ANC chaelekea kugawana madaraka baada ya kushindwa katika uchaguzi

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa anakabiliwa na shinikizo kubwa baada ya kukiongoza chama tawala cha African National Congress (ANC) kwa matokeo mabaya zaidi ya uchaguzi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 30, na kulazimisha kugawana madaraka.
Huku takriban kura zote zikiwa zimehesabiwa, ANC iko kwenye asilimia 40 - chini kutoka asilimia 58 katika uchaguzi uliopita.
Hii ni asilimia ya chini kuliko ile chama iliyokuwa ikihofia asilimia 45, wachambuzi wanasema.
Chama cha ANC kimekuwa na kura zaidi ya asilimia 50 tangu uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia nchini humo mwaka 1994, ambao ulimshuhudia Nelson Mandela kuwa rais.
Lakini uungwaji mkono kwa chama hicho umekuwa ukishuka kwa kiasi kikubwa kutokana na hasira juu ya viwango vya juu vya rushwa, ukosefu wa ajira na uhalifu.
Akitoa mfano wa mzozo wa gharama ya maisha na kukatwa mara kwa mara kwa umeme, mwanamke mmoja aliiambia BBC kuwa alimaliza mfululizo wa miaka 30 wa kupigia kura chama cha ANC kwa kupendelea chama cha mrengo wa kati cha Democratic Alliance (DA) wakati huu.
"Matokeo haya si mazuri. Nilitaka kiondoke serikalini. Tunahitaji kumpa mtu mwingine nafasi," aliambia BBC.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Sanusha Naidoo aliambia BBC kuwa ingawa kuna kura nyingi ambazo bado hazijahesabiwa, hakuna njia ambayo ANC inaweza kufikia asilimia 50 ya kura inayohitajika kuunda serikali peke yake. Alisema asilimia ya juu sana ambayo inaweza kutarajia kupata ni 45.
Hivyo ili kuendelea kuwepo madarakani, chama kitahitajika kuunda muungano na chama kimoja au zaidi.
Mwenyekiti wa ANC Gwede Mantashe alisema chama chake hakina uwezekano wa kuunda muungano na chama cha mrengo wa kati DA, ambacho kwa sasa kiko katika nafasi ya pili kwa asilimia 22.
Alisema itabidi kuwe na "uwianishaji wa sera" kati ya vyama kwenye makubaliano ya muungano.
Kwa ANC, sera zake za uwezeshaji watu weusi - zilizolenga kuwapa watu weusi ubia katika uchumi kufuatia kutengwa kwao wakati wa enzi ya ubaguzi wa rangi - "sio ya kujadiliwi".

Chanzo cha picha, EPA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Aliongeza kuwa mshirika yeyote wa muungano atalazimika kukubaliana na Mswada wa Bima ya Kitaifa ya Afya (NHI), ambao ulitiwa saini kuwa sheria mapema mwezi huu.
DA inapinga sera za Bima ya Kitaifa ya Afya na kuwawezesha watu weusi za chama cha ANC.
Uungwaji mkono wa DA unaonekana kuimarika katika uchaguzi huu, ambapo chama hicho kimepata kura za watu weupe ambao walikuwa wamekiunga mkono chama fulani katika uchaguzi uliopita, na baadhi ya watu weusi ambao waliona ni lazima wapewe nafasi katika serikali ya kitaifa.
Licha ya ANC kusita kuungana na DA, kiongozi wake John Steenhuisen hajaondoa uwezekano huo.
Bw Steenhuisen alisema iwapo muungano na ANC utaafikiwa kutakuwa na mambo machache yasiyoweza kubadilishwa.
“Kuheshimu utawala wa sheria na katiba, uchumi wa soko la kijamii unaochukulia sekta binafsi kama washirika katika ajenda ya ukuaji.
Bw Steenhuisen pia aliambia BBC kwamba atalazimika kushauriana na washirika wa muungano wa kabla ya uchaguzi kabla ya kuzingatia mazungumzo yoyote.
Lakini aliondoa chama cha EFF na MK, ambavyo vyote vinatetea kunyakua ardhi inayomilikiwa na wazungu na kutaifisha migodi, kama washirika wanaoweze kuwepo ndani ya muungano.
"Nadhani kukosekana kwa utulivu sio kwa manufaa ya nchi. Muungano wenye siasa kali za mrengo wa kushoto nchini Afrika Kusini za chama cha MK na EFF utazalisha sera zilezile zilizoiangamiza Zimbabwe, Venezuela," alisema.
Uwezekano mmoja ungekuwa muungano kati ya chama cha zamani cha MK na ANC katika KwaZulu-Natal na kitaifa - lakini kutokana na uhusiano uliovunjika kati ya pande hizo mbili, hilo linaonekana kuwa lisilowezekana.
Wakati Bw Zuma amesimamishwa uanachama wa ANC, bado ni mwanachama. Alionekana kupendekeza angefanya makubaliano na ANC ikiwa kitabadilisha Rais Cyril Ramaphosa kama kiongozi.
"Nina tatizo na uongozi wa ANC, sio ANC yenyewe au wanachama wake," aliiambia BBC hivi majuzi.
Hata hivyo alisita kuzungumzia matarajio ya kuingia katika mapatano ya baada ya uchaguzi na ANC.
Chaguo jingine litakuwa kufanya kazi na EFF, inayoongozwa na Julius Malema, kiongozi wa zamani wa vijana wa ANC. Vyama hivyo viwili kwa sasa vinaunda muungano unaoendesha jiji kubwa zaidi nchini humo, Johannesburg.
Rekodi ya vyama 70 na watu huru 11 walikuwa wanagombea, huku Waafrika Kusini wakipigia kura bunge jipya na mabunge tisa ya majimbo.
DA imetia saini mkataba na 10 kati yao, wakikubali kuunda serikali ya mseto iwapo watapata kura za kutosha kukiondoa chama cha ANC mamlakani.
Lakini hii haijumuishi EFF au MK, ambao wangehitajika ili kuwa na wingi wa wabunge.
Wakati vyama hivyo vikihangaika kuunda muungano, Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta, ambaye anaongoza ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika nchini Afrika Kusini, alitoa ushauri wa kuunda miungano.
Alisema serikali za muungano zinafaa kuzingatia maeneo ya makubaliano badala ya tofauti.
“Niwatakie heri na matumaini kwamba uongozi utachukua uamuzi huu wa wananchi kwa mtazamo chanya,” alisema.

Imetafsiriwa na Asha Juma








