Sri Lanka: Wazazi walazimishwa kuchagua mtoto wa kwenda shule

M

Chanzo cha picha, MANENDRA

Malki mwenye umri wa miaka kumi amefurahi sana kubaki kitandani.

 Ameamka saa moja kabla ya dada zake wawili na kaka zake wawili ili aweze kutoa rangi nyekundu kwenye kucha zake.

Leo ni siku yake ya kwanza kurudi shuleni na anataka kuwa bila dosari.

Lakini ndugu zake lazima wabaki nyumbani - familia yake inaweza kumudu kumpeleka yeye tu shule.

Miezi sita iliyopita, Sri Lanka ilikumbwa na mgogoro mbaya zaidi wa kiuchumi tangu ilipopata uhuru.

Ingawa hali imeanza kutengamaa kwa kiasi kikubwa katika taifa hilo, athari za ukosefu wa ajira na kupanda kwa bei kubwa bado inaonekana miongoni mwa familia nyingi.

Ndoto mbaya ya kila mzazi

Mama yake Malki, Priyanthika amelazimika kusitisha masomo ya watoto wake ili wapate pesa kwa kuuza fataki. 

Gharama ya vyakula nchini Sri Lanka zilifikia viwango vya juu zaidi wakati mfumuko wa bei ulipofikia kiwango cha juu cha karibu 95%.

Baadhi ya siku, hakuna mtu katika familia ya Malki aliyekula.

 Licha ya kwamba shule ni bure nchini Sri Lanka, chakula hakitolewi. Ukiongeza gharama ya sare na usafiri, elimu ni anasa, Priyanthika hawezi kumudu tena.

M

Anasema anahitaji takriban rupia 400 kwa siku ($1.09, 90p) kwa kila mtoto ikiwa watarejea shuleni.

Akiwa amekaa katika nyumba yake ya chumba kimoja kwenye kitanda ambacho wanalala watu wengi, anafuta machozi usoni mwake.

"Watoto hawa wote walikuwa wakienda shule kila siku. Sina pesa za kuwapeleka sasa," anasema.

Malki anaweza kwenda shule kwa sababu viatu na sare zake bado zinafaa. 

Lakini mdogo wake Dulanjalee amejilaza kitandani akilia huku akisikitika kuwa leo si zamu yake kwenda shule.

"Mpenzi wangu, usilie," Priyanthika anasema. "Nitajaribu kukupeleka kesho."

MM

Elimu iliyoporomoka

Jua linapochomoza, watoto wanaenda darasani wakiharakisha kwenye barabara chafu wakiwa wamevalia sare nyeupe , wakiruka nyuma ya pikipiki au kurundikana kwenye bajaji.

Akiwa mjini, Prakrama Weerasinghe anaonekana akiwa na huzuni.Yeye ndiye mkuu wa Chuo Kikuu cha Sekondari cha Kotahena cha Colombo anaona dhiki ya kiuchumi kila siku.

"Shule zinapoanza, tunapokuwa na kusanyiko la asubuhi, watoto huwa wanazimia kwa njaa," asema.

Serikali inasema wameanza kusambaza mchele shuleni lakini shule kadhaa zilizowasiliana na BBC zinasema kuwa hazijapokea msaada wowote.

Bw Weerasinghe anasema mahudhurio ya wanafunzi yalipungua hadi 40% kabla ya kulazimika kuwaomba walimu kuleta chakula cha ziada ili kuwafanya wanafunzi warudi darasani.

Joseph Stalin ni Katibu Mkuu wa Muungano wa Walimu wa Ceylon.

Anaamini kuwa serikali haifahamu ongezeko la idadi ya familia zinazokata tamaa ya kupata elimu kwa sababu ya gharama.

MM

“Walimu wetu ndio wanaona watoto hawana chakula,” anasema. "Waathirika wakubwa wa mgogoro huu wa kiuchumi ni watoto."

"Serikali haitafuti jibu la suala hili. Limeonekana na kutambuliwa na UNICEF na wengine, badala ya serikali ya Sri Lanka."

UNICEF inasema itakuwa vigumu kwa watu kujilisha wenyewe katika miezi ijayo, huku mfumuko wa bei katika gharama za bidhaa za kimsingi kama vile mchele ukiendelea kulemaza familia.

Inatarajiwa watoto zaidi kote nchini watalazimika kuacha kuhudhuria darasa.

Matumaini ya mwisho?

Huku serikali ikionekana kutoweza kudhibiti hali hiyo, mashirika ya misaada yamelazimika kuingilia kati.

Samata Sarana ni shirika la kutoa misaada la Kikristo ambalo limekuwa likiwasaidia maskini zaidi Colombo kwa miongo mitatu.

Leo, ukumbi wake wa chakula umejaa wanafunzi wenye njaa kutoka shule mbalimbali za mji mkuu.

MM

Ingawa shirika la usaidizi linaweza kusaidia karibu watoto 200 kila siku, ni wazi kuwa linashindwa kukidhi mahitaji.

"Wanatupa chakula, mabasi ya kwenda nyumbani, wanatupa kila kitu ili sasa tusome," anasema Manoj mwenye umri wa miaka mitano huku akisubiri chakula cha mchana na kundi la marafiki zake.

Malki anaporudi nyumbani kutoka siku yake ya kwanza kurudi shuleni, anamwambia mama yake jinsi alivyofurahia kuona marafiki zake tena.

Lakini pia anamwambia mama yake anahitaji kitabu kipya cha kazi na anasema walimu wake wanaomba pesa za ziada kununua vifaa vya mradi wa shule.

Pesa ambayo familia haina.

"Tukifanikiwa kupata mlo wa leo, tunaendelea kuhangaika jinsi ya kupata chakula kesho," anasema Priyanthika.

"Hayo yamekuwa maisha yetu."