Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wanajeshi wa Urusi waliiambia BBC: 'Tulishuhudia wenzetu wakiuawa kwa amri ya makamanda wetu'
- Author, Ben Steel, Mike Radford, George Wright
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 8
Onyo: Taarifa hii ina maelezo ya vurugu iliyokithiri na marejeleo ya kujiua.
Wanajeshi wanne wa Urusi wameeleza kwa kina hali ya ukatili na mateso waliyoishuhudia katika mstari wa mbele wa vita nchini Ukraine. Wawili kati yao walithibitishia BBC kuwa waliona wanajeshi wakipigwa risasi na kuuawa papo hapo kwa sababu ya kukataa kutekeleza amri za kijeshi.
Mmoja wao aliiambia timu ya watayarishaji wa makala ya BBC kwamba alimwona mwanajeshi akiuawa kwa amri ya kamanda wake, kamanda ambaye baadaye alitunukiwa cheo cha "Shujaa wa Urusi" mwaka 2024.
Mwanajeshi mwingine kutoka kikosi tofauti alieleza kuwa alimwona kamanda wake akiwapiga risasi watu wanne kwa mikono yake mwenyewe.
"Niliwajua," alisema. "Nakumbuka mmoja wao akipaza sauti: 'Usinipige risasi, nitafanya chochote utakachosema!'"
Mtu mwingine alisimulia kuwa aliona miili ya wanajeshi wenzake ishirini ikiwa imetupwa kwenye shimo baada ya "kuondolewa", neno la msimu wa kijeshi wa Urusi linalomaanisha kumuua mwanajeshi mwenzako.
Katika makala ya televisheni Zero Line: Inside the Russian War, wanaume hao wanasimulia kwa maelezo ya kutisha jinsi walivyoteswa kwa kukataa kushiriki mashambulizi waliyoyafananisha na operesheni za kujiua.
Jeshi la Urusi hurejelea mashambulizi hayo kama "meat storms", yaani, mawimbi ya wanajeshi yanayotumwa kuvuka mstari wa mbele bila kukoma kwa lengo la kuichosha na kuipunguza nguvu adui.
Kwa mujibu wa BBC, hii ni mara ya kwanza kwa wanajeshi wa Urusi walioko mstari wa mbele kutoa ushuhuda rasmi kuhusu makamanda kuamuru wanajeshi wao wenyewe wauwawe.
Mmoja wa mashuhuda alikuwa na jukumu la kutambua na kuhesabu miili ya waliokufa. Alitoa orodha zinazoonyesha kuwa yeye ndiye pekee aliyesalia hai kati ya wanaume 79 waliosajiliwa pamoja naye.
Anasema aliteswa na kudhalilishwa, hata kukojolewa kwa sababu alikataa kwenda mstari wa mbele. Wengine waliokataa walipigwa na mshtuko wa umeme, kunyimwa chakula, kisha kulazimishwa kushiriki mashambulizi hayo bila silaha.
Wanaume hao wanne, ambao baadaye walikimbia jeshi la Urusi, walitoa ushuhuda wao kutoka eneo lisilotajwa nje ya Urusi.
Ndani ya Urusi, karibu aina zote za upinzani wa wazi dhidi ya uvamizi wa Ukraine ulioanzishwa na Rais Vladimir Putin zimezuiwa.
Serikali ya Moscow haitoi takwimu rasmi za waliokufa au kujeruhiwa, lakini Wizara ya Ulinzi ya Uingereza inakadiria kuwa zaidi ya wanajeshi milioni 1.2 wa Urusi wameuawa au kujeruhiwa tangu kuanza kwa uvamizi mkubwa wa Ukraine mwezi Februari, 2012.
Serikali ya Urusi inasema kuwa wanajeshi wao wanaendesha operesheni kwa uangalifu katika mazingira ya mapigano makali. Pia wanadai kuwa ''wanachunguza madai ya ukiukwaji wa sheria ipasavyo''.
Alisema: "Hatuwezi kuthibitisha kwa kujitegemea usahihi au uhalali wa maelezo uliyotoa."
Hata hivyo, ushuhuda wa kina wa wanaume hao unaongeza uzito kwa ripoti zinazoonyesha vitendo vya ukatili na ukiukwaji wa haki za binadamu kwenye mstari wa mbele wa Urusi.
Ilya, aliyekuwa na jukumu la kuhesabu miili ya waliokufa, ni miongoni mwa waliodai kushuhudia wenzao wakiuawa kwa amri ya makamanda.
Kabla ya vita, Ilya mwenye umri wa miaka 35 alikuwa mwalimu wa watoto wenye mahitaji maalum na tawahudi katika mji wa Kungur, katika Milima ya Ural. Mwezi Mei 2024, polisi walivamia nyumba ya wazazi wake na kumjulisha kuwa ameandikishwa jeshini.
Anasema aliandikishwa pamoja na wanaume wengine 78 katika kituo cha usajili mjini Perm.
"Karibu wote walikuwa wamelewa," alisema. "Walikuwa wakipiga kelele: 'Twende vitani! Tutamkamata Zelensky na kupandisha bendera yetu!' Nilijiuliza: Nimefikaje hapa? Nilikuwa na hofu kubwa."
Walipowasili Ukraine, wengi walipelekwa moja kwa moja mstari wa mbele.
Ilya hakutaka kushiriki katika mapigano, hivyo akawekwa katika kituo cha amri. Hata hivyo, anasema alishuhudia watu wanne wakipigwa risasi kwa umbali wa karibu sana kwa sababu walikimbia mstari wa mbele na kukataa kurudi.
"Cha kusikitisha ni kwamba niliwajua," alisema. "Mmoja alipiga kelele: 'Usinipige risasi, nitafanya chochote!' Lakini kamanda aliendelea kuwalenga."
Wanaume hao walituambia kwamba kupiga mbinja kwa kawaida hufanywa kama adhabu kwa kukataa maagizo, na hutumiwa kama njia ya kuwatisha wengine ambao wanaweza kufikiria kufanya jambo lile lile.
Eliya asema: "Hatima yako imeshikamana na kamanda wako. Kamanda anatoa amri kupitia redio: 'Mpigeni mbinja huyu (askari), mpige yule.'"
Unyongaji wa askari ambao walikataa maagizo haukuwa mdogo kwa kitengo cha Ilya.
Dima anasema: "Kwa kweli wanaua wanaume wao, ni kawaida."
Kabla ya vita, Dima, 34, aliishi na mkewe na binti yake na alifanya kazi huko Moscow kama fundi wa kurekebisha mashine za kuosha vyombo.
Mwaka 2022, polisi walimwambia kuwa asipojiunga na jeshi angefungwa gerezani.
Hakutaka kumuua mtu yeyote, hivyo alijiunga na kikosi cha wahudumu wa afya. Baadaye alihamishiwa katika Brigade ya 25, ambako anasema alishuhudia wanajeshi wakinyongwa kwa amri ya kamanda wao.
"Niliona kwa macho yangu mwenyewe, umbali wa mita mbili au tatu tu. Sauti za risasi. Hii si filamu; ni maisha halisi," alisema.
Kamanda wake Alexei Ksenovonov alitunukiwa Nishani ya Nyota ya Dhahabu na kutangazwa "Shujaa wa Urusi" mwaka 2024. Hata hivyo, familia za waliouawa zilimwandikia Rais Putin zikidai uchunguzi wa madai ya ukatili katika kikosi hicho.
Barua hiyo ilisema: "Waliilinda nchi yetu kwa heshima na fahari! Lakini kwa kweli, walijipata miongoni mwa genge la viongozi hawa, ambao walipokea medali kwa gharama ya makumi ya maelfu ya waliokufa na kupotea!"
"Na wanaendelea kuwaangamiza wanaume wetu! Na wanahisi wako juu ya kuwajibishwa!"
Dima alimwelezea kamanda wake kama "mchinjaji".
"Anatoa amri nyingi za kuua askari, na mikono yake ina damu nyingi sana.''
Alisema pia aliona miili ya wanaume ishirini, waliokuwa wamefika kambini usiku uliotangulia, ikiwa imetupwa mtaroni baada ya kupigwa risasi.
Anasema alizungumza na baadhi yao, wote waliokuwa wafungwa, kabla ya kushuhudia wakichukuliwa asubuhi iliyofuata.
Akiwa daktari, Dima alijulishwa mara kwa mara juu ya vifo hivyo, na anasema aliambiwa kuwa watu hao walipigwa risasi na kamanda mmoja, na kadi zao za benki ziliibiwa.
"Vijana ishirini waliletwa kwetu. Walichukua kadi zao za benki na kuwaua," anakumbuka. "Sio ngumu kumuondoa mtu. Tengeneza ripoti tu."
Dima anasema alifahamishwa kuwa viongozi hao ndio walionyakua kadi za benki za waliouawa.
Filamu ya BBC pia inajumuisha ushuhuda kutoka kwa mpiganaji mwingine wa zamani, afisa wa ngazi ya juu, ambaye anasema alihudumu katika jeshi la Urusi kwa miaka 17. Afisa huyo wa zamani, ambaye hatutafichua jina lake, anasema alizungumza na mwanamume aliyesaidia kuua kundi la maafisa wa ngazi za juu.
Afisa huyo wa zamani anakumbuka kwamba mwanamume huyo alisema alikuwa sehemu ya "kikosi cha kufilisi kilichotumwa kuwaangamiza manusura wowote."
Anaongeza: "Sijawahi kuona jambo kama hili katika miaka yangu yote ya utumishi."
Wanaume hao wanne walisimulia kwa undani sana operesheni za kutisha za "Meat storm", sehemu ya mbinu ya "kusagia nyama" iliyotumiwa na jeshi la Urusi kwenye uwanja wa vita wa Ukraine.
Misheni hizi ni mbaya sana hivi kwamba zinafanana na misheni ya kujiua.
Mwanajeshi mwingine wa zamani, aitwaye Dennis, anasema: "Niliwaona (makamanda) wakituma wimbi baada ya wimbi, wakiwarusha watu kama ng'ombe kwa Waukraine, hadi wakaishiwa na risasi na ndege zisizo na rubani, ili wimbi jingine liweze kufikia lengo lake."
Kulingana na Wizara ya Ulinzi ya Uingereza, wastani wa Warusi 900 hadi 1500 waliuawa au kujeruhiwa kila siku nchini Ukraine wakati wa 2025.
Wanaume hao pia walieleza kwa kina operesheni za "meat storms," walizozifananisha na misheni za kujiua.
Dima anaelezea jinsi misheni hizi zinavyotekelezwa kwa vitendo.
"Tuma watatu, kisha watatu wengine," Dima alieleza. "Ikishindikana, tuma kumi. Ikishindikana tena, tuma hamsini. Mwisho tutapenya ulinzi wao, hayo ndio mantiki ya jeshi."
Anasema: "Tulipoteza wanaume 200 kwa siku tatu.
Katika misheni ya kwanza ya 'meat storm' iliyozinduliwa na jeshi letu, tulishindwa, jeshi letu liliharibiwa kwa siku tatu tu."
Dima kisha anaonyesha video, iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii mnamo Oktoba 2023, ya akina mama na wake za wanaume waliouawa katika kitengo chake, ikizungumzia hasara kubwa.
Mwanamke mmoja anasikika akisema, "Vikosi vyetu viliamriwa kusonga mbele wakiwa na bunduki na pikipiki pekee." Mwingine anasema, "Hasara ni nzito. Wanaume wetu wanachinjwa."
Waliokataa kushiriki waliteswa vikali.
Video iliyochapishwa kwenye programu ya Telegram inaonyesha wanaume kutoka kikosi chake wakiwa Panteleimonivka, katika eneo la Donetsk.
Mmoja wao anasema, "Twende tukawalishwe wanyama," kabla ya kuinua kifuniko na kufichua wanaume watatu waliokuwa wamejikunja ndani ya shimo.
"Mna njaa?" "Mnataka kula?" aliuliza mwanaume aliyekuwa akirekodi, kisha mmoja wa waliokuwa shimoni akainua kichwa chake na kutikisa kwa kukubali, huku akinyosha mikono yake wakati nafaka kavu zikimwagiwa ndani ya shimo.
"Angalieni jinsi anavyokula," alisema yule aliyekuwa akipiga picha, wakati mwanaume aliyekuwa shimoni akila nafaka hizo.
Elijah anasema baadhi ya wanaume walinyimwa chakula kwa siku kadhaa na kupigwa mshtuko wa umeme kabla ya kutumwa kwenye operesheni za "meat storms" bila silaha.
Anasema yeye mwenyewe aliteswa baada ya kukataa kushiriki katika moja ya operesheni hizo.
"Walinifunga kwenye mti, wakanipiga mara mbili kwa rungu, na wakaweka bunduki kichwani mwangu."
"Sijui nielezeje, walinikojoea. Kiongozi aliwaambia wote: 'Tumepata choo kipya.' Nilifungwa kwa nusu siku."
Baada ya kufunguliwa kutoka kwenye vifungo vyake, Ilya alijaribu kujiua.
Dennis, anayesema kuwa hapo awali aliwahi kuwaletea kwa siri chakula na maji wanajeshi waliokuwa shimoni, aliwaonyesha watayarishaji wa makala hiyo video iliyodaiwa kuonyesha mwanajeshi aliyeshutumiwa kwa kutoroka jeshini akikojoewa. Hata hivyo, BBC haikuweza kuthibitisha kwa uhuru uhalisi wa video hiyo.
Anasema: "Huu ni ukiukwaji wa heshima na utu wa binadamu. Katika jeshi la Urusi, jambo hili limekuwa la kawaida."
Anaongeza: "Ni kinyume cha sheria, lakini hakuna anayeadhibiwa kwa kufanya hivyo. Kinyume chake, wanajeshi wanahamasishwa kufanya vitendo hivyo."
Dennis, mwenye umri wa miaka 27, pia alionyesha picha aliyosema ilipigwa muda mfupi baada ya meno yake mawili ya mbele kung'olewa na mmoja wa wakuu wake, kwa sababu aliwaambia kwamba alikataa kutafuta ndege isiyo na rubani (droni) iliyopotea.
Anasema: "Ni jambo la kutisha. Sikuwa na chaguo jingine ila kuendelea."
Baadaye, Dima alipandishwa cheo, licha ya kuwa awali alikuwa amesema hataki kuwa afisa. Picha ya hafla ya kupandishwa cheo kwake ilionyeshwa.
Baada ya kupandishwa cheo, anasema alikataa kuwatuma watu wake kushiriki katika operesheni ya "Meatstorm".
"Nilikaa imara na kukataa. Sikulazimika kujitokeza mwenyewe, lakini sikuweza kuwapa amri hiyo," alisema.
Dima anasema hatua hiyo ilisababisha akamatwe na polisi wa kijeshi na kupelekwa Zaitsev, gereza la muda.
"Huko, walinitesa kwa kunipiga mshtuko wa umeme," anakumbuka, akiongeza kuwa mshtuko wa kwanza ulikuwa mkali kiasi cha kujisaidia haja kubwa bila kukusudia.
Anasema aliteswa kila siku kwa muda wa siku 72.
"Ni mateso tu, kila siku, bila hisia zozote usoni mwao. Ni kama wazimu," alisema, akiwaonyesha waliomtesa.
Sasa wote wako nje ya Urusi, lakini wanasema bado wanateseka kisaikolojia kutokana na waliyopitia.
"Katika ndoto zangu naona msitu uliojaa maiti," Dima alisema. "Harufu yake si harufu tu, ni kama ladha."
Ilya alisema anaipenda nchi yake, "lakini si kile Putin ameifanya."
"Wanaweza kumvunja mtu yeyote huko," alisema. "Karibu wanivunje pia, lakini hawakufaulu."
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid