Mashirika ya kimataifa yenye mabilioni ya dola yaliyonaswa nchini Urusi

Chanzo cha picha, Getty Images
Vita vya Ukraine vilipoanza mnamo Februari 2022, kampuni nyingi za Magharibi zinazofanya kazi nchini Urusi ziliondoka nchini.
Zingine, hata hivyo zilendelea na shughuli zao.
Wale walioamua kuendelea kuhudumu nchini Urusi wamepata "faida ya mabilioni ya dola" kulingana na utafiti wa Kituo cha Uchumi cha Kiev (KSE).
Lakini, uchunguzi unaonyesha, Kremlin inawazuia ku pesa hizo kama njia ya kuweka shinikizo kwa mataifa yanayochukuliwa kuwa "uhasama."
Makadirio ya kituo cha utafiti ni kwamba karibu makampuni 700 kutoka nchi zisizofungamana na Moscow zilipata faida ya karibu dola milioni 20,375 za Kimarekani mwaka 2022, kiasi ambacho ni kikubwa kuliko faida walizopata kabla ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Faida kubwa ambayo imegeuka kuwa upanga wenye makali pande zote mbili kwa sababu fedha zimezuiwa.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Makampuni mengi ya Magharibi yalisubiri kwa muda mrefu sana kuondoka Urusi na, wakati huo, mamlaka ilifanya kila linalowezekana kupunguza idadi ya kampuni zilizokuwa zikifunganya virago," naibu mkurugenzi wa maendeleo wa KSE, Andrii Onopriienko, anaiambia BBC Mundo.
Kampuni nyingi ambazo faida zake zimefungiwa nchini Urusi ziko Marekani, Ujerumani, Austria na Uswizi, kulingana na data ya KSE.
"Kumi bora" katika orodha hiyo inaongozwa na kampuni za Raiffeisen, Philip Morris, Pepsi, Japan Tobacco International na Automobile.
Nafasi hiyo inakamilishwa na Mars, Mondelez, KIA Motors, Imperial Energy Corporation na Procter & Gamble.
"Kila kitu kilichopatikana nchini Urusi kitabaki huko, kwa kuwa mamlaka haitaruhusu kurejeshwa kwa gawio na itataifisha mali inayovutia zaidi," anaongeza mtafiti wa Kiukreni.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Moscow inachukulia hatua za kibiashara kama vile kufungia fedha za kampuni hizo kuwa za halali ikizingatiwa kwamba nchi zinazofungamana na Magharibi zimeiwekea Urusi vikwazo vya kiuchumi na kuzuia mali na fedha za watu binafsi na makampuni ya Kirusi nje ya nchi.
Majaribio ya nchi za Magharibi kuadhibu na kuitenga Urusi kifedha kwa ajili ya uvamizi wa Ukraine ni “mazoezi yasiyo halali ya vikwazo na kufungia kinyume cha sheria mali ya mataifa huru, ambayo kimsingi ina maana kwamba wanapuuza kanuni na sheria zote za msingi za biashara huria, ”Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema mwezi Agosti.
Marekani na washirika wake wamezuia uagizaji wao wa mafuta na gesi ya Urusi ili kupunguza mapato ya Moscow na kudhoofisha juhudi zake za vita.
Katika hatua zingine zilizochukuliwa kulemaza uchumi wa Kremlin, nchi za Magharibi zilizuia mabilioni ya dola za akiba ya kigeni ya Benki Kuu ya Urusi, huku zikizuia mashirika ya Urusi kufikia masoko makubwa ya mitaji na kukata muunganisho wa benki kubwa zaidi za nchi katika mfumo wa malipo wa kimataifa wa SWIFT.
Wengine walioongezwa kwenye orodha hiyo ni mamia ya wafanyabiashara mashuhuri wa Urusi ambao fedha na mali zao zilikamatwa.
Akikabiliwa na vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Urusi muda mfupi baada ya vita kuanza, Putin alisema kwamba mpango wa kujaribu kudhoofisha uchumi wa Urusi ulikuwa sawa na "tangazo la vita."

Chanzo cha picha, Getty Images
Pesa kama "mateka"
"Vikwazo vilinasa mabilioni kutoka Urusi katika nchi za Magharibi na Putin alijibu kwa njia sawia na hiyo. "Alishikilia mateka pesa zote za Magharibi ambazo angeweza kupata," anaelezea Alexey Kalmykov, mwandishi wa habari za uchumi wa BBC Idhaa ya Kirusi.
"Sasa haiwezekani kutoa fesha hizo nchini Urusi," anasema.
Kalmykov anasema kuwa makampuni ya Ulaya na Marekani sasa yanakabiliwa na chaguo gumu: kuendelea kutengeneza pesa nchini Urusi bila hakikisho lolote kwamba wataweza kurejesha faida, au kuondoka Urusi, lakini kwa masharti ya Kremlin.
Masharti hayo ni pamoja na kuuza mali zake kwa bei iliyowekwa na mamlaka , kukubali punguzo la angalau asilimia 50 na kutoa mchango wa ziada wa asilimia 10 "kwa hiari" kwa bajeti ya vita vya Urusi.
"Haishangazi kwamba kuondoka Urusi ni dhamira isiyowezekana kwa kampuni za Magharibi," Kalmykov anasema.
“Angalia Heineken. Kampuni kubwa ya kutengeneza pombe ya Uholanzi hivi majuzi iliuza biashara yake nchini kwa mnunuzi wa Urusi kwa karibu dola moja,” anaongeza.
Makampuni kutoka nchi "hasimu"

Chanzo cha picha, Getty Images
Urusi imebuni msururu wa kanuni katika miezi ya hivi karibuni ili kuzuia mali ya makampuni ya Magharibi kulipiza kisasi hatua kukamatwa kwa mali inayomilikiwa na Warusi nje ya nchi.
Kufikia lengo hilo katika baadhi ya matukio, kuna wakati Kremlin ilichukua udhibiti wa hisa za kampuni ya kutengeneza pombe ya Denmark Carlsberg katika kampuni ya Kirusi, pamoja na kampuni tanzu ya Danone ya Ufaransa inayotengeza mtindi nchini Urusi.
Hatua sawia na hiyo pia ilichukuliwa dhidi ya kampuni ua Kifini Fortum na Uniper ya Ujerumani.
Mnamo Agosti Putin alitia saini sheria ya kupiga marufuku wawekezaji wa kigeni kutoka nchi "hasimu" kushikilia hisa katika makampuni makubwa ya Kirusi na benki, kuweka mipaka mipya ya uendeshaji wa kigeni katika taifa hilo.
Sheria haibani tu mipaka ya haki za wawekezaji kutoka kwa mataifa ambayo hayajajiunga na Moscow, lakini pia inasema hisa zao zinaweza kusambazwa kwa uwiano kati ya wamiliki wa Kirusi wa kampuni husika.
Kwa vile Kremlin imeongeza vikwazo kwa mashirika ya kimataifa yanayojaribu kuondoka nchini kwa kuuza kampuni zao tanzu za Urusi, mashirika mengi makubwa ambayo yaliamua kusalia Urusi baada ya vita sasa yanakabiliwa na uwezekano wa kupata hasara ya mamilioni ambayo inaweza kuathiri sana biashara zao. Jambo ambalo pengine hawakutarajia walipoamua kubaki katika soko la Urusi licha ya vita.

Chanzo cha picha, Getty Images
Bado haijajulikana kwa sasa watawezaje kurejesha faida zao na jinsi watakavyoweza kuondoka katika nchi ambayo imewaacha katika njia panda.












