Vifo vya wanamichezo wa Afrika Mwaka 2024

Chanzo cha picha, Getty Images/Reuters
Afrika iliwaaga magwiji kadhaa wa michezo katika kipindi cha 2024.
Katika orodha inayojumuisha mabingwa wa dunia na wavunja rekodi pamoja na nyota wa soka na mpira wa vikapu, vifo kadhaa vilisababisha mshtuko kote ulimwenguni.
BBC Sport Africa inaangazia wachache wanaojulikana ambao hawako nasi tena.
Dikembe Mutombo (DR Congo)
Marais wa zamani wa Marekani Bill Clinton na Barack Obama walikuwa miongoni mwa waliotuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Dikembe Mutombo mwishoni mwa Septemba, wakimsifu kwa aliacha historia nje ya mipaka ya uwanja wa mpira wa vikapu.
Nyota Bora wa NBA mara nane,alikuwa mchezaji stadi wa mpira wa kikapu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.Alicheza misimu 18 katika ligi ya Chama cha Taifa cha Mpira wa Kikapu maarufu kama NBA nchini Marekani.
Hata hivyo Mutombo atakumbukwa sana kwa shughuli zake za kibindamu katika nchi yake ya asili DR Congo na kote barani Afrika na ustadi wake uwanjani kufuatia kifo chake akiwa na umri wa miaka 58 kutokana na saratani ya ubongo.
Miongoni mwa miradi aliyofadhili ni hospitali ya Kinshasa na taasisi ya elimu katika jiji la Mbuji-May.
Rebecca Cheptegei (Uganda)

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 33 aliathiriwa na unyanyasaji wa kijinsia wiki chache tu baada ya kushiriki katika Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024.
Cheptegei alifariki siku chache baada ya kumwagiwa petroli na kuchomwa moto na aliyekuwa mpenzi wake.
Ripoti iliyowasilishwa na msimamizi wa eneo hilo ilidai kuwa raia huyo wa Uganda na mpenzi wake wa zamani walikuwa wakizozana kuhusu kipande cha ardhi kaskazini-magharibi mwa Kenya, ambako alikuwa akiishi na kupata mafunzo.
Baada ya kuwa mwanariadha wa tatu kuuawa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Taasisi ya Riadha ya kimataifa imetangaza kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia kuwa kipaumbele chake.
Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 - ambapo aliibuka wa 44 - ilikuwa mbio za mwisho za Cheptegei.
Kelvin Kiptum (Kenya)

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanariadha mwingine wa mbio za masafa marefu ambaye kibarua chake kilikatizwa, Kiptum na kocha wake walifariki katika ajali ya barabarani nchini Kenya mwezi Februari.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 anasalia kushikilia rekodi ya dunia ya mbio za marathon baada ya kufikia muda wa saa mbili na sekunde 35 mjini Chicago Oktoba 2023.
Baada ya alama hiyo, Kiptum - ambaye hakuweza kumudu jozi ya viatu ili kukimbia katika mbio zake kuu za kwanza za ushindani mnamo 2018 - alisema kazi yake ilikuwa ''imeanza".
Kifo chake cha ghafla kiliwaacha wengi nchini Kenya na ulimwengu mzima katika mshangao, huku watu wengi wakihisi pengo kubwa.
Baba huyo wa watoto wawili alionekana kuwa mwanamume wa kwanza kukimbia mbio fupi za saa mbili katika mashindano ya wazi.
Rachid Mekhloufi (Algeria)

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mshambuliaji huyo alikua alama ya Algeria kupigania uhuru alipojiondoa katika klabu ya Saint-Etienne ya Ufaransa katika nusu ya kwanza ya 1958.
Mekhloufi alisafiri hadi Tunis na kusaidia kupatikana kwa timu ya National Liberation Front (FLN) pamoja na wachezaji wenye nia moja - ambao wengi wao walikuwa wameishi Ufaransa.
Akiwa ameichezea Ufaransa mechi nne, kitendo chake kilimaanisha kuwa alisalimisha nafasi ya kuichezea Les Bleus kwenye Kombe la Dunia la Fifa nchini Sweden majira ya kiangazi.
Timu ya FLN ilicheza mechi kote Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, Ulaya Mashariki na Kusini Mashariki mwa Asia ili kuhamasisha jitihada za nchi yake kudai uhuru, ambayo hatimaye ilipata mwaka wa 1962.
Baadaye Mekhloufi aliifundisha Algeria, ikiwa ni pamoja na kuwa katika majukumu ya pamoja wakati Les Verts ilipoifunga Ujerumani kwenye Kombe la Dunia la 1982, na aliwahi kuwa rais wa shirikisho la soka la nchi hiyo. Alifikwa na umauti akiwa na umri wa miaka 88 mnamo Novemba.
Jacques Freitag (Afrika kusini)

Chanzo cha picha, Getty Images
Bingwa huyo wa dunia wa kuruka juu 2003 alipatikana amekufa akiwa na majeraha mengi ya risasi katika makaburi huko Pretoria mwezi Julai, baada ya kutoweka wiki mbili kabla.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 42, ambaye mama yake alikuwa bingwa wa kitaifa wa kuruka juu, alikuwa miongoni mwa kundi lililochaguliwa la wanariadha walioshinda mataji ya binafsi ya dunia katika ngazi ya Under-18, Under-20 na ngazi ya juu.
Alishinda dhahabu kwenye Mashindano ya Dunia huko Paris kwa kipimo cha 2.35m, na kuwa Mwafrika wa kwanza kushinda taji la ulimwengu.
Freitag alishindwa kufika fainali katika Olimpiki ya 2004 huko Athens lakini mwaka uliofuata aliendeleza rekodi yake ya Afrika hadi 2.38m - alama ambayo bado iko hadi leo.
Haikuwa kifo chake pekee cha kikatili nchini Afrika Kusini mwaka huu, kwani beki wa Kaizer Chiefs Luke Fleurs aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa na umri wa miaka 24 katika wizi wa gari mwezi April.
Issa Hayatou (Cameroon)

Chanzo cha picha, Getty Images
Bingwa wa mbio za kitaifa ambaye pia aliwakilisha nchi yake katika mpira wa vikapu, Hayatou alijitolea maisha yake yote kusimamia michezo na kusaidia kubadilisha Shirikisho la Soka la Afrika katika kipindi cha miaka 29 ya utawala wake kama rais kutoka 1988 hadi 2017.
Aliboresha mizania ya shirikisho, aliandaa mashindano zaidi kusaidia kukuza wachezaji na miundombinu katika bara zima, na alisimamia upanuzi wa Kombe la Mataifa ya Afrika kutoka timu nane hadi 16.
Raia huyo wa Cameroon alikuwa mjumbe wa muda mrefu katika kamati kuu ya Fifa - na alikaimu kwa muda mfupi kama rais wa shirikisho la soka duniani.
Hayatou alihusishwa na kashfa, ikiwa ni pamoja na madai kwamba alipokea hongo wakati Qatar ikiwania Kombe la Dunia la 2022, lakini alikanusha makosa yote.
Mtoto wa sultani, wengi wanaamini Hayatou alikuza maslahi ya soka la Afrika kuliko wengi waliotangulia au waliofuata tangu hapo. Alikufa akiwa na umri wa miaka 77 mnamo Agosti.
Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi












