Lugha ya Kiswahili - kutoka kuwa "lahaja isiyojulikana" hadi lugha inayozungumzwa na watu wengi duniani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Karne nyingi zilizopita ilijulikana kama lugha ya "giza"; leo hii imekuwa inazungumzwa zaidi katika bara ambalo linakua zaidi kidemografia.
Kiswahili -pia huitwa Swahili-, ni lugha ya Kiafrika ambayo kwa miaka mingi imekuwa na ushawishi mkubwa kutoka katika lugha nyingine kama vile Kiarabu, Kiingereza na Kireno.
Asili yake ni pwani ya mashariki ya bara la Afrika, ni sehemu ya familia ya lughat ya Kibantu, aina ya lugha zinazozungumzwa na watu wa Kibantu katika nusu ya kusini mwa Afrika.
Leo, ikiwa na wazungumzaji zaidi ya milioni 200, ni moja ya lugha 10 zinazozungumzwa na watu wengi zaidi duniani na katika miaka ya hivi karibuni hatua kubwa zimefanyika barani Afrika kuifanya kuwa lugha ya bara hilo.
Kiswahili kinachukua takriban 40% ya msamiati wake moja kwa moja kutoka Kiarabu, ambacho kimeshawishiwa kwa karne nyingi na wafanyabiashara kutoka Uarabuni waliokuja pwani ya Afrika Mashariki kutafuta masoko mapya.
Waswahili ndio walikuwa wengi katika ukanda huo, kuanzia Mogadishu, mji mkuu wa Somalia, hadi Mto Rovuma nchini Msumbiji, ukichukua sehemu za Kenya, Tanzania na sehemu za magharibi mwa nchi ambayo sasa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Mawasiliano kati ya mji huu wa pwani na ulimwengu wa Waarabu na Waajemi yalianza muda mrefu kabla ya kuwasili kwa Uislamu karne ya 8.
Lakini baadaye, chini ya ukoloni wa Ujerumani na Uingereza mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20, ilipitishwa kama lugha ya kutumika katika utawala wa ndani na elimu.
"Ilianza kama lugha ndogo ya pwani katika Afrika Mashariki, ambayo baadaye ilikutana na wafanyabiashara kutoka ulimwengu wa Kiarabu na Ureno, hasa," Ida Hadjivayanis, profesa na mtaalamu wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha London aliiambia BBC Mundo.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Lakini lugha hiyo ilikua ghafla na pengine ndiyo maana watu waliona kuwa ni lugha ya 'giza': kutokana na jinsi ilivyokua kwa haraka kutokana na biashara katika Bahari ya Hindi na utumwa," anaongeza.
Lugha "rahisi".
Moja ya sababu za ushindi wake barani Afrika ni kwamba kwa kuwa lugha ya Kibantu, ilikubaliwa haraka na Wabantu, ambao waliweza kuisoma na kuielewa kwa urahisi kwa sababu tayari walikuwa wakizungumza lugha zingine za familia moja.
Kwa hakika, Kiswahili kinasemekana kuwa lugha rahisi zaidi ya Kiafrika kwa mzungumzaji wa Kiingereza au lugha ya kilatini kujifunza.
Ni mojawapo ya lugha chache za Kiafrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo hazitofautiani kimatamshi kati ya saruffi na muundo kama Kiingereza au Kihispania.
Pia ni rahisi zaidi kusoma, kwani maneno yanasomwa jinsi yalivyoandikwa, kama vile Kihispania au Kiitaliano.
Vivyo hivyo, kwa mtu anayezungumza Kiarabu inaweza kuwa rahisi kujifunza Kiswahili kwa sababu ya wingi wa maneno ambayo ameazima kutoka Kiarabu.
"Lugha iliyotelekezwa na wakoloni"
Kwa Mghana Annabel Lankai, anayesoma Kiswahili, Afrika inapaswa "kuwa na kitu ambacho ni chetu na kwa ajili yetu"
Darasa la Annabel katika Chuo Kikuu cha Ghana, kilichopo Accra, mji mkuu wa nchi hiyo, ni takriban kilomita 4,500 magharibi mwa mahali palipo zaliwa Kiswahili: pwani ya Kenya na Tanzania.
Katika mahojiano na BBC, Annabel anakumbuka kwamba marafiki na familia yake mwanzoni hawakuelewa kwa nini alikuwa akisoma Kiswahili.

Chanzo cha picha, ANNABEL LANKAI
"Ni wakati wa sisi kuachana na lugha ya wakoloni," anasema kijana huyo mwenye umri wa miaka 23.
Kwa miaka kadhaa sasa, Waafrika wengi wametaka Kiswahili iwe lugha mbadala ya Kiingereza, Kifaransa au Kireno kama lingua franca katika bara au angalau kama lugha inayoeleweka na watu wengi.
Na kidogo kidogo inafanikiwa.
Inashamiri
Mwaka jana UNESCO iliteua Julai 7 kuwa Siku ya Kiswahili Duniani na mapema mwaka huu Umoja wa Afrika (AU) uliidhinisha kuwa lugha yake rasmi ya kikazi.
Pia ni lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Wazungumzaji wa Kiswahili leo wamesambaa katika nchi zaidi ya 14 ,ni rasmi nchini Tanzania na Kenya, lakini pia hutumiwa sana nchini Uganda, Visiwa vya Comoro na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Kwa kiasi kidogo, ina wazungumzaji katika nchi za Burundi, Rwanda, Msumbiji, Malawi, Sudan Kusini, Somalia, Zambia, na Oman na Yemen katika Mashariki ya Kati.
Baadhi ya mataifa ya kusini mwa Afrika, kama vile Afŕika Kusini na Botswana, yameiingiza shuleni huku Namibia ikifikiria kufanya hivyo.
Kaskazini zaidi, Chuo Kikuu cha Addis Ababa cha Ethiopia hivi karibuni kilitangaza kwamba kitaanza kufundisha Kiswahili.
Wazungumzaji zaidi ya milioni 200 wa Kiswahili wanaitumia lugha hiyo. Wale wanaoizungumza kama lugha mama ni wachache, karibu milioni 15 kulingana na makadirio.
"Katika Afrika Mashariki kuna watu wa makabila mbalimbali, wenye lugha tofauti za asili, ambao wameamua kutumia Kiswahili kuwa lugha yao ya pili ili kuwasiliana wao kwa wao," anasema Ida Hadjivayanis.
Lugha ya ukombozi
Profesa anahakikisha kwamba lugha hii kwa sasa ina jukumu muhimu sana katika ujenzi wa "umoja wa Kiafrika".
"Kiswahili lazima iwe lugha ya Kiafrika. Sidhani kama inapaswa kuwa lugha pekee, lakini inapaswa kuwa rasilimali muhimu ya watu wa Afrika," anaongeza.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wazo la Kiswahili kuwa lugha ya Kiafrika lilianzishwa katika miaka ya 1960 na rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere, ambaye alitumia lugha hiyo kuunganisha taifa lake baada ya uhuru.
"Nyerere alikuwa na mchango mkubwa sana katika ukuaji wa matumizi ya Kiswahili, alielewa kuwa watu wake walihitaji lugha hiyo kwa ajili ya biashara na kuelewana. Aliikubali kwa dhana ya Uafrika na aliiona kama aina ya ukombozi," anaelezea Hadjivayanis.
"Kwake, ilikuwa lugha ya ukombozi," anaongeza.
Katika muongo huo huo, mwandishi wa Nigeria Wole Soyinka, mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Fasihi ya 1986, alisisitiza matumizi ya Kiswahili kama lugha ya kuvuka bara.
"Alikuwa Mnigeria, angeweza kuchagua lugha ya Kinigeria, lakini alipendelea Kiswahili kwa sababu alishiriki wazo la Nyerere na aliona kuwa ni lugha ya ukombozi."
Mengi ya kufanya
Ingawa matumizi ya lugha yamekua kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni, haitakuwa kazi rahisi kukifanya Kiswahili kuwa lugha bora kabisa ya Kiafrika.
Itahitaji utashi wa kisiasa na kuwekeza pesa nyingi ili lugha ifike na kufundishwa kila kona ya bara hili.
Leo, lugha za Ulaya zinaendelea kutawala barani Afrika.
Kiingereza kinaongoza kama lugha rasmi au ya pili katika nchi 27 kati ya 54 barani Afrika, wakati Kifaransa ni rasmi katika nchi 21 kati hizo.
Ingawa Kiswahili kinapendwa Afrika Mashariki, Kati na Kusini, umaarufu wake bado haujaenea katika bara zima.
Kiarabu kinaendelea kutawala kaskazini, wakati magharibi kuna lugha za Kiafrika, kama vile Hausa na Yoruba, ambazo zinaweza kushindana kwa hadhi ya lingua franca katika eneo hilo.
Kwa sababu hii, wataalamu wa lugha (Wanaisimu) wengi wana imani kwamba Kiswahili kinaweza kujiimarisha, kwa juhudi ndogo, kama lugha bora katikati na kusini mwa bara.
Lakini wengine wana shaka kuwa, angalau katika siku za usoni, itakuwa lugha ya bara zima.













