Mazishi ya shinzo Abe: Wajapan watoa heshima zao za mwisho

Chanzo cha picha, Reuters
Umati mkubwa wa watu umekusanyika katika mitaa ya Tokyo kutoa heshima zao za mwisho kwa aliyekuwa waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe, ambaye aliuawa wiki iliyopita.
Kiongozi huyo aliyekuwa na umri wa miaka 67 alipigwa risasi na kuuawa siku ya Ijumaa alipokuwa akizungumza katika hafla ya kampeni katika mji wa kusini wa Nara.
Siku ya Jumanne, gari lililobeba mwili wa Abe lilizunguka mji mkuu na kupita maeneo ya kihistoria hadi eneo la mazishi ambapo alichomwa.
Mazishi ya faragha yalikuwa yamefanyika mapema katika hekalu la Zojoji.
Kote mjini Tokyo, Bendera zilipepea nusu mlingoti na nje ya hekalu, msururu mrefu wa waombolezaji ulishuhudiwa, baadhi ya watu wakiwa wamebeba shada la maua.
'Abe-San, asante sana'
Mazishi ya Shinzo Abe yalipaswa kuwa ya faragha kwa wote isipokuwa familia na marafiki. Lakini umma wa Japani ulikuwa umeamua vinginevyo.
Kuanzia mapema Jumanne asubuhi, walianza kujipanga nje ya hekalu kubwa la Zojoji katikati mwa Tokyo ili kuweka maua kwenye meza ndogo iliyowekwa upande mmoja wa jumba kuu.
Utabiri wa hali ya hewa ulikuwa mvua kubwa ya ngurumo, lakini ibada ya mazishi ilipoanza ndani umati wa watu mitaani nje uliongezeka tu.
Kufikia 14:30 (06:30 GMT) maelfu ya watu walijitokeza na kupanga foleni barabarani kutoka Zojoji hadi jengo la Bunge la Nagatacho.

Chanzo cha picha, Reuters
Nje ya ofisi ya waziri mkuu, gari lililobeba mwili wake lilipokaribia, kimya kilitanda kwenye umati wa watu na ulichosikia ni helikopta zilizokuwa zikizunguka juu.
Waombolezaji waliinama kwa Bi Abe, aliyekaa mbele ya gari la kubebea maiti, huku akiwa ameshikilia kibao kilichoandikwa jina la mumewe. Watu walianza kulia kwa sauti huku wengine wakisema, "Abe-San, asante sana."
Sekunde chache baadaye gari hilo kupita, mwanamke mmoja mwenye umri wa makamo katika umati alifikicha macho yake kwa leso na kusema: "Hatutakuwa na mwanasiasa mwingine kama yeye"
Shinzo Abe ni nani?
Abe bila shaka alikuwa mtu aliyeleta mgawanyiko na mwenye utata. Maoni yake juu ya historia ya Vita vya vya pili vya Dunia mara nyingi yalikuwa na ukakasi.
Lakini kwa umati wa Wajapan waliojitokeza kumuaga, "Abe-San" alikuwa waziri mkuu bora zaidi waliyemjua.
Abe alikuwa waziri mkuu wa Japan alihudumu muda mrefu zaidi baada ya vita na mmoja wa wanasiasa wake mashuhuri.
Na kifo chake kimeleta mshtuko katika taifa hilo ambalo matukio ya ghasia za bunduki ni nadra sana.
Polisi walisema mtu huyo mwenye silaha alimlenga Abe kutokana na malalamiko aliyokuwa nayo na kundi la kidini ambalo aliamini kuwa Abe alikuwa sehemu yake.
Lakini bado wanachunguza nia ya mshambuliaji huyo ilikuwa na nia gani na ikiwa alitenda hivyo peke yake.














