Mambo Matano aliyofichua Papa Francis katika chapisho kuhusu maisha yake

..

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Tarehe 13 Machi 2025, Jorge Bergoglio anasherehekea miaka 12 tangu alipochaguliwa kuwa Papa Francis.
Muda wa kusoma: Dakika 8

Jorge Mario Bergoglio si tu Papa wa kwanza kutoka Latini Amerika, bali pia Papa wa kwanza tangu karne ya 15 kuchapisha kitabu cha kumbukumbu ya maisha yake akiwa madarakani.

Kwa kweli, Hope: The Autobiography -chapisho lililokusudiwa kutolewa baada ya kifo chake, lakini Papa Francis aliamua kulitoa Januari hii.

Wiki chache baadaye, Papa Francis alilazwa hospitalini katika Hospitali ya Gemelli mjini Roma kufuatia maambukizi ya mfumo wa upumuaji yaliyosababisha matatizo mengine ya kiafya.

Ingawa bado yuko hospitalini, Alhamisi hii anasherehekea miaka 12 ya uongozi wake kama Papa akiwa katika hali nzuri ya afya.

Uchunguzi wa hivi karibuni wa picha ya kifua pia umeonyesha kuimarika kwa hali yake ya afya.

"Chapisho kama hili si letu binafsi, bali ni begi letu la safari. Na kumbukumbu si tu kile tunachokikumbuka, bali pia kile kinachotuzunguka," anasema Francisco katika kitabu chake.

Andiko hili linatokana na mazungumzo ya zaidi ya miaka sita kati ya Papa Francis na mwandishi wa habari wa Italia, Carlo Musso.

Ambapo, anaelezea kumbukumbu za ujana wake huko Buenos Aires, tafakari zake kuhusu mada kama uhamiaji, na kuelezea maisha yake kama Papa.

"Katika kila ukurasa, katika kila hatua, pia kuna kitabu cha wale walionitembelea, wale waliotangulia, na wale watakaotufuata," anaongeza.

Hizi ni baadhi ya hadithi na tafakari muhimu kutoka katika chapisho lake lililoitwa Hope.

1. "Kuzama kwa meli."

Hadithi ya Francisco inaanza na kuzama kwa meli.

Miaka tisa kabla ya kuzaliwa kwake, tarehe 11 Oktoba 1927, baba yake, Mario José Bergoglio, alinunua tiketi za kusafiri kutoka Genoa hadi Buenos Aires pamoja na wazazi wake kwa meli.

Lakini siku hiyo, Mario na familia yake hawakuweza kupanda meli hiyo.

Hawakuweza kuuza samani za nyumba waliyoiacha ili kuhamia nchi nyingine kwa wakati. Hivyo basi, familia ya Bergoglio iliamua kurudisha tiketi na kuahirisha safari yao kwenda Argentina.

Baada ya siku chache, wakati familia ya Bergoglio ikiwa bado nchini Italia, meli kubwa ya Principessa Mafalda ilipigwa na radi katika Bahari ya Atlantiki, na ajali hiyo ilisababisha meli kuzama.

Janga hilo lilisababisha takriban watu 300 kufariki dunia, kulingana na simulizi ya Papa.

"Hivyo ndivyo nilivyokuwa hapa sasa," anasema akitafakari namna baba yake alivyonusurika kwa kutopanda meli hiyo.

..

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Meli nyingi za wahamiaji zilifanya safari kutoka Italia hadi Argentina katika kipindi cha miaka ya 1950.

Hatimaye, miaka miwili baadaye, baba ya Bergoglio alifika Buenos Aires, ambapo walisajiliwa kama "wahamiaji kutoka ng'ambo."

"Hii si hadithi mpya; ni kama ya jana vile vile kama ilivyo ya leo," Francisco anasema sababu ambazo, kama ilivyokuwa mwanzoni mwa karne ya 1900 na leo, zinawaongoza maelfu ya watu kuondoka katika nchi zao kutafuta maisha bora.

Ndiyo maana, baada ya miaka mingi, katika safari yake ya kwanza akiwa Papa nje ya Vatican, Francis alitembelea Lampedusa, kisiwa kilichopo Bahari ya Mediterania ambacho kimekuwa ishara ya uhamiaji.

Kwa maoni yake, "ni jambo la dharura kuchukua hatua za kuhakikisha haki ya uhamiaji."

2. Kura ya ziada

Francisco hakutarajia kuchaguliwa kuwa kiongozi mkuu wa kiroho wa Kanisa Katoliki mwaka 2013.

Aliamini kwamba kama kardinali kutoka Latini Amerika, angeweza kusaidia kushawishi baadhi ya kura kati ya majina ya warithi wanaoweza kupewa nafasi wakati huo.

"Kusema kwamba sikuwa na matarajio yoyote kama hayo, maishani mwangu, na hasa mwanzoni mwa mchakato huo ni mawazo finyu," anasema.

Hata hivyo, kwa kuangalia nyuma, mabadiliko yaliyokuwa yakifanyika Vatican yanaweza kuwa yalionyesha kile kilichokuja kutokea.

Katika mkutano wa kabla ya upigaji kura, Mkatoliki huyu kutoka Argentina aliguswa na shangwe aliyoipokea baada ya kutoa hotuba fupi na ambayo haikuandaliwa kabla.

"Sawa, tunahitaji mtu wa kufanya mambo hayo," mmoja wa makardinali alimuambia baada ya kumsikiliza.

"Ndiyo, lakini unampata wapi?" Bergoglio alijibu.

–Kwako.

–Hahaha! Ndiyo, sawa, sawa, endelea, tutaonana baadaye.

Papa alichukulia maoni hayo kama utani.

..

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Baraza la makadinali huchagua Papa mpya kuongoza kanisa katoliki duniani

Baraza la makadinali lilianza tarehe 12 Machi, 2013.

Bergoglio alifika Santa Marta akiwa na begi lililokuwa na mavazi mawili tu na kidogo kingine.

Aliacha mali zake nyingine zote Buenos Aires, mji ambao hakurudi tena baada ya kuchaguliwa kuwa Papa.

Usiku wa kwanza wa baraza hilo ulimalizika bila muafaka.

Asubuhi ya tarehe 13 Machi, kura ya pili na ya tatu zilifanyika bila mafanikio, ambapo hakuna mgombea alifanikiwa kupata idadi ya kura 77 kati ya 115 zinazohitajika.

Katikati ya mapumziko kabla ya kura ya tano, kardinali mmoja kutoka Latini Amerika alimuambia Bergoglio:

–Je, umeandaa hotuba yako? Iandaae vizuri.

"Unazungumzia hotuba gani?" Bergoglio aliuliza.

"Hotuba ambayo utatoa!" alijibu kadinali, akimrejelea hotuba ya kwanza ya Papa mpya.

"Huu ni utani mwingine?" Bergoglio alijiuliza mwenyewe, akiwa haelewi kinachoendelea.

Katika duru ya nne ya upigaji kura, Mkatoliki huyu kutoka Argentina alipokea kura 69. Lakini hiyo haikutosha.

...

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Francisco alitoa hotuba yake ya kwanza kwenye madhabahu kuu ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro.

Duru ya tano ya upigaji kura ilileta jambo ambalo halikutarajiwa: kulikuwa na kura ya ziada. Mtu mmoja alikuwa ameunganishia vipande viwili vya kadi, hivyo ilibidi wachome yote na kurudia mchakato.

Ilikuwa katika duru hiyo ya pili ya upigaji kura ambapo jina la Bergoglio lilisikika zaidi ya mara 77.

"Sijui hasa ni kura ngapi zilikuwa mwishoni; sikuweza kuzisikia tena; kelele zilifunika sauti ya kiongozi," anasema Francisco.

"Je, unakubali uchaguzi wa Papa Mkuu?" Kardinali Re alimuuliza.

"Ninakubali," Bergoglio alijibu.

Miaka kumi na miwili baadaye anakiri: "Nilihisi amani, utulivu."

Walijaza chetezo na moshi mweupe ulifuka, ukipanda kutoka kwenye Kanisa la Sistine huku usiku ukiingia.

3. Sanduku jeupe

Uchaguzi wa Bergoglio ulifanyika baada ya kujiuzulu kwa Papa Benedict XVI, Papa wa kwanza katika karne karibu 600 kujiondoa madarakani kutokana na matatizo ya kiafya.

Akiwa amekumbwa na hali hii ya kipekee, Francisco aliweza kuzungumza na mtangulizi wake, ambaye, mwanzoni mwa utawala wake, alimpa "sanduku kubwa jeupe."

"Kila kitu kiko hapa. Rekodi za hali ngumu na za maumivu zaidi, unyanyasaji, kesi za ufisadi, vipengele vya changamoto, mienendo mibaya," anasema Francisco, akimnukuu Benedict, ambaye alifariki Desemba 2022.

"Nimefika hapa, nimechukua hatua hizi, nimewatoa watu hawa. Sasa ni zamu yako," aliongeza Benedict, kwa mujibu wa Francisco.

Katika kitabu chake, Papa anamtaja mtangulizi wake kama "baba na ndugu," na kusema walikuwa na "uhusiano wa kweli na wa kina, ukweli wa simulizi yoyote iliyojengwa na wale waliodai kinyume."

..

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Katika chapisho lake yake, Francisco anasimulia kwamba Papa Benedict XVI alimpa "sanduku kubwa jeupe" lililokuwa na upande wenye hadithi mbaya kuhusu Kanisa.

Zaidi ya maoni haya na mengine ya jumla, hakuna kwingine popote katika kitabu hicho Francisco alikoweka wazi yaliyomo ndani ya sanduku au kujadili kesi yoyote mahususi.

Kwa mfano, anasema kwamba mageuzi na mijadala yake na mrengo wa kihafidhina wa Kanisa Katoliki yalikuwa "magumu zaidi na yale yaliyoonesha upinzani mkubwa zaidi wa mabadiliko kwa muda mrefu."

Au anafafanua kuhusu usimamizi wa kifedha wa Vatican kwamba "umeachana na laana ambayo 'imekuwa ikitkelezwa hivi kila wakati' haikuwa rahisi, lakini sasa hatimaye tuko kwenye njia sahihi."

Kwa hali yoyote, kutajwa kwa jambo hili kulikuwa na umuhimu kwa sababu, ingawa ripoti kuhusu uwepo wa nyaraka kama hizo ilichapishwa mwaka 2013, hii ni mara ya kwanza kwa Francisco kuzungumzia suala hilo.

4. Mashambulizi mawili

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Dunia ilikuwa bado haijamaliza janga la virusi vya corona wakati Francisco aliposafiri kwenda Iraq.

Katika ziara ya kihistoria, Papa alikwenda mji wa Najaf, unaotazamwa kama kituo cha kihistoria na kiroho cha Uislamu wa Shia, ili kukutana na Ayatollah Ali Al Sistani.

Vatican ilikuwa ikijiandaa kwa mkutano huu kwa miaka mingi, na kuzingatiwa kama hatua muhimu katika mazungumzo ya kidini.

Lakini hatari zinazohusiana na usalama wa Papa, katikati ya vurugu zinazondelea kati ya Waislamu wa Shia na Sunni, zilikuwa kubwa sana kwa mujibu wa Vatican.

"Karibu kila mtu alinishauri nisiende kwenye safari hiyo, ambayo ilikuwa ya kwanza kwa Papa kwenda katika nchi hiyo ya Mashariki ya Kati iliyoathiriwa na vurugu za itikadi kali na itikadi za jihadi," anasema Francisco katika simulizi yake.

"Lakini nilitaka kuimaliza hadi mwisho. Nilihisi ni lazima nifanye hivyo," anaongeza.

Idadi ya Wakristo nchini Iraq inakadiriwa kuwa chini ya 250,000, pungufu sana kutoka milioni 1.4 kabla ya uvamizi wa Marekani mwaka 2003, kulingana na ripoti ya ya Marekani ya mwaka 2019.

..

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Papa Francisco alitembelea Iraq mwaka 2021 katika safari iliyochukuliwa kuwa ya kihistoria.

Alipowasili Baghdad, idara ya usalama ya Vatican ilimjulisha Papa Francisco kwamba Idara ya usalama ya Uingereza ilitibua majaribio mawili ya mashambulizi ya kujitoa muhanga dhidi yake.

Moja ilihusisha mwanamke aliebeba milipuko ambaye alikuwa akielekea Mosul kujilipua wakati wa ziara ya Papa.

Jingine ilihusisha gari la kubebea mizigo ambalo lilikuwa likikimbia kwa kasi kwa nia ya kujilipua njiani.

Francisco alihoji kwa namna gani walitibua mashambulizi hayo mawili.

"Kamanda alijibu kwa kifupi: 'Havipo tena,'" Francisco anasema. "Polisi wa Iraq walikuwa wamevizia na kuvilipua."

"Hilo pia lilinishangaza. Ilikuwa ni matunda yenye sumu ya vita," anasema.

5. Uhusiano wake na mwandishi maarufu wa Argentina, Jorge Luis Borges

Katika chapisho lake, Francisco anakumbuka wakati alipokutana na mwandishi maarufu wa Argentina, Jorge Luis Borges.

Wakati huo, Bergoglio alikuwa na umri wa miaka 27 na alikuwa profesa wa fasihi na saikolojia katika Shule ya Immaculate Conception iliyopo Santa Fe, katikati mwa Argentina, ambapo alifundisha kozi ya uandishi wa fasihi.

Msaidizi wa Borges alikuwa mwalimu wa kinanda wa Bergoglio, hivyo Bergoglio aliamua kumtumia hadithi mbili alizoziandika na wanafunzi wake.

Wakati huo, Bergoglio alikuwa tu kiongozi wa kidini, na Borges alikuwa tayari miongoni mwa waandishi maarufu wa Amerika ya Kusini katika karne ya 20.

Borges hakupenda tu hadithi hizo, bali alipendekeza zichapishwe kwa mfumo wa kitabu na alijitolea kuandika utangulizi: "Utangulizi huu sio kwa ajili ya kitabu hiki tu, bali kwa kila mfululizo wa kazi ambazo vijana waliokusanyika hapa wanaweza kuandika, katika siku zijazo, kwa mujibu wa Bergoglio.

...

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Bergoglio alikutana na Borges wakati akiwa mwana dini chipukizi na mwingine akiwa mwandishi aliyejitolea.

Kisha alimualika kufundisha madarasa kadhaa kuhusu kile kinachojulikana nchini Argentina kama "fasihi ya gaucho."

"Na alikubali; aliweza kuzungumza kuhusu chochote, na hakuwa na kiburi. Akiwa na umri wa miaka 66, alifanya safari ya saa nane kutoka Buenos Aires hadi Santa Fe," anasema Papa, ambaye anajitambulisha kama mpenzi wa usomaji na mwenye shauku ya kufundisha.

"Katika moja ya safari hizo, tulichelewa kufika kwa sababu, nilipokwenda kumchukua kwenye hoteli, aliniomba nimsaidie kumnyoa" anaelezea.

"[Borges] alikuwa akimuamini Mungu na kufanya sala ya Bwana kila usiku kwa sababu aliahidiana na mama yake, na kabla ya kifo chake alipokea sakramenti," anasema Francisco kuhusu mwandishi ambaye alifariki mwaka 1986.

Na anaongeza: "Nilimheshimu na kumthamini Borges sana. Niliguswa na uzito na heshima ya maisha yake. Alikuwa mtu mwenye hekima sana."