Uchunguzi wa siri wafichua 'wanawake' wanaojihusisha na biashara ya ngono ya watoto Kenya

Uchunguzi wa BBC Africa Eye umefichua jinsi wanawake wanaojulikana kama "madam" wamewahusisha watoto wa umri wa miaka 13 katika ukahaba nchini Kenya.
Katika mji wa Mai Mahiu, katika Bonde la Ufa la Kenya, malori huzunguka barabarani mchana na usiku yakisafirisha bidhaa na watu nchini Uganda, Rwanda, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Kituo kikuu cha usafiri, kilomita 50 tu (maili 31) mashariki mwa mji mkuu, Nairobi, kinajulikana kwa ukahaba, lakini pia ni maarufu kwa unyanyasaji wa kijinsia wa watoto.
Wachunguzi wawili wa siri, wakijifanya wafanyabiashara wa ngono walitaka kujifunza jinsi ya kuwa washirika wa biashara hiyo ambapo walitumia miezi kadhaa mapema mwaka huu kujipenyeza katika biashara ya ngono katika mji huo.
Filamu yao ya siri inafichua wanawake wawili tofauti ambao wanasema wanajua kuwa ni kinyume cha sheria na kisha kuwatambulisha wachunguzi hao kwa wasichana wenye umri mdogo katika tasnia ya ngono.
BBC ilitoa ushahidi wake wote kwa polisi wa Kenya mwezi Machi. BBC inaamini kuwa wanawake hao wameondoka katika eneo hilo. Polisi wanasema wanawake na wasichana wadogo tuliowarekodi hawakuweza kupatikana. Hadi leo hakuna mtu aliyekamatwa.
Watu kupatikana na hatia ni ngumu nchini. Kwa mashitaka yenye mafanikio, polisi wanahitaji ushahidi kutoka kwa watoto. Mara nyingi watoto walio katika mazingira magumu wanaogopa sana kutoa ushahidi.
Picha za BBC zilizorekodiwa barabarani gizani zilionyesha mwanamke mmoja anayejiita Nyambura akicheka huku akisema: "Wao bado ni watoto, hivyo ni rahisi kuwadanganya kwa kuwapa peremende tu."
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Ukahaba ni biashara kuu katika eneo la Mai Mahiu; ukichochewa na madereva wa malori. Na hivyo ndivyo tunavyonufaika. Limekuwa jambo la kawaida katika Maai Mahiu," alielezea, akiongeza kuwa alikuwa na msichana mmoja mwenye umri wa miaka 13, ambaye tayari alikuwa "akifanya kazi" kwa miezi sita.
"Ni hatari kubwa unapojihusisha na watoto wadogo. Huwezi kuwapeleka mjini hadharani. Ninawatorosha tu usiku kwa usiri mkubwa," Nyambura alisema.
Kitendo cha ukahaba na mtu mzima aliyekubali hakijaharamishwa waziwazi chini ya sheria za kitaifa za Kenya lakini kimepigwa marufuku na sheria ndogo za manispaa. Hakijapigwa marufuku katika eneo la Maai Mahiu, ambalo ni sehemu ya kaunti ya Nakuru.
Chini ya kanuni ya adhabu ni kinyume cha sheria kuishi kutokana na mapato ya ukahaba, kama mfanyabiashara wa ngono au mtu mwingine anayewezesha au kufaidika kutokana na ukahaba.
Usafirishaji au uuzaji wa watoto walio na umri wa chini ya miaka 18 husababisha kifungo cha kuanzia miaka 10 hadi maisha.
Alipoulizwa iwapo wateja hao wanavaa mipira ya kondomu, Nyambura alisema kwa kawaida anahakikisha wanapata ulinzi lakini yule asiye wa kawaida havai.
"Baadhi ya watoto wanataka kulipwa zaidi [hivyo hawatumii]. Wengine wanalazimishwa [kutotumia] mipra ya kondomu," alisema.

Hakuna takwimu za hivi majuzi kuhusu idadi ya watoto wanaolazimishwa kufanya kazi kazi ya ngono nchini Kenya.
Mnamo mwaka wa 2012, Ripoti ya Nchi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuhusu Matendo ya Haki za Kibinadamu nchini Kenya ilitaja takriban watoto 30,000, ikiwa idadi inayotokana na serikali ya Kenya na sasa shirika lisilokuwa la kiserikali (NGO), Tokomeza Ukahaba wa Watoto nchini Kenya.
Tafiti zingine zimezingatia maeneo maalum, haswa kando ya pwani ya nchi - inayojulikana kwa hoteli zake za kitalii .. Ripoti ya 2022 ya shirika lisilo la kiserikali la Global Fund to End Modern Slavery ilipata takriban watoto 2,500 waliolazimishwa kufanya biashara ya ngono katika kaunti za Kilifi na Kwale.
Mpelelezi wa pili wa siri aliaminiwa na mwanamke aliyejiita Cheptoo na alikuwa na mikutano mingi naye.
Alisema kuuza wasichana wadogo kulimaanisha kwamba angeweza "kupata riziki na kustarehe".
"Mnafanya biashara ya aina hii kwa usiri mkubwa kwa sababu ni kinyume cha sheria," alisema.
"Iwapo mtu yeyote atasema anataka msichana mdogo, ninaomba anilipe. Pia tunao wahudumu wetu ambao huwa wanarudi kwa ajili yao."
Katika mkutano mwingine, aliongoza mpelelezi wa siri hadi kwenye nyumba ambayo wasichana watatu wachanga walikuwa wamejikunyata kwenye sofa, mwingine kwenye kiti cha mgongo mgumu.
Kisha Nyambura akatoka ndani ya chumba kile na kumpa mpelelezi fursa ya kuzungumza na wasichana hao peke yake.
Walielezea kudhalilishwa mara kwa mara kingono, kila siku.
"Wakati mwingine unafanya mapenzi na watu wengi. Wateja wanakulazimisha kufanya mambo yasiyofikirika," alisema mmoja wa wasichana hao.
Sekta ya ngono nchini Kenya ni ulimwengu mgumu na wenye matatizo ambapo wanaume na wanawake wanahusika katika kuwezesha ukahaba wa watoto.
Haijulikani ni watoto wangapi wanalazimishwa kufanya biashara ya ngono huko Maai Mahiu, lakini katika mji huu mdogo wa watu karibu 50,000 ni rahisi kuwapata.
Mfanyabiashara wa ngono wa zamani, anayejulikana kama "Baby Girl", sasa anatoa hifadhi katika Maai Mahiu kwa wasichana ambao wametoroka unyanyasaji wa kingono.
Mzee huyo mwenye umri wa miaka 61 alifanya kazi katika tasnia ya ngono kwa miaka 40 - kwanza alijikuta mitaani katika miaka yake ya ishirini. Alikuwa mjamzito na alikuwa na watoto wake watatu wadogo pamoja naye baada ya kumkimbia mumewe kwa sababu ya unyanyasaji wa nyumbani.
Katika meza yake ya jikoni ya mbao katika chumba chenye kung'aa mbele ya nyumba yake, alitambulisha BBC kwa wasichana wanne ambao wote walilazimishwa kufanya ngono na 'madam' huko Maai Mahiu walipokuwa watoto.
Kila msichana alitoa hadithi sawa za familia zilizovunjika au unyanyasaji nyumbani - walikuja Maai Mahiu baada ya kutoroka makwao, lakini walikumbwa na dhulma nyengine.
Michelle alielezea jinsi, akiwa na umri wa miaka 12, alipoteza wazazi wake kwa VVU kabla ya kufukuzwa mitaani ambako alikutana na mwanamume ambaye alimpa mahali pa kuishi na kuanza kumnyanyasa kingono.
"Nililazimika kumlipa kwa namna fulani kwa kunisomesha. Nilifikia kikomo, lakini sikuwa na mtu," alisema.
Miaka miwili baadaye, alikutana na mwanamke ambaye aligeuka kuwa 'madam' katika eneo la Maai Mahiu na kumlazimisha kushiriki ngono.
Lilian, ambaye sasa ana umri wa miaka 19, pia alipoteza wazazi wake akiwa na umri mdogo sana. Aliachwa na mjomba ambaye alimpiga picha akioga na kuuza picha hizo kwa marafiki zake. Hali hiyo iligeuka na kuwa ubakaji.
"Hiyo ilikuwa siku yangu mbaya zaidi. Nilikuwa na umri wa miaka 12 wakati huo."
Alipotoroka, alibakwa tena na dereva wa lori aliyempeleka Maai Mahiu. Ilikuwa katika sehemu hiyo , kama alivyosema Michelle, ambapo alikutana na mwanamke ambaye alimlazimisha kushiriki kazi ya ngono.
Maisha mafupi ya wasichana hawa yamechochewa na ukatili, kutelekezwa na unyanyasaji.
Sasa, wakiwa wamehifadhiwa na Baby Girl, wanajifunza ujuzi mpya - wawili katika studio ya kupiga picha na wawili katika saluni.
Pia wanasaidia Baby Girl na kazi yake ya kusaidia jamii.
Kaunti ya Nakuru ina mojawapo ya viwango vya juu zaidi vya maambukizi ya VVU nchini Kenya, na Baby Girl, akiungwa mkono na shirika la misaada la Marekani USAID, yuko kwenye dhamira ya kuelimisha watu kuhusu hatari ya kushiriki ngono bila kinga.
Ana ofisi katika Kituo cha Afya cha Jamii cha Karagita, karibu na Ziwa Naivasha, ambako anafanya kazi ya kutoa kondomu na ushauri.
Hata hivyo, kufuatia uamuzi wa Rais wa Marekani Donald Trump kuondoa ufadhili wa USAID, programu zake za kuwafikia watu zinakaribia kukoma.

"Kuanzia Septemba hatutakuwa na ajira," aliiambia BBC World Service, akiongeza jinsi alivyokuwa na wasiwasi kuhusu wasichana wanaomtegemea.
"Unaona jinsi watoto hawa walivyo katika mazingira magumu. Wangewezaje kuishi peke yao? Bado wanapona."
Serikali ya Marekani haikujibu maoni katika uchunguzi huu kuhusu uwezekano wa athari za kupunguzwa kwa ufadhili wake. USAID ilifungwa rasmi mwezi uliopita.
Kwa sasa, Lilian analenga kujifunza upigaji picha na kupona kutokana na unyanyasaji.
"Siogopi tena, kwa sababu Baby Girl yuko kwa ajili yangu," alisema. "Anatusaidia kusahau yaliotukumba awali."
Imetafsiriwa na Seif Abdalla













