Ibrahim Traoré: Je, licha ya hotuba zake za kupinga ubeberu ni sahihi kumlinganisha na Thomas Sankara?

Rais wa zamani wa Burkina Faso Thomas Sankara

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa zamani wa Burkina Faso Thomas Sankara
Muda wa kusoma: Dakika 6

Akiwa kipenzi cha vijana wengi barani Afrika, Kapteni Ibrahim Traoré maarufu kwa jina la [IB] ambaye alitwaa madaraka nchini Burkina Faso takriban miaka mitatu iliyopita, anaendelea kuonesha mfanano wa wazi na kapteni wa mapinduzi wa miaka ya 1980, Thomas Sankara.

Miaka 35 baada ya kuuawa kwa Sankara mnamo Oktoba 15, 1987, sura mpya ya kisiasa na kijeshi ilichomoza nchini humo kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya Septemba 30, 2022.

Tangu wakati huo, Ibrahim Traoré amejiimarisha kama kiongozi mwenye ushawishi mkubwa katika siasa za taifa hilo la Afrika Magharibi.

Kwa hotuba zake kali, mwonekano wake wa kijeshi (akiwa na kofia nyekundu, bastola kiunoni na glavu mikononi), pamoja na mtindo wake wa mawasiliano unaojikita kwa lugha ya watu wa kawaida, Traoré anajenga taswira ya kiongozi wa karibu na wananchi sawa na ile ya Thomas Sankara.

Kwa wengi, yeye ni mwendelezaji wa maono ya Sankara.

Pia unaweza kusoma:
Kapteni Ibrahim Traoré, rais mpya wa Burkina Faso, akiwa katika picha ya pamoja na mwenge uliotolewa na wanamapinduzi wa zamani wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 35 tangu kuuawa kwa Thomas Sankara, huko Ouagadougou, Oktoba 15, 2022.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kapteni Ibrahim Traoré, rais mpya wa Burkina Faso, akiwa katika picha ya pamoja na mwenge uliotolewa na wanamapinduzi wa zamani wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 35 tangu kuuawa kwa Thomas Sankara, huko Ouagadougou, Oktoba 15, 2022.

Uzalendo na kupinga ubeberu: Sifa zinazowaunganisha

Wendyam Hervé Lankoandé, mchambuzi huru wa siasa nchini Burkina Faso, anasema:

"Kapteni Traoré anachukua baadhi ya misingi ya kihotuba ya Thomas Sankara: anazungumza moja kwa moja kwa lugha nyepesi inayofikika kwa wananchi wa kawaida, na anasisitiza uhuru wa taifa katika uamuzi wake wa kisiasa na kiuchumi."

Ingawa muktadha wa kisiasa wa sasa ni tofauti na ule wa miaka ya 1980, Lankoandé anaona mfanano wa msingi baina ya wawili hao, si tu kwa kuwa wote ni wanajeshi na waliwahi kuwa makamanda wa nchi, bali pia kwa misimamo yao ya kitaifa na kijamaa.

"Wote wawili wamejipambanua kimataifa kama wazalendo wenye msimamo dhidi ya ubeberu, wakionesha dhamira ya kuvunja uhusiano wa kiunyonyaji na tabaka la kisiasa la ndani waliloliona kama dhaifu na lisiloaminika," anaongeza Wendyam alipozungumza na BBC Afrique.

Aidha, Sankara na Traoré wanaonekana kushabihiana katika jitihada za kuimarisha ushirikiano na wananchi na kukuza maendeleo ya ndani yanayojengwa juu ya uwezo wa kitaifa.

Soma pia:

Bruno Jaffré, mtaalamu wa historia ya kisiasa ya Burkina Faso na mwandishi wa vitabu vya kumbukumbu kuhusu Sankara kama The Sankara Years na Thomas Sankara: The Homeland or Death [1997], Freedom against Destiny, (2017), anakubaliana kwa kiasi fulani na mlinganisho huu lakini pia anatahadharisha.

Anasema,

"Ni kweli kwamba Ibrahim Traoré anaonesha mwelekeo wa kupinga ubeberu, lakini kwa mtazamo wangu, zaidi ni msimamo wa kupinga Ufaransa pekee. Sijawahi kusikia kauli yake dhidi ya Marekani ilhali Marekani ndiyo kinara wa ubeberu wa Kimagharibi kwa ujumla."

Kwa Jaffré, tofauti nyingine kuu ni kuwa IB tayari amesaini mikataba na taasisi kama IMF na Benki ya Dunia, jambo ambalo lilipingwa vikali na Sankara katika uongozi wake.

Kujenga uchumi wa ndani: lengo la pamoja

gg

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wendyam Hervé Lankoandé anakumbusha kuwa Sankara alikuwa na ndoto ya kujenga Burkina Faso mpya kwa ngazi zote, kupitia sera za umma zilizolenga kuondoa umasikini na utegemezi wa kiuchumi.

Kwa upande wake, Ibrahim Traoré anajikita zaidi katika vita dhidi ya ugaidi wa kijihadi, ambavyo ni msingi wa utawala wake.

''Amechagua kutegemea nguvu za ndani, ikiwa ni pamoja na uundaji wa vikundi vya kujitolea vya kulinda taifa (VDP) na ufadhili wa operesheni hizo kupitia michango ya wazalendo.''Lankoandé anasema:

"Hili ni jambo linaloendana na roho ya Sankarism."

Kwake yeye, moja ya mambo wanayoshabihiana kati ya Ibrahim Traoré na Thomas Sankara ni katika mradi wao wa kujenga uchumi wa asili.

"Ndiyo, kuna juhudi fulani za kupambana na utegemezi. Kuna viwanda vinavyoanzishwa ili kuchakata bidhaa ndani ya nchi, na juhudi za kuuza bidhaa za kitaifa, taifa hilo likionekana lina utajiri kutokana na dhahabu zinazomiliki. Lakini bado taarifa hizo zimegubikwa na propaganda kuliko tathmini huru." anasema Bruno Jaffré.

Tofauti kuu: historia ya kisiasa

Rais wa zamani wa Burkina Faso Thomas Sankara

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa zamani wa Burkina Faso Thomas Sankara

Kwa Jaffré, tofauti kubwa kati ya IB na Sankara iko katika historia yao ya kisiasa.

"Sankara alikuwa mwanajeshi mwenye uelewa wa kina wa siasa na alikuwa na misingi ya kifalsafa, aliyejihusisha kwa muda mrefu na wanamapinduzi wa Kikomunisti nchini. Alipanga na kuendesha mapinduzi kwa kushirikiana nao."

Kwa upande mwingine, Traoré aliibuka bila historia yoyote ya kisiasa au mafunzo ya kiitikadi.

"Kumuita mtu huyu kuwa mpenda mapinduzi wakati hana misingi ya kiitikadi ni jambo linalotia shaka," anasema Jaffre

Uendeshaji wa madaraka: Njia tofauti mbili

Sankara alianzisha Baraza la Kitaifa la Mapinduzi (CNR) ambalo lilihusisha wanajeshi na raia, na ambalo lilihusika katika kufanya maamuzi makubwa ya kitaifa.

Kamati za Ulinzi wa Mapinduzi (CDR) nazo zilitoa nafasi kwa mijadala na ushirikishwaji wa wananchi.

Kwa sasa, chini ya utawala wa Traore ama ukipenda IB, hali ni tofauti.

"Hatujui ni nani hasa yuko ndani ya MPSR, nani anasaidia kuendesha nchi? Zaidi ya Traoré na ndugu zake wawili, hakuna uwazi," anaeleza Jaffré.

"Tuna mtu (IB) ambaye ni mgeni kabisa na hana mafunzo ya kisiasa. Na unapomsoma, unahisi kwamba hana mafunzo ya kisiasa, lakini anashauriwa na wataalamu wa mawasiliano na ana mwelekeo wa kuiga Thomas Sankara katika hotuba na mahojiano," anaeleza Bruno Jaffré.

Kwake yeye, "hufanyi mapinduzi wakati huna historia ya kiitikadi. Sankara aliegemea kwenye Umaksi hata kama mara nyingi alikiri kuwa yeye sio, lakini alikuwa mfuasi wa maksi. Mashirika yote yaliyozunguka CNR yote yalijitangaza kuwa wakomunisti wa Kimaksi."

gg

Chanzo cha picha, Getty Images

Mashirika mawili muhimu (CNR, CDR) ya mapinduzi ya Sankara, hayapo chini ya Traore

Pamoja na CNR na Kamati za Kulinda Mapinduzi (CDR), "ilikuwa watu waliokuwa madarakani kwa namna fulani," anaamini Bruno Jaffré, ambaye anabainisha kutokuwepo kwa aina hii ya chombo ambapo mjadala unaokinzana, lakini "unaodhibitiwa" unaweza kufanyika chini ya utawala wa Sankara.

Wakati wa Sankara, "tulikuwa na mapinduzi yaliyoongozwa na CNR, ambayo ilikuwa uongozi wa serikali kuu ambapo katibu mkuu wa CDR aliwakilishwa.

Kwa hiyo, ilitoa mwelekeo wa kisiasa, kiuchumi, kijamii, nk.

Tulikuwa na mikutano kadhaa ya kitaifa, ambapo CDRs walihusika kufanya maamuzi juu ya bajeti, juu ya makato ya mishahara ya watumishi wa umma.

CDR walikuwa na jukumu la kweli la kazi katika wizara,"". anasema Jaffré

Zaidi ya hayo, wafuasi wa utawala wa sasa ni vikundi vya kiraia vilivyoibuka baada ya mapinduzi, visivyo na uwezo wa kuhoji au kukosoa sera za serikali.

Kuna pia kundi la vijana maarufu kama "Waayiyans" wanaoshabikia IB mitaani bila kuwa na msingi wa kisiasa zaidi ya kauli kali za kupinga Ufaransa au viongozi wa mataifa jirani kama Alassane Ouattara.

Kwa miaka mitatu iliyopita, Traoré ameendeleza utawala unaozidi kuwa wa mkono wa chuma.

Waandishi wa habari, wanasiasa, na wanaharakati wa kiraia wamekuwa wakikamatwa, huku nafasi ya mjadala wa wazi ikizidi kufifia.

"Ni kweli, hata Sankara hakupenda kupingwa hadharani, lakini kuna ushahidi kuwa aliweza kubadilisha msimamo wake baada ya kushauriwa, kwa mfano katika sera ya 'mshahara wa maisha' na marekebisho ya elimu, ambalo lilihusisha kuchukua sehemu ya mshahara wa mtumishi wa serikali ili kumpa mke wake ambaye anahusika na chakula, marekebisho ya elimu na ukataji ambayo haikuondolewa, lakini haikutumika pia''." anakumbusha Jaffré.

Kwa upande wa Wendyam Hervé Lankoandé:

"Sankara aliongoza katika enzi ambayo mijadala ya kifalsafa na kisera ilikuwa sehemu ya uhalali wa mapinduzi. Uwazi wa mjadala huo ulikuwa pia ni chombo cha elimu ya kisiasa, ingawa uwanja wa siasa haukuwa huru kabisa kwa kuwa ulikuwa chini ya usimamizi wa CDR."

Leo hii, chini ya kivuli cha vita dhidi ya ugaidi, Burkina Faso ya IB inaonekana kuzidi kuingia kwenye mfumo wa utawala usio na mjadala wa wazi, huku matumaini ya kurejea kwa utawala wa kikatiba yakizidi kufifia nchini Burkina Faso.

Mada zinazohusiana:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid