Nini mwarobaini wa ‘madudu’ yaliyoibuliwa na CAG?

Chanzo cha picha, Ikulu
- Author, Walter Nguma
- Nafasi, Mchambuzi
Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali Dkt. Charles Kichere wiki hii alisoma taarifa ya ukaguzi mbele ya waandishi wa habari jijini Dodoma yalipo makao makuu ya nchi ya Tanzania.
Katika taarifa aliyoisoma aliibua mambo mengi ambayo yanaonesha upotevu mkubwa wa fedha za umma na baada ya kutoa taarifa hiyo ambayo iliwaacha wananchi mbalimbali midomo wazi huku wakijiuliza maswali mengi yasiyokuwa na majibu juu ya matumizi mabovu ya fedha za umma, upotevu mkubwa wa fedha za umma na ufisadi wa kimakusudi wa fedha za walipa kodi.
Maduhuli ya fedha zilizopotea kwa mujibu wa ripoti ya CAG
Katika ripoti iliyotolewa na CAG inaonesha fedha nyingi katika serikali kutumiwa pasipo ya kufuata utarartibu uliowekwa na serikali na hasara mbalimbali zimeonyesha maeneo mengi kuonekana kuwepo kwa kasoro hizo na baadhi ya maeneo hayo ni kama ifuatavyo;

Shirika la ndege la Tanzania(ATCL) limeendelea kuonekena kuwa linaendeshwa kwa hasara tokea kufufufliwa kwake, kwani kupitia ripoti ya CAG shirika la ndege la Tanzania kwa miaka mitano (5) limeendeshwa kwa hasara zaidi ya bilioni 153.542.
Huku ikiwa kwa mwaka 2019/2020 shirika hilo likiendeshwa zaidi ya hasara ya bilioni 60.
CAG ameongeza kuwa shirika la ndege Tanzania katika bodi yake ya wakurugenzi hakuna mtaalamu hata mmoja wa masuala ya anga.
Mradi wa reli ya kisasa(SGR) unaojengwa unaonekana kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya bilioni 35 kutokana na kuwa na wafanyakazi zaidi ya 1538 katika mradi huo kutoka nje ya nchi na wote hawana vibali.
Hivyo imeonekana kati ya wafanyakazi 2,408 kati yao 1538 ni raia wa kigeni wasiokuwa na vibali vya kufanya kazi Tanzania.

Sekta muhimu katika uchumi wa Tanzania ambayo ni sekta ya utalii imeonyesha kupitia ripoti ya CAG kuwa kumekuwa na upotevu mkubwa wa fedha hasa kwa kufanya malipo yasiyozingatia taratibu zilizowekwa na serikali.
Katika ripoti hiyo aliyekuwa waziri wa wizara hiyo DKT. Kigwangwala ametajwa na CAG moja kwa moja kuwa mshirika mkubwa wa upotevu wa fedha hizo.

CAG ameonyesha kuwa kuna ubadhilifu mkubwa wa fedha za umma katika bandari ya Dar es salaam ambapo hatua kadhaa tayari zimekwisha kuchukuliwa ambapo aliyekuwa Mkurugenzi mtendaji wa bandari aliweza kusimamishwa na Rais wa Tanzania ili kupisha uchunguzi wa ufisadi wa zaidi ya bilioni 3.7 lakini CAG ameeleza kuwa bado kuna majnaga makubwa ya ubadhirifu wa mabilioni ya fedha na uchunguzi bado unaendelea.
Makusanyo kupitia ripoti ya CAG imeonyesha kuwa zaidi ya makusanyo bilioni 18 katika wilaya 135 hazikupita benki na hivyo fedha hizi kuna uwezekano zimeingia kwenye mifuko ya watu wenye nafasi serikalini.
Madai ya watumishi; ripoti inaonesha kuwa kuna madai ya zaidi ya bilioni 331.52 ya watumishi katika taasisi 80 za serikali kuu.
Maswali magumu ya kujiuliza kupitia Ripoti ya CAG
- Waziri wa fedha alikuwa wapi wakati wa upotevu wa fedha hizi?
- Ni hatua gani zilichukuliwa kwa wabadhirifu hawa kupitia vyombo vya kupambana na rushwa na ufisadi kama TAKUKURU?
- Makatibu wakuu wa wizara ukianza na wizara ya fedha na wahasibu wakuu wa wizara hizi walifanya nini katika madudu haya yaliyoainishwa na CAG kwenye ripoti yake?
- Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliwahi kusema kwenye utawala wake hakutakuwa na upotevu wa fedha za umma. Je kwenye hili nani amfunge paka kengele?
- Ni nani wakumwamini hivi sasa katika usimamizi wa fedha za umma dhidi ya ubadhilifu na ufisadi?
Nini mwarobaini wa 'madudu' yaliyoibuliwa na CAG
Viongozi waliotajwa katika ripoti ya CAG mara moja wasimamishwe kazi, wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo husika husussani kwenye mahakama ya ufisadi na pale watakapo bainika kuwa wameshiriki katika upotevu wa fedha hizi basi hatua kali za kisheria zichukuliwa juu yao na mali wanazomiliki ili lipate kuwa somo na fundisho kwa viongozi wote.
Kuundwe tume maalumu zitakazo chunguza mapungufu yote yaliyopo katika miradi mikubwa inayonedelea hivi sasa kama vile SGR, ATCL, Bwawa la kufua umeme ili kuweza kuzuia upotevu wa fedha za serikali.
Sheria za manunuzi katika serikali nalo ni jambo jingine lakutizama upya kwani kunaonekana kuna mianya mingi ya kufanya ufisadi kupitia sheria za manunuzi tulizonazo hivi sasa.
Maboresho ya haraka katika taasisi za kiserikali; kwa ripoti ya CAG ni dhahiri kabisa kwamba taasisi za kiserikali haziko imara kiasi kwamba kuna kuwa na upotevu mkubwa wa fedha.
Mfano ni shirika la ndege (ATCL) kutokuwepo na mtaalam wa masuala ya anga .
Tanzania ikiweza kuwa na taasisi imara tutazuia ufisadi na upotevu mkubwa wa fedha, unaonekana hivi sasa kupitia taasisi hizi.
Kutokuwapa nafasi za uongozi, wala kugombea watu wote wanaokuwa wanahusishwa na upotovu wa fedha za umma.
Hili litasaidia kurudisha nidhamu katika matumizi na manunuzi kupitia fedha za umma.

Mifumo ya ukusanyaji wa mapato lazima kutizamwa upya hasa hasa katika ngazi za wilaya, manispaa na halmashauri, kwani huku kunaonekana kuwepo na ubadhinifu mkubwa wa fedha za watanzania walipa kodi.
Ripoti ya CAG inaonyesha kuna upotevu wa bilioni 18 kupitia ngazi ya wilaya na kuna uwezekano upotevu huo ukawa mkubwa zaidi kwa namna hiyo mfumo wa ukusanyaji wa mapato ni wakutizama upya kabisa katika ngazi hizo.
Kuruhusu vyombo vya habari kufanya kazi zake kwa uhuru bila kuzuiwa kwani hili litamsaidia hata rais kuweza kuona matendo maovu au njama za kifisadi dhidi ya mali za umma. Tukumbuke jinsi ESCROW na RICHMOND ambavyo vyombo vya habari viliibua mambo mengi na kusaidia serikali kukabiliana na tatizo hilo.
Mikataba yote ya serikali ipitishwe sheria kuwa ipelekwa bungeni kwanza na kujadiliwa kabla ya kusainiwa. Hii itazuia nia ovu ya watendaji wakuu wa kiserikali kufanya ufisadi na kuwa na mikataba mibovu yenye kuingizia taifa hasara.
Kwa kupitia ripoti ya CAG ni muhimu kwa Rais kuchunguza kwa kina watu anaowateua kushika nyadhifa mbalimbali serikalini kwani wengi wao ni hawa wanaohusishwa kwa namna moja ama nyingine na upotevu huu mkubwa wa fedha za umma.
Hivyo ni vyema kuangalia sifa ya ziada kuliko kuangalia tu uzoefu pamoja na viwango vya elimu.
Sasa kwa kuangalia atizame sana uadilifu wa mtu anayemteua kushika nyadhifa fulani serikalini ili kuweza kepukana na madadu kama haya yanayoonekana katika ripoti ya CAG ya 2019/2020.














