Tetesi za soka Ulaya Jumatatu: Liverpool kurudi na dau jipya kwa Isak wiki hii

Muda wa kusoma: Dakika 2

Newcastle wanajiandaa kupokea ofa nyingine kutoka Liverpool kwa mshambuliaji wao wa Sweden, Alexander Isak, mwenye umri wa miaka 25, baada ya mchezo wa leo wa Ligi Kuu kati ya timu hizo. (The I paper)

Winga wa Manchester City, Savinho, bado ndiye chaguo namba moja la Tottenham, ambapo kocha Thomas Frank anataka kumsajili nyota huyo wa Brazil mwenye umri wa miaka 21 baada ya Spurs kumkosa Eberechi Eze, 27, aliyehamia Arsenal (Independent).

Tottenham wameweka wazi kwa Manchester City kuwa wako tayari kulipa pauni milioni 60.7 kumpata Savinho, ambaye naye anatamani kujiunga na klabu hiyo ya London (Talksport).

Katika juhudi za kufanya usajili mzuri, Tottenham pia wamewasilisha ofa iliyoboreshwa ya pauni milioni 43 kwa ajili ya kiungo wa Como na Argentina, Nico Paz mwenye umri wa miaka 20, lakini klabu hiyo ya Italia inashikilia msimamo wa kutaka dau la karibu pauni milioni 60 (Sky Sports Italia).

Manchester City, Arsenal na Liverpool zote zinaonyesha nia ya kumsajili winga wa Real Madrid na Brazil, Rodrygo, mwenye umri wa miaka 24, lakini hadi sasa klabu hiyo ya Uhispania haijapokea ofa yoyote rasmi kutoka kwa timu hizo (Marca).

Kiungo mshambuliaji wa Brazil wa West Ham, Lucas Paqueta, mwenye umri wa miaka 27, ananyatiwa na vilabu vya Tottenham pamoja na Aston Villa (Daily Mail).

Monaco wako tayari kukubali ofa ya karibu pauni milioni 47.5 kwa ajili ya kiungo mshambuliaji wa Ufaransa, Maghnes Akliouche, mwenye umri wa miaka 23, ambaye pia yupo kwenye rada za Tottenham.

Kipa wa Paris Saint-Germain, Gianluigi Donnarumma, amekubaliana masharti binafsi na Manchester City, huku klabu hizo mbili zikiwa kwenye mazungumzo ya kukamilisha dili litakalompeleka kipa huyo wa Italia mwenye umri wa miaka 26 kujiunga na kikosi cha Pep Guardiola (Fabrizio Romano).

Kipa wa Ubelgiji, Senne Lammens, mwenye umri wa miaka 23, alikosa mechi ya Royal Antwerp Jumapili kutokana na mpango wa uhamisho wake wa pauni milioni 17 kujiunga na Manchester United (Guardian).

Kocha wa West Ham, Graham Potter, kwa sasa yuko salama dhidi ya kufukuzwa, lakini kocha huyo Mwingereza mwenye umri wa miaka 50 anatakiwa kuboresha matokeo haraka iwapo anataka kubaki kwenye nafasi yake huko London (Mirror).

Chelsea wataendelea na mpango wa kuwasajili winga wa Manchester United na Argentina, Alejandro Garnacho mwenye umri wa miaka 21, pamoja na kiungo wa RB Leipzig, Xavi Simons wa Uholanzi mwenye umri wa miaka 22, endapo watafanikiwa kuwauza baadhi ya wachezaji wao wasiokuwa na nafasi (Sky Sports).

Leeds wapo kwenye mazungumzo ya mkataba wa kumruhusu winga wa Ubelgiji, Largie Ramazani mwenye umri wa miaka 24, kujiunga na Valencia kwa mkopo (Athletic).

Arsenal wamekubaliana kumsajili kiungo chipukizi wa Ireland, Victor Ozhianvuna mwenye umri wa miaka 16, kutoka Shamrock Rovers (Daily Mail).