Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Silaha zenye nguvu ambazo Marekani inatumia kushambulia Iran
Shambulio la pamoja la kijeshi lililofanywa na Marekani na Israel dhidi ya Iran ilianza tarehe 28 Februari 2026.
Mwanzoni mwa mashambulizi hayo, ndege za kivita za jeshi la anga la Israel aina ya F 15 Eagle, F 22 Raptor, na F 35 Lightning II, zilishambulia maeneo mbalimbali ndani ya Iran kwa kurusha mabomu kutoka angani.
Wakati huo huo, Marekani ilijiunga na operesheni hiyo kwa kurusha makombora ya masafa marefu aina ya Tomahawk cruise missile pamoja na kutekeleza mashambulizi ya anga.
Kwa mujibu wa taarifa za kijeshi, Marekani imekuwa ikijiandaa kutekeleza mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran tangu Januari mwaka huu.
Huu ni uchunguzi uliofanywa na shirika la BBC idhaa ya Sinhala, kuhusu aina ya silaha na uwezo wa kivita uliotumika saa 48 za kwanza za mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran.
Droni aina ya Lucas
Kituo cha central command, ambacho kinasimamia operesheni za kijeshi za Marekani katika Mashariki ya Kati, kimethibitisha kwamba Marekani imetumia kwa mara ya kwanza katika operesheni za vita, droni zinazojulikana kama Lucas.
Droni hizi za gharama nafuu, zilizoundwa kwa muundo unaofanana na droni za Iran aina ya Shahed 136, zimetengenezwa na kampuni ya ulinzi yenye makao yake eneo la Arizona, iitwayo SpektreWorks.
Ndege ya kurusha mabomu aina ya B-1
Ndege hiyo, inayojulikana kama Rockwell B 1 Lancer, ilitumiwa na Marekani Jumatatu iliyopita kushambulia vituo vya chini ya ardhi vya kuhifadhi makombora ya balistiki pamoja na maeneo ya kurushia makombora nchini Iran.
Vikosi vya ulinzi vya Marekani vilisema kwamba mashambulizi hayo yalifanywa na ndege za mabomu za masafa marefu aina ya Rockwell B 1 Lancer zilizoruka kutoka Marekani kwenda Iran, na kwamba ndege tatu zilishiriki katika shambulio hilo.
Ndege za Mabomu za Masafa Marefu za B 2
Ndege ya B 2 Spirit, iliyotengenezwa na Northrop Grumman, ni moja ya ndege za kurusha mabomu kwa masafa marefu zilizo za kisasa zaidi katika jeshi la anga la Marekani.
Mnamo Juni 2025, Marekani ilitumia ndege nne za aina hii kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran. Ndege hizi zilipaa kwa karibu saa 37 kutoka kambi ya jeshi ya Whiteman Air Force nchini Marekani ili kutekeleza shambulio hili.
Marekani mara nyingine tena ilitumia ndege nne za B 2 Spirit kushambulia maeneo tofauti ndani ya Iran tarehe 1 mwezi Machi.
Kulingana na mtengenezaji wa ndege hiyo, B 2 inaweza kubeba mzigo wa kilo 18,000. Hata hivyo, jeshi la anga la Marekani limesema kuwa B 2 imefanyiwa majaribio kwa mafanikio ya kubeba mabomu mawili ya aina ya GBU 57A/B bunker busters, ambayo uzito wake jumla ni takriban kilo 27,200 .
Ndege hii ya mabomu ya masafa marefu inaweza kuruka umbali wa takriban kilomita 11,000 bila kuongezwa mafuta, na hadi kilomita 18,500 baada ya kuongezwa mafuta mara moja, na hii inaifanya ndege hiyo kuweza kufika mahali popote duniani ndani ya masaa machache.
Ndege ya B 52
B 52 Stratofortress ni ndege ya mabomu ya kimkakati ya jeshi la anga la Marekani.
Ndege ya B 52, iliyotengenezwa na kampuni ya Boeing, imekuwa ikitumika na jeshi la anga la Marekani tangu mwaka 1955.
Ndege hii ya mabomu ya masafa marefu inaweza kubeba silaha hadi kilo 32,000 na ina uwezo wa kuruka umbali wa takriban kilomita 14,200 bila kuongezwa mafuta.
Mfumo wa ulinzi wa anga wa Patriot
Mfumo huu wa ulinzi wa anga unaojulikana kama Patriot, umetumika na jeshi la Marekani kama mfumo wake wa ulinzi wa anga tangu mwaka 1981 na hutumika na Marekani pamoja na nchi zake washirika.
Ndege ya MIM-104 Patriot inatumiwa na baadhi ya mataifa ya Ghuba, ikiwemo Saudi Arabia.
Mfumo wa ulinzi wa anga wa THAAD
Mfumo huu wa ulinzi wa anga, unaojulikana kama Terminal High Altitude Area Defense (THAAD), umeundwa kushambulia na kuharibu makombora ya balistiki ya masafa mafupi, ya kati, na ya wastani yanayotumika na Marekani.
Jeshi la Marekani ilianza kutumia mfumo huu wa ulinzi wa anga mwaka 2008, na umetengenezwa na kampuni ya Lockheed Martin Missile.
Gharama ya mfumo huu wa ulinzi wa anga ni takriban dola za Marekani bilioni 1.25, huku gharama ya kombora linalotumika katika mfumo huu ikiwa takriban dola milioni 12.7.
Mfumo wa ulinzi wa anga wa THAAD umetumika kwa ufanisi katika mashambulizi ya makombora ya balistiki mwaka 2022 dhidi ya Falme za Kiarabu na waasi wa Houthi wa Yemen, vita vya siku 12 kati ya Israel na Iran mwaka 2025, pamoja na vita vya sasa Mashariki ya Kati.
Ndege za kivita na ndege za upelelezi wa anga
Ndege za kivita zinazotumika na Marekani katika operesheni dhidi ya Iran ni F 15, F 16, F 18, F 35, na A 10.
Ndege hizi zinatokea katika kambi za kijeshi za Marekani zilizoko Mashariki ya Kati na pia kwenye meli za kivita zilizoko katika Bahari ya Arabia.
Zaidi ya hayo, kituo cha kutoa amri ya kijeshi ya Marekani, kinasema kwamba ndege za aina ya EA 18 Growler, ambazo zimewekwa na mifumo ya kuzima ishara, inayoweza kuzimisha mawasiliano ya kielektroniki na mifumo ya rada ya adui, pia zimekuwa zikitumika katika operesheni dhidi ya Iran.
Wakati huo huo, Marekani pia imetumia ndege za aina ya Airborne Early Warning & Control (AEW&C), ndege za upelelezi wa baharini P 8 Maritime Surveillance, na ndege za Airborne Communication Relay katika operesheni zake dhidi ya Iran.
Marekani imepeleka idadi ya ndege za kuchangia mafuta angani aina ya KC 46A, KC 135R, na KC 135T kusaidia operesheni zake za anga katika eneo la Mashariki ya Kati, Ujerumani na Uingereza.
Droni za MQ 9
Marekani imeishambulia Iran kwa kutumia droni za aina ya MQ 9 Reaper ambazo zina uwezo wa kufanya uchunguzi pamoja na mashambulizi.
MQ 9 Reaper, (ndege isiyo na rubani) inayoendeshwa na injini ya turboprop ilitumika na Marekani kumuua kamanda wa Iran wa jeshi la Revolutionary Guard, Qassem Soleimani, huko Iraq mwaka 2020.
MQ 9A ni toleo la droni ya MQ 9 Reaper lenye uwezo wa kuruka kwa zaidi ya masaa 27 na lina uwezo wa kufanya operesheni kwenye urefu wa hadi futi 50,000.
Inaweza kubeba makombora ya mashambulizi yenye uzito wa kilo 1,746.
Mfumo wa Makombora ya M-142
'M-142 High-Power Artillery Rocket System' ni mfumo wa kurusha makombora yenye majukumu mengi uliotengenezwa kutumika na jeshi la Marekani mwaka 2005.
Jeshi la Marekani limetumia mfumo wa makombora wa M-142 katika vita vya Afghanistan, vita vya Syria, vita vya Urusi dhidi ya Ukraine, na vita vinavyoendelea dhidi ya Iran.
Mfumo huu wa kurusha makombora, yenye thamani ya takriban dola za Marekani milioni 20, unaweza kusafirishwa pekee na ndege za mizigo aina ya C-17 Globemaster, C-5 Galaxy, na C-130 Hercules.
Meli za kubeba ndege za kivita
Meli ya kubeba ndege ya kivita USS Abraham Lincoln ilipelekwa eneo la Mashariki ya Kati wiki tano kabla ya Marekani kuanzisha operesheni dhidi ya Iran.
USS Abraham Lincoln ni meli ya tano ya ndege za kivita za Nimitz za Navy ya Marekani. Ni meli ya tatu ya jeshi la majini ya Marekani iliyopatiwa jina la Rais wa zamani wa Marekani, Abraham Lincoln.
Meli hii inayosogezwa kwa nguvu ya nyuklia ina kikosi cha watu 5,600 na ina uwezo wa kubeba ndege 90.
Wakati huo huo, USS Gerald R. Ford, meli kubwa zaidi ya ndege za kivita ya Marekani, ilipelekwa kutoka Bahari ya Caribbean hadi Mashariki ya Kati.
Meli ya ndege ya kivita, iliyopatiwa jina la Rais wa 38 wa Marekani, ina uwezo wa kubeba ndege 74 za kivita na ina kikosi cha karibu watu 4,600.
Zaidi ya hayo, Marekani pia kwa sasa imetuma meli kadhaa za mashambulizi zinazoweza kurusha makombora aina ya Tomahawk katika eneo la Mashariki ya Kati.
Marekani pia imetuma meli za kubeba mafuta katika pwani za Mashariki ya Kati ili kutoa vifaa na usaidizi kwa meli hizo.