Vita vya Israel, Marekani na Iran: Kwa nini Urusi haisaidii Iran?

    • Author, Elizabeth Fox
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 9

Vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran vimeiweka Urusi katika hali isiyoeleweka. Kwa upande mmoja, mapigano ya Mashariki ya Kati yanaondosha mazungumzo na rasilimali za nchi za Magharibi kutoka kwa kile kinachotokea Ukraine.

Kwa upande mwingine, Vladimir Putin amepoteza mshirika wake Ayatollah Ali Khamenei na kwa sasa anaiunga mkono Iran, mmoja wa washirika wake wakuu, kwa kauli tu.

Inaonekana hataki kuharibu uhusiano na Donald Trump.

"Kuhusu Iran, tuna uhusiano na ushirikiano wa kipekee," Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema katika mkutano wa kilele wa BRICS Oktoba 2024.

Mwaka huo, Tehran ilijiunga rasmi na klabu ya nchi ambazo Urusi inazitazama kama mbadala wa miungano ya Magharibi.

Miezi michache baadaye, Putin na Rais wa Iran Massoud Pezeshkian walisaini makubaliano ya "ushirikiano wa kimkakati" katika Kasri la Kremlin.

Katika nchi za Magharibi, uhusiano kati ya nchi hizi, hasa ushirikiano wao wa silaha, ulizidi kuleta wasiwasi. Wanasiasa wa Magharibi waliuita ushirikiano kati ya Moscow na Tehran "mhimili mpya wa uovu."

Hata hivyo, ushirikiano kati ya nchi hizo mbili haukuwa na nguvu ya kutosha kwa Moscow kuisaidia Iran wakati huu wa vita.

Wakati Israel na Marekani ziliposhambulia maeneo ya kijeshi ya Iran wakati wa "vita vya siku 12", Urusi ilitoa msaada wa maneno tu kwa Tehran.

Na baada ya vita vikubwa kuzuka Mashariki ya Kati, Februari 28, Kremlin imelaani vikali vitendo vya Marekani na Israel, lakini haijaingilia kati kile kinachoendelea.

Vladimir Putin alikosoa mauaji ya Kiongozi Mkuu Ali Khamenei, lakini hata hakutaja majina ya wale waliohusika katika kuuawa kwake.

Washirika wa Moscow

Mwezi Desemba 2024, Moscow ilitazama kwa utulivu kupinduliwa kwa dikteta wa Syria Bashar al-Assad.

Miezi michache iliyopita, kiongozi wa Venezuela Nicolas Maduro, mshirika wa muda mrefu wa Moscow, alikamatwa na wanajeshi wa Marekani na kupelekwa Marekani.

Haya yote yanaleta maswali: Je, thamani ya ushirikiano na Urusi ni ipi?

"Tangu mwanzo wa vita vyake nchini Ukraine, Moscow imekuwa ikijaribu kuimarisha ushawishi wake katika nchi za Kusini mwa Dunia," anaelezea Ruslan Suleymanov, mtaalamu wa mambo ya mashariki na katika Kituo cha NEST.

Katika hali hii, kile kilichotokea kwanza Venezuela na kisha Iran kinaweza kuchukuliwa kuwa pigo kwa itikadi ya Kremlin, anaongeza: "Katika nadharia Moscow inataka kuzilinda nchi za Kusini mwa Dunia, lakini kiuhalisia haina msaada ikiwa nchi za "Magharibi zitawateka nyara na hata kuwaua viongozi rafiki."

Kulingana na Hannah Notte, mkurugenzi wa mpango wa Eurasia katika Kituo cha Marekani cha Kuzuia Usambazaji wa Silaha za Maangamizi:

"Urusi haijaweza kufanya chochote kuzuia vita. Trump anafanya anachotaka. Kwa namna fulani, Urusi inaonekana haina msaada."

Lakini kulingana na Notte, hii haitaleta pigo kubwa kwa sifa ya Urusi miongoni mwa washirika wake.

"Katika sehemu kubwa ya Kusini mwa dunia, katika ulimwengu usio wa Magharibi, Urusi haionekani tu kama nchi iliyo vitani na Ukraine, pia ni nchi iliyo vitani na Magharibi," Notte anaelezea. "Na hilo, nadhani, husababisha mtazamo wa uvumilivu zaidi kwa Urusi: nchi zingine zinaelewa kwamba uwezo wake ni mdogo."

Zaidi ya hayo, Notte anasema nchi zinazotegemea usaidizi wa kijeshi wa Urusi — kama vile Mali, Burkina Faso, na Niger barani Afrika — mara nyingi hazina njia mbadala ila Urusi.

Je, sasa wataipa kisogo Urusi?

“Sidhani. Lakini wakati huo huo, nadhani sasa kila mtu anaelewa kwamba katika mgogoro mkubwa, Urusi haitakuwa 'shujaa wao,'" anasema Notte.

Pia isisahaulike, licha ya kukosoa mashambulizi dhidi ya Iran na kushirikiana nayo katika uwanja wa kijeshi na viwanda, Urusi haijawahi kuiahidi Tehran itapigana upande wake katika vita hivyo.

Hakuna kifungu kama hicho katika makubaliano yao ya "ushirikiano wa kimkakati.”

"Wajibu pekee Urusi ilio nao; iwapo vita vitatokea, hawataunga mkono upande wa adui," anasema Ruslan Suleymanov. "Huu, bila shaka, sio ushirikiano wa wa kijeshi. Ni tofauti na ushirikiano kati ya Urusi na Korea Kaskazini."

Ushirikiano wa Urusi na Iran

Kabla ya mashambulizi dhidi ya Iran mwezi Februari, vyombo vya habari na waangalizi walielekeza ongezeko la vifaa vya kijeshi vya Urusi kwenda Tehran: Iran ilipokea ndege za kivita, magari ya kivita, helikopta za mashambulizi, na hata mifumo ya ulinzi wa anga.

Baadhi ya silaha hizi, pamoja na teknolojia ya intaneti zinazotolewa na Urusi, zilitumiwa na serikali ya Iran kukandamiza maandamano makubwa mwezi Januari: maelfu ya Wairani walishambuliwa.

Nchi hizo zilikuwa zikishirikiana waziwazi katika anga za juu na teknolojia ya nyuklia. Urusi ilikuwa ikijenga kiwanda cha nguvu za nyuklia nchini Iran, na wanasayansi wa nyuklia wa Iran walikuwa wakitembelea Moscow kwa siri, kulingana na Financial Times.

Kulingana na Notte, haipaswi kusahaulika kwamba Iran, kulingana na baadhi ya ripoti, ilitaka ulinzi wa kisasa kutoka Urusi au silaha ambazo zingeiruhusu kuzuia vita kama vile vinavyotokea sasa.

"Kwa mfano, mifumo ya kisasa ya ulinzi wa anga au ndege za kivita za kisasa, kama vile Su-35. Hili ni suala tata ambalo limekuwepo katika uhusiano wa Urusi na Iran kwa muda mrefu. Lakini hatujawahi kuona Urusi ikitoa mifumo kama hiyo," anasema Notte.

Mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati na Asia, Ruslan Suleymanov pia anataja mizozo mingine kati ya nchi hizo mbili. Kwa mfano, Urusi haikuiunga mkono Iran katika mzozo wake wa kieneo dhidi ya UAE.

Tehran na Abu Dhabi zimekuwa zikibishana kwa miaka mingi kuhusu nani anamiliki visiwa vya Abu Musa, Greater na Lesser Tunb katika Ghuba ya Uajemi (inayodhibitiwa rasmi na Iran).

Urusi ilitoa wito wa "suluhisho la kidiplomasia la mzozo huo," jambo ambalo liliikasirisha Iran.

Tehran, kwa upande wake, ilitoa matamshi yanayounga mkono "unyakuzi wa Urusi katika eneo la Ukraine." Kwa hivyo, ushirikiano wa kijeshi na kiuchumi kati ya Urusi na Iran unaweza kutazamwa zaidi kama "ushirikiano ambao haujanyooka," anasema Suleymanov.

Kumekuwa na "mstari mwekundu" katika kile ambacho Urusi inakiona katika uungaji mkono wake kwa Tehran, anasema Nikol Grayevsky, profesa msaidizi katika Kitivo cha Masomo ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Sciences Po na mtaalamu wa mahusiano kati ya Urusi na Iran.

Anasema, “waangalizi wengi wametia chumvi ukaribu wa nchi hizo kutokana na ushirikiano wa kijeshi kati ya Moscow na Tehran katika vita nchini Ukraine.”

"Urusi na Iran zilipigana upande mmoja nchini Syria - Iran ilijifunza mengi kutoka kwa Urusi. Uzalishaji wa pamoja wa ndege zisizo na rubani za 'Shahad' ni jambo muhimu, lilikuwa na manufaa sana kwa Iran," Graevsky anasema.

"Lakini huu si muungano imara. Kwangu naona, unaweza kusambaza silaha, lakini hii haimaanishi una wajibu wa kujiunga na vita vya upande wake."

Kulingana na Reuters, serikali ya Iran "haikushtushwa" na kiwango cha usaidizi mdogo wa Urusi wakati wa vita vya siku 12.

Shirika hilo lilisema Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi, ambaye alifika Moscow wakati mapigano yalipopamba moto, kuwasilisha barua kutoka kwa Ayatollah Khamenei kwa Vladimir Putin, ambayo inadaiwa ni ya kuomba msaada zaidi kwa Tehran.

Kremlin ilisema Iran haikutoa barua yoyote, ingawa kulikuwa na "ishara fulani" kwamba ilitoa.

Moscow ilikataa shutuma kwamba usaidizi haukutosha: Msemaji wa serikali ya Urusi, Putin Dmitry Peskov alisema Urusi inaunga mkono Iran "kwa msimamo ulio wazi."

Hadi sasa, Moscow inataka kuwa mpatanishi kwa pande zinazopigana, lakini hakuna upande ulio tayari.

Urusi ilikuwa ikijivunia uhusiano imara na nchi zote katika eneo hilo, kuanzia Israel na Iran hadi nchi za Ghuba ya Uajemi kabla ya vita vyake na Ukraine.

Lakini baada ya vita kuanza, Kremlin imeongeza ushirikiano na Iran na vikosi vyake (kama vile kundi la Hamas huko Gaza na Hezbollah huko Lebanon), jambo ambalo limeharibu uhusiano wake na Israel kwa kiasi kikubwa.

"Sasa uwezo wa Urusi wa kuwa na ushawishi katika eneo hilo umepungua sana - imepoteza taswira yake kama "mpatanishi asiyeegemea upande wowote," anasema Nikol Graevski.

Kuthibitisha hofu za Urusi

Kuiunga mkono Tehran kunamaanisha kuingia katika mzozo wa moja kwa moja na Washington, wakati ambao Urusi inajaribu kuishinda Marekani katika vita nchini Ukraine.

Utawala wa Trump umekuwa ukifanya kazi kama mpatanishi kati ya Kremlin na Kyiv kwa miezi kadhaa iliyopita.

Ingawa hakuna maendeleo makubwa yaliyopatikana, katika kipindi hiki chote Vladimir Putin amejizuia kumkosoa vikali Donald Trump na Marekani. Jukumu la kumkosoa limekabidhiwa kwa Wizara ya Mambo ya Nje na maafisa wa ngazi ya chini.

Wataalamu wanaozungumza na BBC wanasema vita nchini Iran na kuondolewa madarakani kwa kiongozi wake kunaweza kuchelewesha kumalizika kwa vita nchini Ukraine, kwa kuifanya sera ya kigeni ya Urusi kuwa kali zaidi na kuifanya Kremlin kutoiamini zaidi Magharibi.

"Kinachoendelea kinathibitisha hofu zote za Urusi, na vita vya Marekani nchini Iran, vinahalalisha hofu kuhusu juhudi za Magharibi za kutaka mabadiliko ya utawala," anasema Nikol Graevski.

Israeli na Marekani zimeanzisha vita dhidi ya Iran licha ya mazungumzo kadhaa yaliyoongozwa na Oman.

Kwa kuwa Kremlin yenyewe inafanya mazungumzo na Ikulu ya White House, hii itaongeza tu kutoaminiana, anasema Hanna Notte: Kwa mtazamo wa Urusi, hakuna uhakika kwamba Marekani itajadiliana "kwa uaminifu."

Anasema ni muhimu kwa Putin kudumisha uhusiano wa "kirafiki" na Donald Trump ili asitoe sababu ya hatua kali dhidi ya Moscow.

Hii ina maana Rais wa Urusi lazima aweke uwiano kati ya ushupavu na tahadhari, Notte anasema. "Lakini uwiano huu utakuwa mgumu zaidi kuudumisha, kwani Marekani inaweza kuendelea kuwashambulia washirika wa Urusi, kama vile Cuba."

Matokeo ya moja kwa moja ya mapigano ya Mashariki ya Kati yanaweza kuimarisha shughuli za nyuklia za Urusi.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema, “matokeo ya vita hivi yanaweza kutoa "uamuzi wa mwisho" kuhusu ushawishi wa Urusi katika matukio ya kimataifa..

“Ikiwa tunaona kwamba Urusi haina msaada katika hali ya sasa, ni muhimu kuelewa hili ni kutokana na vita nchini Ukraine. Kwa mtazamo wa Moscow 'lazima tutoke na ushindi katika vita hivi - vinginevyo kwa nini tuliteseka sana?”

Moscow inanufaika?

Wataalamu waliozungumza na BBC wanakubali kwamba kwa namna fulani, mzozo katika Mashariki ya Kati unaweza kuwa na manufaa kwa Moscow.

Kulingana na Notte, moja ya manufaa ni ongezeko la bei ya mafuta, ambalo linaweza kutoa "nafuu" kwa bajeti ya Urusi. Matatizo katika soko la mafuta yaliyosababishwa na vita yanavyoweza kuinufaisha Moscow.

Si tu kwamba bei kubwa za mafuta huongeza mapato ya Urusi, pia usumbufu katika usambazaji katika mlango wa bahari wa Hormuz, huiruhusu Urusi kuongeza sehemu yake ya upelekaji wa mafuta kwenda China na India kupitia Ghuba.

Jambo lingine ni rasilimali za kijeshi ambazo Marekani italazimika kuzitumia katika operesheni dhidi ya Iran.

Rais Volodymyr Zelensky ameweka wazi kwamba ikiwa vita vitaendelea, inaweza kuathiri upataji wa silaha kwa Ukraine. Tatizo kubwa zaidi kwa Kiev ni uhaba wa vifaa vya kuzuia makombora, ambavyo ni muhimu kwa mifumo ya ulinzi wa anga.

Mahitaji yameongezeka nchini Marekani na miongoni mwa washirika katika Ghuba ya Uajemi kutokana na mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya Iran.

"Ongezeko lolote la matumizi ya mifumo ya Patriot ni faida kwa Urusi, kwani kutakuwa na mipaka ya kile Ukraine inachoweza kununua kutoka sokoni," anaelezea Nikol Graevsky wa Sciences Po.

Ukraine pia inakubali waziwazi ukweli huu.

Kwa upande mwingine, inasemekana kwamba mahitaji yanayoongezeka ya matumizi ya ndege zake zisizo na rubani nchini Iran hayatakuwa na athari kubwa kwa uwezo wa Urusi. Kulingana na wataalamu:

"Urusi ilikuwa ikitegemea Iran kwa ushirikiano wa ulinzi mwanzoni mwa vita nchini Ukraine - wakati Iran ilipotoa ndege zisizo na rubani za Shahed, pamoja na teknolojia na leseni zao za uzalishaji, 2022-2023. Lakini sasa tuko katika hatua ya vita ambapo Urusi haihitaji Iran kupigana. Urusi inaweza kutengeneza ndege zisizo na rubani za Shahed huko Alabuga," Notte anaelezea.

Vita vya Mashariki ya Kati tayari vimeathiri mwenendo wa mazungumzo ya pande tatu kati ya Urusi, Ukraine, na Marekani.

Kulingana na Volodymyr Zelensky, kusitishwa kwa mazungumzo hayo kunahusiana moja kwa moja na ukweli kwamba maafisa wa Marekani sasa wanaangazia Iran.

Kulingana na Graevsky, kinachoendelea Iran hakitaathiri moja kwa moja mwendo wa mapigano nchini Ukraine. "Lakini nadhani Urusi inaweza kujifunza mengi kwa kutazama vita hivi. Itakuwa somo muhimu kwake, itaona jinsi Magharibi inavyopigana vita leo," anasema.

"Putin hawezi kuonyesha "uwezo" wa Urusi katika wakati huu kwa sababu ametumia rasilimali na uwezo wote wa nchi hiyo kwa kuanzisha vita dhidi ya Ukraine."