Tetesi za Soka Ulaya: Real Madrid wawasiliana na Dalot

Muda wa kusoma: Dakika 3

Real Madrid wanawasiliana na Diogo Dalot wa Manchester United, Mohamed Salah yuko tayari kukubali mkataba wa mwaka mmoja Liverpool, huku Wayne Rooney akikabiliwa na shinikizo Plymouth Argyle.

Real Madrid imewasiliana na beki wa Ureno Diogo Dalot, 25, na wameambiwa Manchester United itadai pauni milioni 41.5. Hata hivyo, beki wa Liverpool na Uingereza Trent Alexander-Arnold, 26, anasalia kuwa kipaumbele cha mabingwa hao wa Uhispania. (Relevo - kwa Kihispania)

Winga wa Misri Mohamed Salah yuko tayari kusaini kandarasi mpya ya mwaka mmoja katika klabu ya Liverpool lakini mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 anazidi kukasirishwa na jinsi klabu hiyo inavyoshughulikia mazungumzo. (Athletic - usajili unahitajika)

Paris St-Germain hawajafanya mazungumzo na Salah licha ya kuhusishwa na winga huyo. (Sky Sports)

West Ham wanamfikiria kocha wa Porto Sergio Conceicao kuchukua nafasi ya Julen Lopetegui, ambaye mustakabali wake kama kocha unakabiliwa na shinikizo kubwa. (Guardian)

Mkufunzi wa Manchester United Ruben Amorim anatazamiwa kufanya mazungumzo kuhusu mkataba mpya na winga wa Ivory Coast Amad Diallo, 22, ambaye kandarasi yake inakamilika msimu wa joto. (Telegraph - usajili unahitajika)

Bayern Munich wameanza mazungumzo ya kuongeza mkataba na winga wa Ujerumani Leroy Sane, 28. (Sky Germany)

Leicester City wanafikiria kusitisha mkataba wa mkopo wa msimu mzima wa mshambuliaji wa Crystal Palace Odsonne Edouard mwenye umri wa miaka 26 mwezi Januari. (Football Insider)

Wayne Rooney anapigania kibarua chake kama mkufunzi wa Plymouth Argyle baada ya matokeo mabaya. Mechi zijazo za nyumbani dhidi ya Oxford United na Swansea City zinakadiriwa kuwa muhimu. (Telegraph - usajili unahitajika)

Real Madrid wanapanga kumpa beki wa Uhispania Raul Asencio mkataba mpya wenye masharti bora zaidi. (Fabrizio Romano)

Aston Villa italenga beki mpya wa kulia kwenye dirisha la usajili la Januari. (Football Insider)

Tottenham na Newcastle United wanamfuatilia beki wa Lens wa Uzbekistan Abdukodir Khusanov, 20. (Telegraph - usajili unahitajika)

West Ham wameamua kumpa Vladimir Coufal mkataba mpya badala ya kumuuza beki huyo wa kulia wa Jamhuri ya Czech mwenye umri wa miaka 32. (Football Insider)

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi