Daktari wa Syria: 'Mara tu aliponitazama, nilianza kulia'

Chanzo cha picha, SYRIAN AMERICAN MEDICAL SOCIETY
"Muonekano wa macho ya mtoto huyu ulinigusa sana," anasema Dkt Ahmed al-Masri. "Sijui kwanini lakini aliponitazama tu, nilianza kulia."
Ilikuwa zaidi ya saa 30 baada ya tetemeko kubwa la ardhi kukumba Uturuki Jumatatu wiki hii na alikuwa amedhoofika.
Yeye na daktari mwenzanke mmoja walikuwa wakiwatibu majeruhi wengi waliokuwa wakiletwa katika hospitali yao huko Afrin, mji unaoshikiliwa na upinzani kaskazini-magharibi mwa Syria.
Mara, Mohammed mwenye umri wa miaka saba aliletwa, baada ya kutolewa chini ya vifusi vya nyumba yao iliyoporomoka.
Waokoaji walimkuta akiwa amelala kando ya mwili wa baba yake ambaye alikuwa amepondwa hadi kufa pamoja na mama yake na ndugu zake.
"Jinsi yule mvulana alivyokuwa akitutazama, nilihisi kama anatuamini, alijua kuwa sasa yuko kwenye mikono salama," Dkt Masri alimwambia mwandishi wa BBC kupitia simu ya Zoom.
"Lakini pia nilihisi ana nguvu nyingi, kana kwamba alikuwa amevumilia maumivu ya majeraha yake. Ni nini kinamchofanya mtoto wa miaka saba kuwa na nguvu na uvumilivu kiasi hiki?"
Dkt Masri ni daktari wa upasuaji katika Hospitali ya Al-Shifa, ambayo inaungwa mkono na shirika la hisani la Jumuiya ya Madaktari ya Marekani nchini Syria (SAMS). Anasema ilipokea zaidi ya wagonjwa 200 mara baada ya janga hilo.

Chanzo cha picha, SYRIAN AMERICAN MEDICAL SOCIETY
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mtoto mwingine aliyeletwa na waokoaji baada ya kunusurika atetemeko hilo la ardhi alikuwa na uri wa miezi 18.
Dkt Masri alimchunguza na kubaini kuwa yuko sawa. Lakini alitambua kwamba wazazi wa mvulana huyo hawakuwa pamoja naye.
“Ghafla nilimuona baba yake akimkimbilia na kumshika huku akilia na kulia,” anasema.
"Baba aliniambia mtoto huyu ndiye pekee aliyenusurika katika familia yake. Wengine wa familia walikuwa wamelazwa kwenye baraza, wakiwa wamekufa."
Dkt Masri anasema wafanyakazi katika hospitali hiyo walishangazwa na ukubwa wa janga hilo, huku "makundi" ya wagonjwa wakifika wote mara moja.
"Sijawahi kufikiria kuwa tetemeko la ardhi linaweza kusababisha uharibifu mkubwa namna hii, linaweza kusababisha idadi hii ya wagonjwa."
Cha kusikitisha ni kwamba amezoea kufanya kazi katika mazingira magumu.
Mwaka wa 2013, alikuwa akifanya kazi katika hospitali moja wakati makombora yenye sumu yaliporushwa katika vitongoji kadhaa vilivyokuwa vikishikiliwa na upinzani viungani mwa mji mkuu, Damascus. Mamia ya watu waliuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa.
"Wakati huo, tulifunzwa na kutayarishwa kufanya kazi hali kama hiyo ikitokea," Dkt Masri anasema. "Tuliweza kujipanga haraka. Lakini katika tukio hili hatukujitayarisha. Hali hii ilikuwa mbaya zaidi."

Chanzo cha picha, AHMED AL - MASRI
Kufuatia tetemeko la ardhi la Jumatatu, yeye na wenzake huko Afrin walishughulikia wagonjwa ambao walionekana kujeruhiwa kidogo hapo awali.
"Yalikuwa majeraha ambayo unadhani sio makubwa, lakini mtu anahitaji kukatwa kiungo," anasema. "Hatuna uwezo katika hospitali zetu kushughulikia maafa ya aina hii."
"Jambo baya zaidi ni kuwa daktari katika mazingira haya. Unaposhindwa kuokoa mgonjwa au kumsaidia kupunguza maumivu - hilo ndilo jambo baya zaidi unaweza kuhisi."
Alipokuwa akiwatibu wagonjwa, Dkt Masri pia alilazimika kufanya kazi bila kutojua ikiwa familia yake mwenyewe ilikuwa salama kwa sababu huduma za umeme na mtandao ilikuwa hafifu.
Wazazi wake na kaka zake wanaishi umbali wa mita mia chache kutoka hospitali, lakini mke wake na watoto wanaishi mpakani katika mji wa kusini mwa Uturuki wa Gaziantep, ambao ulikuwa karibu na kitovu na pia uliathirika vibaya.
"Tunamhudumia mgonjwa kwa umakini - jicho moja likikagua majeraha, lingine likiangalia kama ni jamaa yako au la."

Chanzo cha picha, SYRIAN AMERICAN MEDICAL SOCIETY
Moyo wake ulutulia pale kaka yake alipoenda hospitali kumhakikishia Dk Masri kuwa familia yake yote iko salama. Pia alifanikiwa kupata mapumziko mafupi katika hospitali hiyo.
"Nilipolala wakati huo, nilianguka tu," anasema. "Kuna wakati nilihitaji mtu wa kunishikilia ili niendelee kufanya kazi."
Kisha Dkt Masri aliweza kuondoka kazini na kupata kifungua kinywa na familia yake. Anatumai hatimaye atafanikiwa kusafiri kumwona mke wake na watoto huko Gaziantep.
Anasema pia alikwenda kumtazama Mohammed siku iliyofuata na kumuuliza mtoto huyo wa miaka saba kama anamkumbuka.
"Ndiyo, wewe ndiye daktari uliyeokoa maisha yangu," Mohammed alijibu.














