‘Je, ni kosa langu mpaka nitumiwe picha za utupu na ujumbe usiofaa?’

Emily

Mtangazaji nyota wa televisheni ya Uingereza Emily Atack anatumiwa mamia ya picha chafu na ujumbe usiokuwa na staha kila siku.

Anauliza nini kinawapa motisha wanaume wanaofanya hivi na nini kifanyike kuwakomesha?

"Kila asubuhi ninapoamka naona picha ya mtu ambaye sijaomba kumuona."

 Muigizaji, mtangazaji na mchekeshaji Emily Atack, mwenye umri wa miaka 33, anaangaziwa na mamia ya mara kwa siku mtandaoni.

"Ni ukosefu wa heshima kabisa," anasema. "Ni jambo baya kwa kweli linaloendelea kufanyika.

Emily - ambaye alitengeneza makala ya BBC kuhusu suala hilo – amekuwa akipokea ujumbe mchafu moja kwa moja kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii kwa miaka.

Lakini wingi wa ujumbe wa namna hiyo uliongezeka zaidi wakati wa marufuku ya kutoka nje, walizidi kutuma ujumbe nyingi za maudhui ya kingono.

Emily alikuwa na umri wa miaka 17 alipoigiza kama Charlotte Hinchcliffe katika vichekesho maarufu vya Channel 4, The In betweeners.

"Alikuwa msichana maarufu shuleni," anasema Emily. "Suala ni kwamba ndio, ni mhusika wa kubuni, lakini ni wazi watu wanakuhusisha na uhusika unaocheza."

mm
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hisia za lawama

Nikiwa na umri mdogo sana, Emily anasema alianza kusumbuliwa na baadhi ya wanaume. Ili kukabiliana na hali hiyo, anasema aliambiwa na familia yake kuwa bora kuacha kufanya baadhi ya mambo, kama vile kutojipodoa au kutovaa sketi shuleni.

"Ni suala gumu sana, njia pekee ambayo wale wanaokupenda wanaweza kuidhibiti ni kukubadilisha," anasema.

"Hayo yote yanaingia mahali fulani, kwa hiyo nilianza kujilaumu katika maisha yangu yote kwa sababu hiyo."

Emily alibeba hisia hii ya lawama katika maisha yake. 

"Nina wasiwasi juu ya haya yote kwa sababu niliweka picha za bikini kwenye Instagram, nazungumza kuhusu ngono katika maonesho yangu na mimi ni mkali na sipendi utani," anasema. 

 "Kutakuwa na watu wakisema, 'Lakini ukiuliza maoni haya mabaya ya watu, unatarajia nini?' 

"Je, Hili ni kosa langu? Je! kuna jambo ninaloweka huko nje?'

Emily amekuwa akitumia ucheshi kama njia ya utetezi ili kufanya ujumbe kuwa mwepesi, lakini anasema sio jambo la kuchekesha tena.

"Ikiwa tutaangalia undani wake, wasichana wadogo wako kwenye Instagram wakipokea ujumbe kama huu," anasema.

mm

"Ni nini kingetokea ikiwa huyu angekuwa binti yako au mpwa wako?

 Ni mjadala mzito zaidi kuwa nao mara tu kicheko kitakapokoma."

Utafiti wa mwaka 2020 uligundua kuwa 76% ya wasichana wenye umri wa miaka 12-18 walikuwa wametumiwa picha za uchi za wavulana au wanaume ambazo hazijaombwa.

 Emily alipozungumza na baadhi ya wasichana wa shule ya sekondari, alishtuka kwamba wote walisema walikuwa wanapokea ujumbe mchafu wa kingono mtandaoni.

“Kilichonishtua zaidi ni kwamba nilidhani wasichana wangesema kuwa ni wavulana shuleni ambao hawakuwa na udhibiti na simu zao, lakini ni wanaume wakubwa mtandaoni ambao wanawaendea wasichana hawa,” anasema.

 Emily aliweka chapisho kwenye mtandao wake wa kijamii akiwauliza wanaume wanaomtumia ujumbe mchafu waeleze kwa nini wanafanya hivyo.

"Niliangalia barua pepe zangu - sikupokea chochote," anasema. "Wanaume hawa wanatumia maisha yao kunishambulia kwa matusi na kusema mambo ya kutisha zaidi na huwa ninajibu na kusema, 'Sawa nataka kusikia kutoka kwako, tuzungumze'.

"Nilichokuwa nacho ni wanawake wengi waliofikia kusema yale ambayo wangelazimika kushughulika nayo." 

Emily anasema hajawahi kujadili unyanyasaji huu mtandaoni na wazazi wake, na mama yake, mcheshi Kate Robbins, anakasirika sana anapoonyeshwa ujumbe unaotumwa unavyokuwa.

Anasema ana wasiwasi kuhusu athari za kisaikolojia inayompata binti yake na usalama wake wa kimwili.

Ingawa jumbe hizo zinatoka kwa wanaume wengi tofauti, baba yake Emily, Keith, anaona jinsi anavyohisiwa kuwa zinatoka kwa mtu mmoja.

Ili kujaribu kuelewa zaidi kuhusu sifa za watu hawa, Emily aliwatumia ujumbe moja kwa moja wanaume wawili ambao mara kwa mara wanamtumia maudhui machafu kuwauliza kwa nini wanafanya hivyo. Mmoja alimfungia asitume ujumbe kwake mara tualiposoma ujumbe wa Emily, huku mwingine akijibu akimlaumu - akisema alikuwa akijaribu kuwa rafiki yake kutokana na umaarufu wake.

Emily alizungumza na Jamie Klingler, mwanzilishi mwenza wa Reclaim These Streets, ili kujaribu kuelewa mawazo ya wanaume hawa. Jamie alianza kupokea picha chafu, vitisho vya kubakwa na kuuawa mtandaoni baada ya kuandaa mkesha kufuatia mauaji ya Sarah Everard.

"Sio juu ya kile tunachovaa, sio juu ya kile tunachofanya," anasema. "Inahusu wao kutaka kukunyamazisha na kukudhibiti na wao kutaka kuwa na uwezo wa kukufanya ujisikie kuwa sehemu yao."

Utafiti wa Prof Jane Monckton-Smith unaangazia uzuiaji wa mauaji - vitendo vinavyosababisha kifo cha mtu mwingine. Anasema mifumo ya unyanyasaji dhidi ya wanawake inaongezeka kutoka kitu kinachoonekana kidogo hadi unyanyasaji mkubwa wa kijinsia.

Kwa sababu hii, anapendekeza kila mara uripoti unyanyasaji mtandaoni kwa polisi ili jina la mtu huyo liwekwe kwenye rekodi.

"Ubakaji si kosa la kuanzia, mauaji si kosa la kuanzia," Prof Monckton-Smith anamwambia Emily.

"Kutakuwa na ishara na tabia na mifumo kabla ya kufika huko, lakini ishara hizo nyingi zitatetewa na haki ingawa kutakuwa na lawama fulani kwa mwathirika."

mm

Kubadilisha tabia

Kufuatia mazungumzo yao, Emily anaripoti unyanyasaji wa mtandaoni kwa polisi na bila kutarajia anajikuta amekasirika sana anapoelezea unyanyasaji huo.

Afisa mmoja anasema wanaweza kuwafuatilia wanaume hao ikiwa watu wengine wameripoti unyanyasaji na wanaweza kuchukua hatua ikiwa tabia hiyo inahusisha kipengele cha uvamizi. 

Lakini baada ya maafisa hao kuondoka, Emily anahisi mkanganyiko kuhusu kama anataka mtu yeyote akamatwe.

"Ninawahitaji kukiri tu kwamba wamefanya makosa," anasema.

Mnamo 2021, Emily alitoa hotuba Bungeni akishiriki uzoefu wake wa unyanyasaji na Mswada wa Usalama Mtandaoni unajumuisha kosa jipya la mtandaoni ambalo litachukua kifungo cha juu zaidi cha miaka miwili jela.

Mswada huo uliidhinishwa na wabunge wiki iliyopita.

Lakini Emily amefanya kampeni kwa hili, sasa anashangaa ikiwa kubadilisha sheria pekee ndilo jibu.

Mwanaharakati wa usalama mtandaoni Seyi Akiwowo anasema ingawa sheria inaweza kusaidia, elimu ina jukumu muhimu, pamoja na kubadilisha kanuni za jamii.

"Kwa kweli tunahitaji kuchukua hatua na kujua kiini cha haya yote?' Na kwa kweli ni kubadilisha tabia za wanaume. Ni kuwafanya kuelewa uhusiano mzuri ni nini. Inawafanya kuelewa maana ya kupewa kibali ni nini, "anasema.

Andrea Simon, mkurugenzi wa kikundi Tokomeza Unyanyasaji Dhidi ya Wanawake, anakubali kwamba jamii inapaswa kuondokana na kugawanya lawama kwa wanawake.

Emily anasema kukabiliana na unyanyasaji mtandaoni imekuwa moja ya mambo magumu zaidi ambayo amewahi kufanya - alipitia matibabu katika mchakato mzima kwani ilihusisha kupata msongo wa mawazo.

"Mambo ambayo nimepitia, ambayo nimeyarekebisha maisha yangu yote, kadiri ninavyozungumza juu yake, ndivyo ninavyogundua kwamba sikupaswa kuvumilia - wakati huo au leo," anasema. "Bado ninajifunza hilo, bado ninajishughulisha na nitakuwa hivyo kila wakati.

“Sitabadili ninachofanya kwa sababu huwa nanyanyaswa kila wakati, si tabia zetu zinazopaswa kubadilika, ni zao.

"Sipaswi kujilaumu."