Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump aonya 'kushambulia' Iran mara ishirini zaidi ikiwa itavuruga njia ya mafuta duniani

Rais wa Marekani anasema vita vya Iran vitakwisha "haraka sana" lakini Washington bado "haijashinda

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Putin aweka masharti magumu kusitishaji mapigano

    Taarifa kutoka Ikulu ya Marekani kuhusu mazungumzo ya Trump na Putin inaonyesha kuwa amekataa ombi la kusitisha mapigano haraka ya ardhini, angani na baharini, badala yake, Putin amekubali kusimamisha mashambulizi ya makombora ya masafa marefu kwenye miundombinu ya nishati ya Ukraine.

    Hili lilikuwa pendekezo la Ukraine ambalo Wamarekani walilipuuza wiki moja iliyopita.

    Trump na Putin pia wameonekana kukubaliana kufanya mazungumzo ya haraka kupata suluhu ya muda mrefu.

    Vladmir Putin amemthibitishia Trump "ahadi yake ya msingi" ya makubaliano ya azimio la amani lakini kwa masharti yafuatayo:

    • Taarifa ya Urusi inasema Putin alimwambia Trump "sharti muhimu" la kuzuia kuongezeka kwa mzozo "linapaswa kuwa kukomesha kabisa misaada ya kijeshi ya kigeni na kushirikishana taarifa za kijasusi na Ukraine"
    • Putin pia alizungumzia kuhusu "hitaji la kukomesha usajili wa wanajeshi wa kulazimishwa nchini Ukraine na upangaji upya wa Vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine"
    • Makubaliano yoyote "yanapaswa kuwa magumu, thabiti na ya muda mrefu" na lazima "yazingatie hitaji kamili la kuondoa sababu kuu za mgogoro", taarifa hiyo ilisema.
    • Pia lazima izingatie "maslahi halali ya Urusi katika eneo la usalama"
  2. Putin anataka 'kusaidia' Mashariki ya Kati - Trump

    Rais Donald Trump amezungumzia mazungumzo aliyofanya awali na Rais wa Urusi Vladimir Putin na kusema kuwa anataka 'kusaidia' Mashariki ya Kati.

    Akifafanua mazungumzo yake ya simu na Putin wakati akijibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari, Trump alisema, "Tulikuwa tunazungumzia kuhusu Ukraine, ambayo imekumbwa na mapigano yasiyoisha".

    "Kuna chuki kubwa kati ya Putin na Zelensky na inaonekana hawawezi kupatana. Lakini nadhani ilikuwa wito mzuri juu ya mada hii."

    Aliongeza kwamba pia walizungumzia kuhusu Mashariki ya Kati, na Putin "anataka kusaidia."

    "Nilimwambia, 'unaweza kuwa msaada zaidi kwa kumaliza vita ya Ukraine. Hilo litakuwa msaada mkubwa.' Lakini tulikuwa na mazungumzo mazuri sana."

    Pia siku ya Jumatatu, Putin alimpongeza Mojtaba Khamenei kwa kuwa kiongozi mkuu mpya wa Iran na akathibitisha tena uungaji mkono wa Moscow kwa Tehran, kulingana na ujumbe uliochapishwa kwenye tovuti ya Urusi.

    Mwishoni mwa wiki, vyombo kadhaa vya habari vya Marekani, ikiwa ni pamoja na The Washington Post, The New York Times, na Associated Press, viliwanukuu maafisa wasiojulikana wakidai kwamba Urusi ilikuwa ikiipa Iran taarifa za kijasusi zilizosaidia kulenga wanajeshi na mali Mashariki ya Kati.

    Hata hivyo, Urusi haijathibitisha rasmi kwamba inaisaidia Iran.

    Lakini imelaani mashambulizi hayo dhidi ya Iran, ikiyaita "hatua ya kizembe".

    Kinadharia, kuisaidia Iran kushambulia maeneo ya kimkakati ya Marekani kunaweza kuathiri uhusiano wa Urusi na utawala wa Trump.

    Marekani na Urusi zilikutana mara kadhaa mwaka huu kwa mazungumzo yenye lengo la kukomesha vita nchini Ukraine — mazungumzo ambayo Urusi imekuwa ikitumai Marekani itashinikiza Ukraine.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Waandamanaji wazuia basi lililobeba timu ya soka ya wanawake ya Iran waliopewa hifadhi Australia

    Wanaharakati wa Iran nchini Australia walilala barabarani nje ya hoteli ya Gold Coast kuzuia njia ya basi lililokuwa limewabeba wachezaji wa Iran.

    Wachezaji watano wa timu ya mpira wa miguu ya wanawake ya Iran wamepewa viza zenye kuhusisha na masuala ya kibinadamu nchini Australia baada ya kuondolewa katika Kombe la Asia.

    Siku ya Jumatatu, Trump aliitaka Australia "itoe hifadhi" kwa timu ya mpira wa miguu ya wanawake. "Marekani itawachukua ikiwa hamtakubali," aliongeza.

    Karibu saa moja baadaye, Trump alichapisha tena ujumbe akisema alikuwa amezungumza na Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese na "watano hao tayari walikuwa wanaendelea kupewa huduma huku wengine wakiwa njiani".

    Ujumbe wa Trump ulionekana pia kuashiria baadhi yao walihofia usalama wa familia zao huko Iran na hivyo walihisi lazima "warudi".

    Pia unaweza kusoma:

  4. Jeshi la Iran lamjibu Trump

    Kikosi cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC ) limejibu matamshi ya Trump kwamba vita nchini Iran vitaisha hivi karibuni, kikisema kwamba wao ndiyo "watakaoamua kumalizika kwa vita".

    Iran haitaruhusu "lita moja ya mafuta" kusafirishwa nje ya eneo hilo ikiwa mashambulizi ya Marekani na Israel yataendelea, IRGC imesema, kulingana na Reuters.

    Bei ya mafuta imekuwa ikibadilika badilika kutokana na kuongezeka kwa mvutano kuhusu Mlango-Bahari wa Hormuz, ambao ni muhimu kwa soko la mafuta duniani huku karibu moja ya tano ya mafuta duniani yakipita kwenye njia nyembamba ya maji.

    Soma zaidi:

  5. Trump asema vita 'vitaisha hivi karibuni'

    Rais Donald Trump amehudhuria mkutano wa Wabunge wa Republican huko Miami na kusema kuwa "vitaisha hivi karibuni".

    "Ndani ya wiki moja wangetushambulia kwa 100%. Walikuwa tayari. Walikuwa na makombora mengi zaidi ya mtu yeyote angefikiria, na wangetushambulia, lakini pia wangeshambulia Mashariki ya Kati na Israel yote."

    "Na kama wangekuwa na silaha za nyuklia, wangeitumia dhidi ya Israeli. Na hili lingekuwa shambulizi kubwa. Ninajua walikuwa na maeneo yote ya makombora na vifyatuaji vyote ambavyo tumeviharibu, karibu 80% kufikia sasa, tumeharibu sehemu kubwa ya makombora. Wana kidogo sana waliobaki nayo."

    Trump aliendelea kusema jeshi limefanya "kazi nzuri".

    "Na makombora yamepunguzwa kwa kiasi kikubwa. Ndege zisizo na rubani zimedondoshwa, na tunashambulia mahali wanapotengeneza ndege zisizo na rubani," Trump alisema.

    "Tunawajua wote, na tunawamaliza kabisa. Pale, wanapotengeneza ndege zisizo na rubani. Kazi kubwa inaendelea. Lakini tutakuwa na ulimwengu salama zaidi mara tu itakapokamilika, na itakamilika hivi karibuni."

    Vita havitaisha wiki hii, lakini 'hivi karibuni' - Trump

    Akijibu swali kutoka kwa mwandishi wa habari kuhusu muda ambao "operesheni" ya kijeshi ya Marekani itachukua nchini Iran, Trump alirejelea alichosema awali, operesheni hiyo itaisha "hivi karibuni" - lakini si wiki hii.

    "Nafkiri hivi karibuni. Kila kitu Iran iko nacho kimemalizwa, ikiwa ni pamoja na uongozi wao," alisema.

    "Watu wengi hata hawajasikia kuhusu kiongozi wanayemzungumzia (kuchukua nafasi ya ayatollah)," Trump alisema.

    Soma zaidi:

  6. Trump aonya 'kushambulia' Iran mara ishirini zaidi ikiwa itavuruga njia ya mafuta duniani

    Rais Donald Trump ametoa onyo lingine kwa Iran kuhusu kuvuruga usafirishaji wa njia ya meli katika Mlango-Bahari wa Hormuz.

    "Ikiwa Iran itafanya chochote kinachozuia usafirishaji wa mafuta ndani ya Mlango-Bahari wa Hormuz, itashambuliwa na Marekani mara ISHIRINI ZAIDI kuliko ilivyoshambuliwa hadi kufikia sasa," Trump alisema katika ujumbe wa mtandaoni.

    Takriban 20% ya mafuta duniani hupita kwenye mlango bahari huo na vita hivyo vimepunguza sana safari za usafirishaji mafuta baharini na kusababisha bei ya mafuta duniani kupanda.

    "Kama haitoshi, tutataja maeneo ya kuyalenga kwa urahisi na kuharibiwa kiasi kwamba itakuwa vigumu kwa Iran kujengwa tena, kama Taifa — Vifo, matukio ya Moto, na Ghadhabu vitatawala — Lakini natumaini, na kuomba, kwamba isitokee!" alisema.

    Bei ya mafuta yashuka baada ya Trump kuashiria kwamba vita vitaisha hivi karibuni

    Wakati huo huo, bei ya mafuta duniani ilishuka mapema Jumanne asubuhi barani Asia.

    Bei ilishuka kwa takriban 8.5% kwa pipa la $92.50 (£68.85). Mafuta yaliyouzwa Marekani pia yalishuka kwa takriban 9%, hadi $88.60 kwa pipa.

    Bei bado ziko juu kwa takriban 30% kuliko ilivyokuwa mwanzoni mwa mzozo.

    Kushuka huko kunafuatia matamshi ya Rais wa Marekani Donald Trump Jumatatu kwamba vita vitaisha "hivi karibuni".

    Soma zaidi:

  7. Hujambo msomaji wetu. Karibu katika matangazo yetu mubashara ya tarehe 10/03/2026.