif, shambulio la Oktoba 7, lililosababisha vifo vya zaidi ya watu 1,200.

Marwan Issa ni nani?

B

Chanzo cha picha, IDF

Maelezo ya picha, Picha ya angani, Israel inasema ni eneo ambalo Marwan Issa alikuwepo

Marwan Issa, Mkuu wa Wafanyakazi wa Al-Qassam, wadhifa ambao kwa kawaida hupewa Naibu Kamanda Mkuu wa Brigedi za Izz al-Din al-Qassam. Pia ni mwanachama wa ofisi ya kisiasa na kijeshi ya harakati ya Hamas.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Alizaliwa mwaka 1965 katika kambi ya wakimbizi ya Bureij katikati mwa Ukanda wa Gaza. Haijulikani mwaka gani alijiunga na Hamas baada ya kuasisiwa vikosi vya Al-Qassam mwaka 1987.

Issa alifungwa jela nchini Israel kwa miaka mitano kwa kuhusika kwake katika mashambulizi dhidi ya Israel, na pia inadaiwa alinusurika katika jaribio la jeshi la Israel la kumuua mwaka 2006.

Juni 25, 2006, Hamas ilimkamata mwanajeshi wa Israel Gilad Shalit, wakati huo akiwa na umri wa miaka 19, na kumshikilia kama sehemu ya mpango wa kubadilishana wafungwa uliojadiliwa Oktoba 2011.

Uso wake haukujulikana kabla ya 2011, lakini alionekana katika picha ya pamoja iliyopigwa wakati wa mapokezi ya wafungwa walioachiliwa katika mpango wa kubadilishana na askari Shalit.

Novemba 14, 2012, jeshi la Israel lilianzisha mashambulizi kadhaa ya anga kwenye Ukanda wa Gaza, na kumuua Ahmed al-Jaabari, naibu wa Muhammad al-Deif. Issa alilengwa katika uvamizi huo lakini alinusurika, na kumrithi al-Jaabari katika nafasi yake.

DXC

Chanzo cha picha, SOCIAL MEDIA

Maelezo ya picha, Muhammad, mtoto wa kiume wa Marwan Issa, aliuawa kutokana na shambulio la Israel, kulingana na vyombo vya habari vya Palestina.

Ndege za kivita za Israel pia ziliharibu nyumba yake mara mbili wakati wa vita huko Gaza mwaka 2014 na 2021, na kusababisha kifo cha kaka yake.

Januari 2019, wanachama wa kitengo cha usalama cha Hamas waligundua vifaa vya kijasusi ambavyo vilikuwa kwenye nyumba karibu na nyumba ya Issa, na kuviharibu, kulingana na gazeti la Al-Akhbar, ambalo liko karibu na Hezbollah.

Hii haikuwa mara ya kwanza kwa Israel kujaribu kumfikia Issa, kwani vitengo vya Hamas vilifichua kifaa kingine cha kijasusi ambacho wakala alikuwa amekitega kwenye gari la rafiki wa Issa.

Wakala huyo alikiri alipokea kifaa hicho kidogo kutoka Israel na kisha kukiweka katika eneo ndani ya gari na ikabainika kuwa kilikusudiwa kufanya upelelezi wa sauti kwa waliokuwa ndani ya gari pamoja na kufuatilia.

Kifaa cha kijasusi pia kiliwekwa kwenye mtandao wa mawasiliano ya kibinafsi katika eneo analoishi Issa.

Mwezi Septemba 10, 2019, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilimuweka Issa katika orodha ya magaidi kwa nafasi yake kama kiongozi wa Hamas.

Tarehe 8 Disemba, Umoja wa Ulaya ulimwongeza Kamanda Mkuu wa Brigedi za Al-Qassam, Muhammad Al-Deif, na naibu wake, Marwan Issa, kwenye orodha yake ya magaidi wa kimataifa.

Mwishoni mwa Disemba, vyanzo vya ndani vya Palestina viliripoti kuuawa kwa mtoto wa Marwan Issa aitwaye Muhammad katika shambulio la Israel katikati mwa Ukanda wa Gaza.

Sura ya Marwan Issa

V

Chanzo cha picha, WALA

Maelezo ya picha, Alichagua kusimama nyuma ya kila mtu na alikuwa amevaa barakoa.

Gazeti la Israel, Walla linasema: Picha hii ni ya wajumbe wa ofisi ya kisiasa ya vuguvugu la Hamas baada ya uchaguzi wa ndani uliofanyika mwaka 2021.

Miongoni mwa ishirini wanaoonekana kwenye picha hii, wakiongozwa na Sinwar na wanawake wawili, mmoja wa watu hao ni Marwan Abdel Karim Issa.

Hivyo ndivyo jina lake linavyoonekana katika orodha ya watu kwenye kompyuta za waratibu wa shughuli za serikali ya Gaza.

Nafasi yake ya sasa ni naibu mkuu wa tawi la kijeshi la vuguvugu la Hamas. Alichagua kusimama nyuma ya kila mtu na alikuwa amevalia barakoa ya kujikinga dhidi ya virusi vya uviko 19.

Vikosi vya Al-Qassam vinaongozwa na Muhammad al-Deif (kamanda mkuu), Marwan Issa (naibu wake), na Abu Ubaida (msemaji rasmi).

Wakati wa vita vinavyoendelea Israel ilitangaza kuuawa kwa baadhi ya viongozi wakuu wa Brigedi za Qassam, na Hamas ilithibitisha kuuawa kwa baadhi yao.

Baadhi ya makanda waliouwawa ni Ahmed Al-Ghandour (Abu Anas), kiongozi mkuu wa tatu wa Brigedi za Qassam na ni kamanda wa kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.

Mwingine ni Ayman Nofal (Abu Ahmed) mjumbe wa Baraza la Kijeshi na kamanda, Saleh Al-Arouri, afisa wa harakati hiyo katika Ukingo wa Magharibi. Mwingine ni Murad Abu Murad, kamanda wa kundi la anga la Hamas, Ayman Siyam, mkuu wa uundaji wa kijeshi kwa miaka 15.

Pia yupo Issam Abu Rukba, kamanda wa kikosi cha anga cha Hamas, na Ibrahim al-Biyari, kamanda wa kikosi cha kati cha Jabalia.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah