Ilikuwaje serikali ya Kenya ikakosa mishahara ya wafanyakazi wake?
Na Abdalla Seif Dzungu
BBC News

Chanzo cha picha, Ikulu ya rais Kenya
Kwa mara ya kwanza tangu Kenya ijinyakulie Uhuru 1963 , serikali imeshindwa kuwalipa mishahara wafanyakazi wa umma na wabunge.
Kufikia sasa wafanyakazi wa umma hawajui ni lini watalipwa mishahara yao hali ambayo ilianza mwezi Disemba na imeendelea kuwepo hadi sasa.
Na sio hapo tu, serikali za kaunti zimeendelea kulalama huku zikishindwa kutoa huduma baada ya serikali kuu kushindwa kutuma fedha kwa takriban kipindi cha miezi minne iliyopita.
Kwa sasa ni walimu na maafisa wa jeshi waliopokea mishahara yao ya mwezi Machi.
Viashiria vyote vinaonesha kuwa tatizo hili linaweza kuendelea kwa miezi kadhaa. Waziri wa fedha Njuguna Ndung’u ameonya kuhusu nyakati ngumu zijazo, akisema, serikali iko katika "tatizo la kifedha."
Haya yanajiri huku watumishi wa umma wakipanga kugoma kuishinikiza serikali iwalipe, hatua ambayo inaweza kuweka huduma za serikali kwa umma katika hali tete.
Hivi karibuni maelfu ya wafanyakazi wa umma walienda likizo ya Pasaka bila mishahara ya Machi huku wafanyakazi wa serikali za kaunti wakidai malimbikizi ya hadi malipo ya miezi minne.
Hatua hii inajiri huku baadhi ya maafisa wakuu serikalini akiwemo makamu wa rais akinukuliwa kusema kwamba serikali haina fedha miezi sita baada ya kuchukua uongozi.
Hazina ya serikali inahitaji wastani wa Ksh. 50 bilioni kila mwezi kwa mishahara ya watumishi wa umma na nyingine Ksh. 8 bilioni kwa malipo ya pensheni.
Ripoti zinaarifu kwamba serikali inakabiliwa na uhaba wa fedha huku matumizi ya kupitia kiasi yakizidi kodi ya kiwango cha chini inayokusanywa na shirika la kutoza kodi nchini KRA.
Ruto: ‘Hatutakopa kulipa mishahara’
Siku ya Jumanne rais William Ruto alitia chumvi katika kidonda alipotangaza kwamba serikali yake haitakopa fedha ili kulipa mishahara ya wafanyakazi wa umma.
“Najua tulikuwa na suala la kuchelewesha mishahara. Ni mara ya kwanza tunacheleweshewa mishahara lakini pia ni mara ya kwanza kuwa na madeni makubwa kama haya. Ninataka kuhakikishia nchi kwamba hilo litaangaziwa, "rais alisema.
“Ninachoihakikishia nchi ni ahadi niliyoitoa kwamba hatuendi kukopa fedha kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikiwa ni pamoja na mishahara. Huo ndio msimamo wa serikali ya Kenya.”
Siku ya Jumatatu Mwenyekiti wa baraza la Washauri wa Kiuchumi wa Rais William Ruto David Ndii aliikosoa serikali ya Muungano wa Kenya Kwanza kwa matumizi mabaya, huku kukiwa na uhaba mkubwa wa fedha.

Chanzo cha picha, AFP
‘Matumizi yetu hayaendani na hali tulionayo’
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Akizungumza na chombo kimoja cha habari siku ya Jumatatu usiku, Ndii alisema kuwa hali ya sasa, ambayo mishahara ya watumishi wa umma imecheleweshwa, inatokana na mipango duni.
"Nakubaliana na baadhi ya shutuma ambazo zinaelezwa na wananchi, kwamba hatuonyeshi matumizi mazuri ya fedha yanayoendana na hali tuliyonayo ya uchumi."
Ndii alifananisha hali ya sasa ya kuyumba kisiasa na kiuchumi na "usimamizi mbaya wa kisiasa" ambao anadai ulifanyika wakati wa marehemu Rais Mwai Kibaki.
"Nilimtazama Mwai Kibaki akisimamia vibaya siasa kutoka 2003 hadi 2005, yote tuliyofanya kiuchumi yaliambulia patupu 2007. Tulichokuwa nacho ni ushupavu, na nadhani kwa sasa tuko katika hali ambayo si tofauti," Ndii alisema.
Kulingana na kiongozi wa wachache bungeni Opiyo Wandayi serikali inadaiwa na vitengo mbalimbali vya serikali Ksh 204 billioni.
"Utawala unadaiwa na mashirika ya serikali Ksh 204 bilioni huku kaunti zikidai Ksh92.5 bilioni ambazo ni malipo ya miezi ya Januari, Februari na Machi."
Matamshi ya kiongozi huyo yanajri siku chache tu baada ya serikali kubuni nyadhfa 50 za makatibu wa kudumu suala lililozua pingamizi miongoni mwa mashirika yasio ya kiserikali kutokaa na uhaba wa fedha unaokumba serikali.

Chanzo cha picha, AFP
Lakini ilikuwaje hadi Kenya ikafikia hali hiyo?
Na mchambuzi David Burare
Kulingana na mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Kenya David Burare, mikopo iliyochukuliwa chini ya serikali ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta imefikia wakati wa kulipwa hivyo basi serikali iliyopo haina budi ila kuilipa.
Bwana Burare anasema kwamba mikopo hiyo haikutumika vizuri kwa mfano katika miradi inayoweza kuleta fedha na kwamba kiwango kikubwa kiliibwa hatua iliyofanya baadhi ya mashirika ya serikali kama vile vyuo vikuu kufilisika huku baadhi ya kampni za binafsi pia zikifungwa kutokana na hali mbaya ya kiuchumi.
Vilevile ametaja ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali kama sababu kuu zilizolifanya taifa hili kukosa fedha kuwalipa wafanyakazi wake.
Anasema kwamba kushindwa kwa serikali kuyapa kipaumbele masuala muhimu na badala yake kuwaridhisha baadhi ya viongozi wake waliopoteza katika uchaguzi uliopita kumechangia pakubwa katika matumizi mabaya ya rasilimali.
Katika ukusanyaji wa kodi, bwana Burale anadai kwamba kumekuwa na hoja zinazokinzana kati ya serikali na mamlaka ya kukusanya kodi KRA.
Anasema kwamba huku serikali ikidai kwamba mamlaka hiyo ilishindwa kuafikia malengo yake ya ukusanyaji wa kodi , mamlaka hiyo badala yake imekana na kusema kwamba ilifanikiwa kukusanya fedha za kutosha .
Suali ni je fedha hizo zimekuwa zikitoweka kutoka chanzo chake ambacho ni mamlaka ya KRA, ama hupotea zinapowasili katika wizara au sababu zote mbili?
Akihitimisha ameitaka serikali kuangazia kile walichoahidi Wakenya kupitia kuuinua uchumi ili uweze kutimiza mahitaji ya kila mwananchi na kusita kunyooshea kidole cha lawama kwa serikali iliyopita akisema kwamba hatua hiyo haitawasaidia kwasababu Wakenya wamechoshwa na tabia hiyo na kwamba wanachohitaji ni huduma.















