Siku ya Kiswahili Duniani:Kwa nini Kiswahili kutumiwa Uganda itakuwa changamoto?
Na Isaac Mumena
BBC Swahili,Kampala

Ulimwengu leo unaadhimisha siku ya lugha ya Kiswahili .Ni Maadhimisho ambayo yamekuja na sadfa nzuri-baraza la mawaziri nchini Uganda kuidhinisha Kiswahili liwe somo la lazima katika shule za msingi na upili nchini humo .
Ni hatua nzuri hasa ikizingatia kwamba mwaka huu ,umekuwa mzuri kwa ukuaji wa lugha hiyo baada ya nchi kadhaa na taasisi kubwa kama vile Umoja wa Afrika kuidhinisha iwe mojawapo ya lugha zake za kikazi
Kuhusiana na uamuzi huo wa Uganda ,itawalazimu wananchi wa taifa hilo sasa kujifunza Kiswahili hatua ambayo imewapa wengi wanaoienzi lugha hiyo tabasamu hasa katika kanda hii ya Afrika mashariki .
Ndoto ya kuwa na lugha moja miongoni mwa watu wa eneo hili inakaribia kutimia lakini huenda safari hii isiwe rahisi na telezi kama inavyoonekana .
Kwenye shule za msingi Kingereza na lugha za mama kama vile Kiganda ndizo zinazofunzwa katika shule za msingi .
Siku ya Jumanne waziri wa TEHEMA nchini humo Chris Baryomunsi alifahamisha mkutano wa wandishi habari mjini Kampala kuwa mkutano wa Baraza la mawaziri ulioongozwa na Rais Museveni uliridhia Kiswahili kiwe soma la lazima katika shule zote nchini humo .
“ Katiba yetu ya Uganda inaeleza wazi kuwa Kiswahili ni lugha ya pili ya taifa nchini Uganda, lakini raia wa Uganda wamekuwa nyuma kujifunza kiswahili huku lugha hiyo ikitumiwa sana nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika mashariki, hivyo tunatakiwa kujifunza haraka na kuanza kuzungumuza Kiswahili na wenzetu wa Jumuiya ya Afrika mashariki.Ingawaje kuna baadhi ya shule zinazofundisha Kiswahili, sasa ni lazima kwa kila shule”.Alisema Baryomunsi
Tamko hilo limepokelewaje Uganda?

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tamko hilo limepongezwa na wadau wa Kiswali nchini lakini bado wana hofu iwapo pendekezo hilo litatekelezwa.
Nilitembelea Chuo Kikuu cha Kyambogo jijini Kampala na kuzungumuza na baadhi ya wahadhiri ili kupata walivyopokea tangazo hilo .
Mwalimu Yunus Luubuka anasema ni tamko zuri katika kuendeleza lugha ya Kiswahili nchini .
“Ni tamko zuri katika kuendeleza lugha ya kiswahili Uganda na tumesubiri kwa muda mrefu ... pia ni zawadi kutoka kwa Rais Museveni ikiwa leo dunia inaadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani'. Anaongeza.
Hata hivyo anaiomba serikali kuhakikisha kwamba mara hii pendekezo hilo linatekelezwa kwani wamezungumuza kwa mda mrefu kufundisha lugha ya Kiswahili katika shule bila kutekelezwa.
'Maoni yangu ni kwamba Serikali inafaa kuamuru Wizara ya Elimu na Michezo kufundisha shuleni sio kupendekeza, hapo litatekelezwa kwa haraka”.
Mhadhiri mwingine Mbaruku Julius naye anatoa maoni yake akisema- “Kwanza Kiswahili kifundishwe na kutahiniwa, kwani kuna walimu wengi nchini Uganda hawana kazi kwa sababu vyuo vyote vya walimu Uganda vinafundisha Kiswahili lakini hawana shule za kufundisha hiyo itakuwa fursa kwa walimu”.
Raia wa Uganda wana historia tofauti na lugha ya Kiswahili. Watu wengi wanaichukulia lugha hiyo kwa aina fulani ya uwoga .
Wanadai ilitumiwa katika serikali zilizopita za Idd Amin na Milton Obote na askari wa serikali hizo ambao mara nyingi walionekana kuwakandamiza raia.Hilo liliwafanya wengi kukichukia Kiswahili .
Tangu Rais Yoweri Museveni kuingia madarakani mwaka 1986 alijaribu kugeuza fikra za Waganda kuwa Kiswahili sio lugha mbaya kama wanavyofikiria lakini baadhi ya watu bado wana dhana hiyo kuhusu Kiswahili.
Mwalimu Mike Bamujeya ana mapendekezo ya kuvutia wananchi- “Kwanza walimu wa Kiswahili wapewe mshahara wa juu kama walimu wa Sayansi ili watu wafahamu Kiswahili ni ajira, pili kuhamasisha wananchi na kuundwa kwa Baraza la Kiswahili litakaloshughulikia lugha ya Kiswahili kama inavyotakiwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki”
Watu wengi wa Kati mwa Uganda , mkoa wa Buganda ambako jamii kubwa ni Waganda wanapinga somo la Kiswahili wakidai litatokomeza lugha yao ya Kiganda jambo ambalo wadau wanasema sio kweli
Mtazamo wa wadau wa Kiswahili nchini Uganda ni kwamba wakati umefika Waganda kuanza kuzungumuza lugha ya Kiswahili kama mataifa mengine ya Jumuiya ya Afrika Mashariki -Tanzania, Kenya na Burundi.
Leo tarehe 7 Julai ni siku ya kuadhimisha lugha ya Kiswahili duniani mjini na Kampala wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbali mbali wanaaadhimisha siku hii kwenye viwanja vya ubalozi wa Tanzania mjini Kampala.














