Mashirika ya Umma Tanzania kuendelea kupata hasara mpaka lini?

g

Chanzo cha picha, TRC

    • Author, Yusuph Mazimu
    • Akiripoti kutoka, Dar es Salaam
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Nilikua mmoja wa watu karibu 70 tumekaa kwenye viti kusubiri huduma na wengine kusindikiza wagonjwa katika hospitali moja jijini Dar es Salaam. Lilikuwa eneo lenye skrini kubwa ya televisheni ikining'inia ukutani, lakini sauti yake ilikuwa inazimwa na makelele, watoto wakilia, wauguzi wakiita wagonjwa kwa namba, na watu wakizungumza kwa sauti kana kwamba hapakuwa na taarifa muhimu inayoendelea kwenye TV.

Nilikuwa nimekaa nyuma kabisa, takribani mita saba kutoka kwenye televisheni. Macho yangu yakatua kwenye sura ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere. Nilijua alikuwa anawasilisha ripoti yake ya mwaka kuhusu hesabu za mashirika ya umma na taasisi za serikali.

Nilihisi msukumo wa kusogea karibu. Nikasimama na kuanza kusogea, lakini hakukuwa na kiti kilicho wazi. Jamaa mmoja aliyekuwa ameketi akaniangalia, akasema, "Kaka kaa hapa." Akanipisha, nikakaa. Nilimtazama kwa shukrani, kisha nikajielekeza kwenye televisheni.

Nilikuwa na shauku kubwa ya kusikiliza ripoti hiyo, lakini jambo moja lilinishangaza: ni watu wachache mno walionekana kujali. Wengi walikuwa na simu zao, wengine wakipiga soga. Kulikuwa na hisia kana kwamba taarifa hizi hazikuhusu mtu yeyote hapo.

Roho iliniuma. Kwa nini watu hawa wanapuuza ripoti zinazohusu fedha zao? Mkaguzi huyu ni jicho lao, ndiye anayekagua matumizi ya kodi zao, lakini hakuna anayemsikiliza.

Dakika chache baadaye, yule aliyenipisha kiti akarudi haraka. Alikuwa amesahau funguo zake za pikipiki. Alipoinama kuzichukua, nikamwita, "Kaka, mbona hutaki kufuatilia ripoti yenu?"

Akauliza, "Ripoti gani?"

"Ya CAG," nikamjibu.

Akatikisa kichwa kwa uchovu, "Aaah! Najua tu… mambo ni yale yale. Hasara tu."

Aliamua kusimama dakika chache kufuatilia TV. Aliposikia mashirika kadhaa yakitajwa kwa hasara kubwa, akageuka kunitazama na kusema kwa sauti ya unyonge, "Si unasikia mwenyewe? Kila siku hasara… sijui hii hasara itakwisha lini?"

Aliyeyasema hayo ni mwananchi wa kawaida. Sitaki kumuita jina lake halisi, lakini kwa makala hii nitamuita Getorare.

Swali lake lilikaa kichwani mwangu. Kila mwaka tunasikia mashirika ya umma yanapata hasara. Je, kweli kuna siku hii hali itabadilika? Au ni jambo ambalo tumezoea tu? Hasara hizi mpaka lini?

Ripoti ya CAG na hali ya Mashirika ya Umma

.
Maelezo ya picha, Jedwali kuonyesha, hasara kwa baadhi ya mashirika makubwa katika kipindi cha miaka mitatu kuanzi mwaka wa fedha 2021/2022 mpaka 2023/2024
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ripoti ya CAG ya mwaka wa fedha 2023/2024, iliyowasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan, imeonesha kuwa mashirika kadhaa ya umma bado yanaendelea kupata hasara kubwa licha ya uwekezaji mkubwa wa serikali.

Kwa mfano, Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ilipokea ruzuku ya serikali ya shilingi bilioni 99.8, lakini bado ikapata hasara ya shilingi bilioni 91.8. Hasara hii ni ongezeko la asilimia 62 kutoka shilingi bilioni 56.6 mwaka uliotangulia.

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) lilipata mapato ya shilingi bilioni 24, lakini likapata hasara ya shilingi bilioni 27.7. Hali ilikuwa mbaya zaidi kwa Shirika la Posta Tanzania, ambalo limepata hasara ya shilingi bilioni 23.6.

Kwa ujumla, ripoti ya CAG ilionesha kuwa mashirika 58 kati ya 215 yalipata hasara kwa miaka miwili mfululizo (2021/2022 na 2022/2023). Mashirika haya yanapoteza mabilioni ya fedha za umma kila mwaka.

CAG alieleza kuwa sababu kubwa za hali hii ni 'uwepo wa changamoto za kiutendaji na kiungozi".

Udhaifu, maamuzi yasiyo na tija, na matumizi mabaya ya rasilimali inaweza kuwa msingi wa hoja ya CAG. Pia, mashirika haya yanabeba madeni makubwa. Kwa mfano, deni la jumla la mashirika ya umma hadi Juni 30, 2024 lilikuwa shilingi trilioni 7.23, ambapo mashirika ya umma yalikuwa na madeni ya trilioni 3.7.

Kadhalika kuna suala la weledi katika utendaji, kwani ripoti ya CAG inaonesha kuwa benki mbili za serikali; Benki ya Biashara (TCB) na na Benki ya Maendeleo-TIB zilitoa mikopo ya zaidi ya shilingi bilioni 200 lakini kwa dhamana zenye thamani ya shilingi bilioni 50.

"Hatua za haraka za kiusimamizi zinatakiwa kuchukuliwa, kuhakikisha Mashirika haya yanafikia viwango vya tija na ufanisi", anaweka bayana CAG, lakini je ni hatua gani hasa?

Hatua za kubadili hali hii

c

Chanzo cha picha, maelezo

Maelezo ya picha, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa akiteta na mtoto, mmoja wa abiria kwenye treni za kisasa za umeme (SGR). TRC liko kwenye hatua kubwa za mabadiliko, kuanzia Julai, 2024 lilipoanza safari zake za treni ya umeme hadi Novemba 2024, liliingiza Sh30bilioni. Likiongeza pia abiria kutoka 400,000 kwa mwaka hadi zaidi ya milioni 1 kwa kipindi kisichozidi nusu mwaka.

Swali la Getorare lilihitaji jibu la msingi: Ni lini hali hii itabadilika? Je, suluhisho lipo?

Kwanza, mashirika haya yanapaswa kuendeshwa kwa misingi ya biashara, lakini mara nyingi yamekuwa na uongozi wenye changamoto. Wataalamu wanapendekeza kuwa badala ya viongozi wa mashirika haya kuteuliwa kwa misingi ya kisiasa, waajiriwe kwa mchakato wa wazi na kwa vigezo vya kitaaluma.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sabatho Nyamsenda, anasema, "Uongozi uimarishwe, kwa kuleta watu ambao ni mahiri", Na kuongeza "Waende wakajifunze wenzao Wachina kwa mfano wachina makampuni yote yanayokuja hapa yanaendeshwa na serikali, waende wakajifunze Dubai".

Pili, mashirika haya lazima yajifunze kujiendesha kwa faida badala ya kutegemea ruzuku za serikali. ATCL, kwa mfano, inaweza kuanzisha mikakati ya ushirikiano na mashirika binafsi kama ilivyofanya Kenya Airways, ambayo sasa inaendeshwa kwa mfumo wa ubia na sekta binafsi.

x

Chanzo cha picha, ATCL

Maelezo ya picha, Licha ya kununuliwa ndege kadhaa katika miaka mitano iliyopita, ATCL imeendelea kupata hasara kila mwaka

Ethiopian Airlines, ambayo ni shirika la umma, imeweza kufanikisha operesheni zake kwa kuwa na usimamizi makini na mifumo ya uwajibikaji inayozingatia faida. Tanzania inaweza kujifunza kutoka kwao.

Badala ya mashirika haya kuendelea kuwa mzigo kwa serikali, yanaweza kushirikiana na sekta binafsi ili kupata mitaji na kuboresha huduma zao.

Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, alisema katika kongamano la Mwananchi Jukwaa la Fikra kuwa, "Tunategemea mashirika haya yaweze kuzalisha faida na kusaidia uchumi badala ya kuwa mzigo wa serikali."

Mchechu akaeleza kwa sasa mabadiliko na mageuzi katika Taasisi za umma, ikiwemo mashirika ya umma, hayaepukiki ili kuleta ufanisi.

Mashirika yanayopata faida

.

Chanzo cha picha, TPA

Maelezo ya picha, Rais Samia akiwa katika bandari ya Tanga, Machi 1, 2025 kukagua maboresho ya mradi wa gati mbili mpya za bandari hiyo. TPA kupitia usimamizi wa bandari zake nchini Tanzania, imetajwa kuingiza faida ya zaidi ya Sh100bilioni

Licha ya changamoto hizi, ripoti ya CAG inaonesha kuwa kuna mashirika yanayopata faida.

Kwa mfano, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) lilipata faida ya shilingi bilioni 248.75, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lilipata faida ya shilingi bilioni 242.9, na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ilipata faida ya shilingi bilioni 140.48.

Haya ni sehemu ya mashirika 31 yaliyopata faida katika mwaka wa fedha 2023/2024

Hii inaonesha kuwa, kwa usimamizi sahihi, mashirika ya umma yanaweza kuwa vyanzo vya mapato badala ya kuwa mizigo kwa serikali.

Je, hasara kwa Mashirika mengine ya umma itaendelea mpaka lini?

Kwa sasa, bado hakuna uhakika wa lini mashirika haya yatabadilika kutoka kwenye hasara kwenda kwenye faida. Lakini jambo moja ni wazi hatua madhubuti zinahitajika.

Katika miaka minne iliyopita serikali imeongeza kwa asilimia 27 uwekezaji wake katika Taasisi za umma yakiwemo mashirika haya, kuziwezesha kimtaji, hilo linaonesha dhamira ya kuleta mageuzi katika uendeshaji wa mashirika ya umma.

Katika kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wa taasisi za serikali ikiwemo Mashirika ya umma jijini Arusha hivi karibuni, Rais Samia Suluhu Hassan alisema, "Safari ya mageuzi kwenye mashirika ya umma inaendelea, tayari matokeo chanya yameanza kuonekana ikiwemo kuongezeka kwa mapato, kujiamini ndani ya mashirika na ubunifu wa watendaji'.

Getorare na Watanzania wengine wanaweza kupata jibu matokeo chanya anayotaja Rais Samia, yatakapokuwa kwa upana wake na kugusa mashirika yote ya umma. Naamini Getorare na wengine watachoka kuendelea kuuliza swali hili milele: Hasara mpaka lini?