Kwanini Traore anabadilisha dhana ya mapinduzi ya kijeshi Afrika?

Chanzo cha picha, TRAORE
- Author, Yusuph Mazimu
- Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Katika historia ya siasa za Afrika, mapinduzi ya kijeshi mara nyingi yamechukuliwa kama njia haramu, hatari, na isiyo na uhalali wa kisiasa. Kuingia madarakani kwa kutumia nguvu za kijeshi kumehusishwa na umwagaji damu, uharibifu wa mali, utekaji wa haki za binadamu, na kusababisha mateso kwa raia wa kawaida.
Lakini kuibuka kwa Kapteni Ibrahim Traore nchini Burkina Faso kunachochea mjadala mpya kuhusu uhalali, umuhimu na hatima ya mapinduzi ya kijeshi hasa pale yanapotokea kama njia ya kupinga ukandamizaji, ufisadi, na utawala wa mabavu unaojificha katika mwavuli wa "demokrasia."
Tofauti na wanasiasa waliokita mizizi kwenye mifumo ya kidemokrasia lakini wakatumbukia katika matumizi mabaya ya madaraka, baadhi ya wanajeshi kama Traore wameibuka kama 'viongozi wa mabadiliko' wanaojitambulisha kwa uzalendo, uthubutu, na kujali maslahi ya wananchi. Mjadala uliopo sasa Je, Kiongozi huyu kijana, Traore, anabadilisha dhana ya mapinduzi kwa ujumla?
Historia ya mapinduzi ya kijeshi barani Afrika
Mapinduzi ya kijeshi yamekuwa sehemu ya historia ya Afrika tangu mataifa mengi yalipopata uhuru. Moja ya mapinduzi maarufu na ya kiitikadi ni lile la mwaka 1983 lililoongozwa na Thomas Sankara nchini Burkina Faso, ambaye alijulikana kwa ajenda zake za kupinga ukoloni mamboleo na kupigania maendeleo ya ndani kwa kutumia rasilimali za kitaifa. Lakini si Burkina Faso pekee.
Nchini Ghana, Kanali Ignatius Acheampong aliongoza mapinduzi mwaka 1972; Nigeria imepitia mapinduzi kadhaa tangu miaka ya 1960, yakiwemo yale ya Yakubu Gowon (1966) na Sani Abacha (1993). Uganda ilishuhudia mapinduzi yaliyomweka madarakani Idi Amin mwaka 1971. Nchini Ethiopia, Derg ilipindua utawala wa kifalme mwaka 1974. Hadi hivi leo, Sudan, Guinea, Mali, na Niger zimetumbukia kwenye mapinduzi yanayoongozwa na jeshi.
Hii historia imejenga taswira hasi ya mapinduzi, yakionekana kama kichocheo cha udikteta, vurugu, na migogoro ya kisiasa. Hata hivyo, historia hii pia inaonyesha jinsi mapinduzi yalivyotumika kama njia ya kuondoa tawala kandamizi katika mazingira ambako demokrasia ilishindwa kuleta haki na maendeleo.
Athari za mapinduzi

Chanzo cha picha, Getty Images
Hakuna anayeweza kupuuza madhara ya mapinduzi ya kijeshi. Kwa kawaida huambatana na mapigano, vifo, mateso ya raia, uharibifu wa miundombinu, na uchumi kudorora. Viongozi wa mapinduzi mara nyingi hujenga utawala wa kiimla, wakifuta katiba, kuvunja bunge, na kudhibiti vyombo vya habari na vyama vya siasa.
Kwa mfano, Sudan ilikumbwa na vurugu kubwa baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2019 yaliyomuondoa Omar al-Bashir. Baadaye, mvutano baina ya jeshi na raia uliibua mapigano ya silaha mwaka 2023, yaliyosababisha maelfu ya vifo na mamilioni kukimbia makazi yao. Guinea ilipitia ghasia baada ya mapinduzi ya 2021, huku Mali ikipitia matatizo makubwa ya kiusalama na kiuchumi tangu mapinduzi ya 2020.
Zaidi ya hayo, mapinduzi huleta hofu ya kutoaminika kwa serikali, hali ambayo huathiri uwekezaji wa nje, misaada ya kimataifa, na ushirikiano wa kikanda. Taasisi kama AU na ECOWAS mara nyingi huwekea vikwazo mataifa yanayopinduliwa kijeshi, jambo linaloathiri maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kwanini Traore anaonekana kubadilisha dhana ya mapinduzi?

Chanzo cha picha, TRAORE
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ibrahim Traore alichukua madaraka mnamo Septemba 2022, akimng'oa Paul-Henri Damiba kwa kile alichokitaja kuwa "kutoweka kipaumbele kwa maslahi ya taifa na kupuuza vita dhidi ya ugaidi." Tangu wakati huo, ameibuka kama kiongozi anayependwa sana si tu na watu wa Burkina Faso, bali pia na Waafrika wengi waliokata tamaa na viongozi wa kidemokrasia wanaotumia uhuru kama kichaka cha kujineemesha.
Kwa muda mfupi, Traore ameanzisha sera za kiuchumi za kujitegemea, kuimarisha vita dhidi ya ugaidi kwa msaada wa jamii, na kuhamasisha uzalendo miongoni mwa vijana. Moja ya nukuu yake maarufu inayosambaa mitandaoni ni:
"Hatuwezi kuwa huru ikiwa tumevaa suti za wakoloni, kutumia lugha zao na hata kuendesha siasa kwa mifumo yao."
Katika hotuba yake ya Novemba 2023, alisema: "Afrika haiwezi kuwa huru mpaka waafrika waache kuwa na woga mbele ya mataifa ya Magharibi."
Anaonekana kama kiongozi anayepinga kwa dhati ukoloni mamboleo. Uamuzi wake wa kuvunja ushirikiano wa kijeshi na Ufaransa, kufunga baadhi ya vituo vya kijeshi vya kigeni, na kuanzisha ushirikiano mpya na nchi kama Mali na Niger kupitia muungano wa AES (Alliance des États du Sahel) umemwongezea umaarufu.
Alipoelekezewa tuhuma na AFRICOM wiki iliyopita za kutumia mamlaka vibaya, badala ya lawama, Afrika nzima ililipuka kwa kumpa uungwaji mkono wa kipekee. Maandamano makubwa yalifanyika Ouagadougou, pamoja na miji ya nje kama Accra (Ghana), Brussels (Ubelgiji), New York (Marekani), Nairobi (Kenya), na Bamako (Mali).
Mitandaoni, kiongozi wa AFRICOM, Jenerali Michael Langley, alikumbwa na wimbi la ukosoaji mkubwa huku hashtag kama #HandsOffTraore na #AfricaForAfricans zikisambaa kwa kasi.
Wachambuzi wa siasa kama Dr. Kemi Adeoye (Chuo Kikuu cha Cape Town) wanasema: "Traore anaonekana kama jibu la kisasa kwa Lumumba na Sankara. Kizazi kipya kimeona kiongozi anayesema ukweli hadharani na hadhaniwi,". Alikuwa akizungumza na kupitia kipindi cha BBC Focus on Africa, Machi 2024.
Hatari Iliyo Mbele

Chanzo cha picha, MD
Pamoja na sifa na matumaini makubwa yanayomzunguka Traore, wachambuzi wanaonya kuwa huenda mafanikio yake yakatumika kama kigezo cha kuhalalisha mapinduzi zaidi barani Afrika. Kuna hofu kwamba jeshi katika mataifa yenye migogoro ya ndani linaweza kutumia mfano wake kuingilia siasa kwa tamaa ya madaraka.
Tayari, viongozi wa kijeshi kama Assimi Goïta (Mali) na Abdourahamane Tchiani (Niger) wamechukua madaraka kupitia mapinduzi na baadaye kuanza kuonyesha nia ya kugombea katika uchaguzi wa kiraia. Wachambuzi kama Prof. Mahamane Sissoko wa Chuo Kikuu cha Dakar wanasema: "Mapinduzi yanapoanza kuonekana ya kuvutia, yanahamasisha wengine kuiga kwa sababu mbaya , si kwa ajili ya watu bali kwa maslahi ya binafsi."
Ikiwa mfano wa Traore hautaambatana na ujenzi wa taasisi thabiti, hofu ni kuwa kutakuwa na wimbi la mapinduzi yasiyokuwa na ajenda ya kitaifa, bali tamaa ya madaraka, jambo linaloweza kurejesha Afrika katika duru ya migogoro na machafuko.















